Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya kuimarisha huduma za afya Tanzania (THPS)
akimkaribisha Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo alipowasili kufungua
mkutano wa wadau wa mapambano ya ukimwi Hoteli ya Zanzibar Beach Resort
Mbweni.
Waziri
wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akifungua mkutano wa wadau wa mapambano ya
ukimwi Zanzibar katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni.
Waziri
wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akizindua Mpango Mkakati wa miaka mitano
wa THPS katika mkutano wa wadau wa mapambano ya ukimwi uliofanyika
Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mbweni, anaeshirikiana nae katika
uzinduzi huo ni Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Redempta Mbatia.
Mshiriki
wa mkutano wa wadau wa mapambano dhidi ya ukimwi kutoka Jumuia ya
Maimamu Zanzibar Muhiddini Zubeir akitoa mchango wake katika mkutano
huo.
Mkurugenzi
Mtendaji wa THPS Dkt. Redempta Mbatia akizungumza na wadau wa mapambano
ya ukimwi Zanzibar katika mkutano wa siku moja uliofanyika Hoteli ya
Zanzibar Beach Resort Mbweni.
Muhudumu
Mkuu wa huduma za mama na mtoto na huduma za upimaji vvu kwa jamii
kutoka Hospitali ya Mwembeladu Mwanakhamis Alawi Nguzo akipokea zawadi
maalum kutoka Waziri wa afya baada ya kuwa kituo bora katika mapambano
ya ukimwi kipindi cha miezi mitatu Octoba – Disemba.
Mkurugenzi wa Idara ya Kinga na
Elimu ya Afya Zanzibar Dkt. Fadhil Abdalla kifunga mkutano wa wadau wa
mapambano ya ukimwi ulioandaliwa na Taasisi ya THPS katika Hoteli ya
Zanzibar Beach Resort Mbweni.
Picha na Makame Mshenga.
Na Ramadhani Ali-Maelezo Zanzibar.
Taasisi
zinazojishughulisha na mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya
ukimwi (VVU) na ukimwi Zanzibar zimetakiwa kuelekeza nguvu katika
makundi maalum ambayo maambukizi bado ni makubwa.
Waziri wa Afya
Mahmoud Thabit Kombo alitoa ushauri hao alipokuwa akifungua mkutano wa
siku moja wa wadau wa mapambano ya ukimwi uliotayarishwa na Taasisi ya
kuimarisha huduma za afya Tanzania (THPS) na kuzindua mpango mkakati wa
miaka mitano wa taasisi hiyo katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort
Mbweni.
Alisema wakati
Zanzibar inajivunia kuwa na asilimia chini ya moja ya maambukizi ya VVU,
katika makundi maalumu maamukizi yapo kwa asilimia 10 hadi 19 ambapo ni
hatari.
Aliyataja makundi
hayo kuwa ni vijana wanaojidunga sindano za madawa ya kulevya, wanawake
wanaofanya biashara ya ngono na wanaume wanaofanya ngono na wanaume
wenzao.
Alisema kunapokuwa na kikundi kidogo cha watu wenye hali kubwa ya maambukizi ya VVU hatari ya maambukizi inaelekea kwenye jamii.
“Makundi maalum
yanaonekana kuwa ni daraja la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutoka
kwao kuja kwenye jamii, ”alisisitiza Waziri wa Afya.
Aliongeza kuwa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeridhia kuyafanyia kazi malengo ya
dunia ya kutokomeza kabisa maambukizi ya VVU ifikapo mwaka 2030 hivyo
mashirikiano zaidi yanahitajika katika kufikia malengo hayo.
Hata hivyo
alieleza kuwa ushiriki wa wananchi katika kupima VVU bado hauridhishi na
wale wanaopima na kubainika na maambukizi wengi wao hawajiungi kwenye
huduma za tiba na wachache wanaotumia dawa hawazitumii ipasavyo.
Waziri wa Afya
alikumbusha kuwa wakati huu ambapo Zanzaibar inatekeleza Mpango wa
kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa
ujauzito lakini wanaume hawajitokezi kupima afya zao.
“Akinababa
tuwasindikize wake zetu kliniki ili na sisi tupimwe Virusi vya ukimwi,
hivi sasa tupo chini ya asilimia tano wakati wenzetu Tanzania Bara
wamefikia asilia 80, “Waziri Mahmoud alihimiza.
Mkurugenzi
Mtendaji wa THPS Dkt. Redempta Mbatia alisema katika kupambana na ukimwi
Zanzibar, taasisi hiyo imekuwa ikiwajengea uwezo wafanyakazi wa afya na
taasisi nyengine zinazoshiriki katika mapambano hayo.
Aidha alisema
wamekuwa wakisaidia masuala ya uongozi pamoja kuimarisha utawala bora na
kusaidia vifaa tiba katika Hospitali na vituo vya afya ili kuhakikisha
huduma za afya zinakuwa endelevu na kufikia malengo yaliyowekwa.