Siku chache baada ya Polisi
wa Dar es Salaam kutangaza kumsaka mmiliki wa iliyokuwa kliniki ya tiba
asilia ya Foreplan, Juma Mwaka ‘Dk Mwaka’ kwa agizo la Naibu Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis
Kigwangallah, tabibu huyo ameamua kujisalimisha polisi.
Dk Kiwangallah
alitoa agizo hilo siku sita zilizopita baada ya kutembelea kliniki hiyo
kwa mara ya pili. Dk Mwaka alijisalimisha jana saa nne asubuhi katika
Kituo cha Kikuu cha Polisi, jijini Dar es Salaam na kuhojiwa kwa saa
kadhaa kabla ya kuachiwa kwa dhamana.
Msako wa Dk Mwaka unachagizwa na
madai ya ukiukwaji wa agizo la Serikali la kuendelea na utoaji wa tiba
licha ya kufungiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Salum
Hamdani alisema jana kuwa baada ya kujisalimisha muda huo, alihojiwa na
kuachiwa kwa dhamana lakini akatakiwa kuripoti leo kwa mahojiano zaidi.
“Kuhusu kupelekwa mahakamani, ni mpaka jeshi la Polisi litakapomaliza
kukusanya ushahidi na kumkabidhi DPP ambaye atautumia kufungua kesi,”
alisema.