Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amemtaka Rais Dk. John Magufuli,
kutafakari hatima ya masheikh wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya
Kiislamu Zanzibar (Jumuki) maarufu ‘Uamsho’ wanaosota gerezani kwa miaka
minne sasa bila kesi yao kuamuliwa.
Masheikh
hao ambao wamefunguliwa kesi ya ugaidi, awali kesi yao ilikuwa
ikiendeshwa katika Mahakama Kuu ya Zanzibar na baadaye kuhamishiwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam inakoendelea
hadi sasa.
Lowassa,
alisema ni jambo la fedheha kwa nchi iliyopata uhuru zaidi ya miaka 50
kuwaweka mahabusu viongozi wa dini muda mrefu kiasi hicho bila kesi
kusikilizwa mahakamani.
Lowassa
ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), aliyasema hayo juzi alipokuwa akizungumza kwenye futari
iliyoandaliwa na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema).
Alisema
kama masheikh hao wamefanya makosa wapelekwe mahakamani ili haki
itendeke lakini kuendelea kuwashikilia ni fedheha kubwa kwa Taifa.
Waziri
Mkuu huyo wa zamani alisema kama ambavyo Rais Dk. John Magufuli,
ametekeleza ahadi ya vyama Vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) kwa kuunda Tume mbili za kushughulikia madini ya dhahabu, hana
budi kutekeleza na ahadi yake (Lowassa) kuwatoa kizuizini masheikh hao
wa Uamsho.
“Nilipokuwa
nagombea urais, nilizunguka nchi nzima nikiahidi kuunda tume ya
kuchunguza madini ya dhahabu, bahati mbaya kura zetu walizihesabu vibaya
na kutunyima kura zetu, sasa niliposikia bwana mkubwa kaunda tume
nikasema naam… Rais ameanza kutekeleza ahadi yetu ya Ukawa.
“Sasa
nimwombe aangalie na hili la masheikh wetu, sisemi kwamba hawana
makosa, lakini kuwaweka ndani miaka minne bila kesi kuamuliwa ni fedheha
kwetu na kwa Serikali pia.
“Nchi
gani hii, ina uhuru wa miaka 50, watu wako tena waumini wa dini
wanawekwa ndani bila kesi, kwa sababu ya tofauti ya kiitikadi, tuwaombee
masheikh wetu wale watoke, lakini na nyinyi masheikh mliopo hapa
zungumzeni mfanye nini, msiwe baridi sana, pengine kuna lugha
watakayoweza kuwasikia,” alisema Lowassa.
Akizungumzia
suala la kuenzi amani ya nchi aliwataka waumini wa dini ya Kiislamu
wanapotafakari mambo mbalimbali kupitia mwezi Mtukufu wa Ramadhan
wakemee jambo hilo ambalo alisema linavurugwa na chuki zikiwamo za
kisiasa.
Awali
Imamu Mkuu wa Msikiti wa Gongolamboto na Amiri wa Shura ya Maimamu
Wilaya ya Ilala, , Sheikh Hassan Abbas, alimwomba Mbunge Waitara
kupeleka kilio chao bungeni kuhusu viongozi hao wa dini wanaosota
gerezani bila kesi yao kuamuliwa.
“Nimshukuru
Mbunge kwa kutambua katika eneo lake kuna kada mbalimbali za viongozi
kujumuika pamoja kuelekea sikuu zetu hizi baada ya Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani.
“Lakini
kuna jambo linatuuma sisi waislam, wakati tunaelekea kula sikuu wenzetu
wako mahabusu, kwakweli jambo hili linatuuma sana na tunaomba
utufikishie kero hii huko bungeni,” alisema Sheikh Abbas.
Kwa
upande wake, Waitara alisema juzi ilikuwa siku maalum ya kujumuika
pamoja kula futari na kwamba baada ya kumaliza vikao vya Bunge Julai 2,
mwaka huu atakaa nao na kujadili kwa undani kero mbalimbali za wananchi.
“Tunatarajia
kumaliza Bunge la Bajeti kati ya Julai 2 au 3, kimsingi nina mambo
mengi nitakuja tujadiliane, kuna sheria ambayo imepitishwa juzi bungeni,
faini ya utupaji taka ovyo imepanda kutoka 50,000 za awali hadi 200,000
na milioni 1,000,000.
“ Na kwa wenzetu washereheshaji (MC’s) na mama lishe kuanzia sasa wataanza kulipa kodi. Haya mambo muwe nayo makini,” alisema Waitara.
==>Msikilize hapo chini akiongea
==>Msikilize hapo chini akiongea
0 comments:
Chapisha Maoni