MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali maombi ya kufutwa
kwa shitaka la utakatishaji fedha katika katika kesi ya kuisababishia
serikali hasara ya Sh bilioni 14 inayomkabili, mfanyabiashara Mohammed
Yusufali ‘Choma’ na mwenzake.
Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri alitoa uamuzi huo jana baada ya
kupitia hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili katika kesi hiyo.
Kutokana na uamuzi huo, washitakiwa wataendelea kusota rumande hadi kesi itakapokwisha kwa kuwa kisheria mashitaka ya utakatishaji wa fedha hayana dhamana.
Kutokana na uamuzi huo, washitakiwa wataendelea kusota rumande hadi kesi itakapokwisha kwa kuwa kisheria mashitaka ya utakatishaji wa fedha hayana dhamana.
Katika kesi hiyo Choma aliyewahi kutajwa kujipatia Sh milioni saba
kwa dakika moja kwa njia ya udanganyifu katika mapato ya serikali,
pamoja na mfanyabiashara Samuel Lema, wanakabiliwa na mashitaka 222 ya
kula njama, kutakatisha fedha, na kuisababishia serikali hasara hiyo kwa
kukwepa kulipa kodi.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mashauri alisema Mahakama imetupilia mbali
maombi hayo yaliyowasilishwa na upande wa utetezi kwa kuwa haina mamlaka
ya kusikiliza shauri hilo.
Alisema mahakama inakubali kuwa hati ya mashitaka inayowahusu
washitakiwa hao haina makosa, hivyo Mahakama haiwezi kubadili hati hiyo
kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Aidha aliongeza kuwa, kama upande wa utetezi ungekuwa na nia ya
kutaka kufutwa kwa shitaka hilo ungewasilisha maombi hayo tangu awali.
Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 18, mwaka huu kwa
ajili ya kutajwa.
Katika hoja za ombi hilo, Wakili wa utetezi Alex Mgongolwa aliomba
shitaka hilo kufutwa kwa kuwa lina mapungufu kisheria na kuongeza kuwa
si kila kosa la wizi na kughushi ni utakatishaji fedha, bali makosa
yanayofuata baada ya vitendo hivyo yaani kuficha chanzo au asili ya
upatikanaji wa fedha hizo ndiyo kosa la utakatishaji.
Alidai maelezo ya kwenye shitaka la 221 hayajengi kosa la
utakatishaji fedha hivyo aliiomba mahakama ifute shitaka hilo ili
waendelee na mashitaka mengine.
Upande wa Jamhuri uliiomba mahakama itupilie mbali ombi hilo kwa kuwa
halina msingi kisheria na shitaka hilo lina maelezo ya kutosha kujenga
kosa la utakatishaji wa fedha.