WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka Maafisa Elimu wahakikishe wanafunzi
wanaoshiriki mashindano hayo ni wale waliovuka katika ngazi ya shule,
kata, wilaya na mkoa, ambao wote ni wanafunzi halali wa shule na
marufuku kuchezesha mamluki.
“Endapo
itabainika yupo mchezaji aliyeletwa kushiriki michezo hii ambaye si
mwanafunzi (yaani mamluki) naagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya
wahusika kwa kuzingatia kanuni na sheria za mashindano haya,”
amesisitiza.
Waziri
Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa ametoa agizo hilo
jana (Jumamosi, Juni 9, 2018) wakati akifunguaMashindano ya Umoja wa
Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi na Sekondari Tanzania
yanayofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Pia,
Waziri Mkuu amewataka viongozi wa mikoa na wilaya zote nchini
wahakikishe kuwa masomo ya haiba, michezo na stadi za kazi yanafundishwa
kikamilifu kwenye shule zote za msingi.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema somo la elimu ya michezo kwa Shule za
Sekondari nalo lifundishwe kikamilifu na vyuo vya michezo kama Malya
viendelee kuwaendeleza walimu wa michezo.
Amesema
utafiti na ubunifu wa kuendeleza michezo nchini ni jambo linalohitaji
kupewa msukumo wa pekee, ambapo ameviasa vyama vya michezo na asasi za
sanaa zijihusishe na ukuzaji wa michezo shuleni, bila kuathiri taratibu
za shule.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaagiza Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya
wahakikishe maeneo ya michezo na burudani yanapimwa na yasiingiliwe,
pia vitengo vya michezo kwenye ofisi za Halmashauri na Mikoa vitengewe
fedha za kuendeshea michezo.
Amesema
pamoja na manufaa yatokanayo na michezo, kiwango cha michezo nchini si
cha kuridhisha, hivyo ni vema kujenga msingi wa kupata matokeo mazuri
kwa kuwa na viwanja vyenye viwango vinavyokubalika, walimu wenye
utaalamu wa michezo na vifaa.
“Inawezekana
kuna sababu za msingi, lakini ni lazima tuhakikishe kuwa vijana kuanzia
Shule za Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo wanatengenezewa mazingira
mazuri ikiwa ni pamoja na kupewa fursa za kucheza na kushindana miongoni
mwao,” amesema.
Amesema
kutokana na hali hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais
Dkt. John Magufuli kupitia shule za msingi na sekondari, itahakikisha
walimu waliosomea michezo wanapata ajira ili waendeleze vipaji vya
vijana nchini.
Waziri
Mkuu amesema vipaji vya michezo na sanaa vitaitangaza nchi kimataifa na
kuongeza fursa ya ajira kwa Watanzania. Amesema kauli mbiu ya michezo
ya UMISSETA na UMITASHUMTA ya mwaka huu ni “michezo, sanaa na taaluma
ni msingi wa maendeleo ya mwanafunzi katika Taifa letu”.
Amesema
kauli mbiu hiyo inawataka wanafunzi wajihusishe na michezo na sanaa
kama sehemu ya taaluma, ambapo wataweza kuonesha vipaji vyao ambavyo
vikiendelezwa vema vitawapatia manufaa ikiwemo afya, matokeo mazuri ya
kitaaluma na ajira.
Pia
amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella na wananchi wote
kwa kukubali kuwa wenyeji wa mashindano hayo kwa mara ya tatu mfululizo,
pamoja na kampuni ya COCA COLA kwa kudhamini michezo ya mpira wa miguu
na kikapu kwa Shule za Sekondari na kampuni ya AZAM kwa kujitolea
kuonesha michezo hiyo kwa mwaka huu.
Aidha,
amewataka wanafunzi wanaoshiriki mashindano hayo watumie ushiriki wao
kwa kuuthibitishia umma dhamira waliyonayo ya kuonesha kuwa, zipo fursa
nyingi za ajira endapo vipaji vya michezo na sanaa vitatumika
kikamilifu.
Amesema
mashindano kama hayo yanatoa fursa kwao kuonesha uwezo wao na kuonekana
kwa wadau mbalimbali wanaoweza kuwaendeleza. “Si hivyo tu, uwepo wenu
hapa unawapa fursa ya kutambua uwezo mlionao pamoja na kujiwekea
malengo na mwelekeo wa maisha yenu ya baadaye,”.
Amesema
uhalali wa michezo na mashindano shuleni unatajwa katika Ilani ya
Uchaguzi ya CCM ya 2015-2020, Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka
1995, Sera ya Elimu ya mwaka 2014 ambazo kwa pamoja zinaelekeza
kutambua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi shuleni kufikia malengo ya
maendeleo endelevu.
Mashindano
hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri waNchi, OR – TAMISEMI, Joseph
Kakunda, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana
Shonza, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella pamoja na viongozi
mbalimbali wa Serikali, Wadhamini wa Mashindano hayo, Wadau wa michezo
na baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mwanza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 comments:
Chapisha Maoni