test

Ijumaa, 9 Septemba 2016

SOMA KISHA TAZAMA VIDEO KWA HABARI KAMILI:RAIS JOHN MAGUFULI APONGEZWA: KIKAO CHA DHARURA CHA EAC CHAPATA MAFANIKIO MAKUBWA.


NCHI za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zimekubaliana kuendelea na majadiliano kwa miezi mitatu mpaka Januari mwakani kuhusu kusaini mkataba wa ushirikiano wa kibiashara na Umoja wa Ulaya (EPA).
Aidha, jumuiya hiyo imeutaka Umoja wa Ulaya kuacha kuiadhibu Kenya kutokana na kutosaini mkataba huo ifikapo Oktoba mosi mwaka huu kwa kuanza kuwatoza ushuru katika mazao ya maua na mboga.
Maamuzi hayo yamefikiwa na viongozi wa nchi mwanachama wa jumuiya hiyo katika Kikao Maalumu cha 17 cha Jumuiya hiyo, kilichofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Naibu Rais wa Kenya, William Rutto, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Burundi, Balozi Alain Nyamitwe, Mwakilishi kutoka Sudan Kusini, Aggrey Sabuni na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Rais John Magufuli alisema katika kikao chao walichokaa, wamelijadili suala hilo kwa muda mrefu na lilikuwa gumu.
“Lakini kama ilivyo kawaida ya jumuiya hiyo kushauriana katika jambo gumu linapotokea na kupata suluhisho na kama hawajapata ufumbuzi wa pamoja hutafuta njia muafaka kupata ufumbuzi wa amani hata katika masuala ambayo ni magumu,” alisema Rais Magufuli.
Alisema mpaka kufikia Januari mwakani watakuwa wamefikia uamuzi kamili kwa jumuiya nzima na siyo nchi moja moja na sasa wanaandaa njia ya kushughulikia kwa kuitaka Sekretarieti kuandaa utaratibu wa mahusiano yanayohusu suala hilo na kuwasiliana na EU.
Alisema wamefikia uamuzi huo kutokana na mambo kadhaa yaliyotaka ufumbuzi wa pamoja ikiwemo kulinda na kukuza viwanda baada ya kuanza kuingia bidhaa baada ya kusaini na EU.
"Tanzania tulisita kusaini kwani tumejipanga kujenga viwanda vyetu hivyo vinaweza kushindwa kupambana na vile vya Ulaya ambavyo ni vikongwe,” alisema.
Alizungumzia masuala mengine yanayohitaji muda kujadili kuwa ni pamoja na kulinda bidhaa za kilimo ambazo ni katika nchi za Ulaya wakulima wanapewa ruzuku na wanazalisha bidhaa bora pamoja na usafirishaji wa bidhaa ghafi.
Alisema pia wanahitaji kuzungumzia Burundi, ambayo watawezaje kusaini mkataba huo wakati wamewekewa vikwazo pamoja na suala la Uingereza kujitoa katika Umoja wa Ulaya huku wakitafuta nchi za Afrika Mashariki kujiunga na umoja huo.
Aidha, wanaangalia makusanyo ya kodi kwa bidhaa kutoka nje ambayo Tanzania watapoteza asilimia 45 ya kodi za bidhaa kutoka nje Ulaya kwa miaka 20 ikiwa itasaini mkataba huo.
Katika mkutano huo, Sudan Kusini ilihudhuria kwa mara ya kwanza kama mwanachama kamili huku akiteuliwa na kuapishwa kwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Christopher Bazibhano kutoka Burundi.
Rais Museveni akizungumza katika mkutano huo, aliutaka Umoja wa Ulaya usikasirike kwa maamuzi hayo, bali wawape muda ili kujadili mkataba huo kwa maslahi ya nchi za jumuiya hiyo na kutoka na msimamo wa pamoja.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx