Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ametoa rai
kwa wawekezaji wazawa na wafanyabiashara nchini kujenga viwanda vya dawa
na vifaa vya tiba hapa nchini ili kuongeza kasi ya ujenzi wa uchumi wa
viwanda na kukuza ajira.
Rais
Magufuli ametoa rai hiyo jana Jijini Dar es Salaam, kwenye hafla ya
uzinduzi wa magari 181 yenye thamani ya shilingi bilioni 20.7 ya
kusambaza dawa na vifaa vya tiba yaliyotolewa msaada na Shirika la
Global Fund kwa Serikali ya Tanzania kupitia Bohari ya Dawa (MSD).
“Asilimia
94 ya dawa zinanunuliwa nje ya nchi, hivyo wawekezaji wazawa watumie
changamoto hii kama fursa ya kuanzisha viwanda vya dawa na vifaa tiba
hapa hapa nchini kwetu,” alisema Rais Magufuli.
Rais
Magufuli alibainisha kuwa ujenzi wa viwanda hapa nchini utasaidia
kuongeza ajira kwa Watanzania hasa vijana pamoja na kupunguza gharama za
kuagiza bidhaa nje ya nchi zikiwemo dawa na vifaa vya tiba.
Aidha
Rais Magufuli alitoa wito kwa wataalamu na wasomi wazawa wa masuala ya
afya na tiba kujiunga pamoja na kuanzisha viwanda vya dawa ili kuchochea
uchumi wa viwanda na kuongeza mapato.
“Tunapoteza
shilingi bilioni 500 kila mwaka kwa ajili ya kununua dawa nje ya nchi
lakini tungekuwa na viwanda vyetu fedha hizo tungetumia kwenye mambo
mengine ya maendeleo,” alisisitiza Rais Magufuli.
Pia
Rais Magufuli alisisitiza kuwa madereva watakaoajiriwa kuendesha magari
hayo mapya wachaguliwe kwa umakini ili kupata watu waaminifu
watakaoweza kuyatunza kwa manufaa ya Watanzania.
Bohari
ya Dawa Tanzania (MSD) ilianzishwa mwaka 1994 kwa ajili ya kununua,
kuhifadhi na kusambaza dawa na vifaa vya tiba nchini kote.
0 comments:
Chapisha Maoni