test

Ijumaa, 24 Juni 2016

Waliokula fedha za watumishi hewa waendelee kusakwa kila kona


Map of Tanzania
RAIS John Magufuli wakati akiwahutubia wafanyakazi katika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi mkoani Dodoma, aliwatangazia neema watumishi wanaopokea mshahara wa kima cha chini.

Neema hiyo ni ile ya kushusha Kodi ya Mshahara (PAYE) kwa wafanyakazi kutoka asilimia 11 ya sasa hadi tisa na hii itaanza mwaka wa fedha kwa 2016/2017. Hili ni jambo jema na la kumpongeza Rais Magufuli kwa kuwakumbuka wafanyakazi wa kada ya chini, ambao kimsingi ndio watendaji wakubwa katika maeneo mengi ya kazi.
Kada hii inayopokea mshahara wa kima cha chini kuanzia Sh 170,000 hadi Sh 360,000, ndio wengi, si tu katika taasisi na mashirika ya umma, bali hata katika sekta binafsi wapo wengi.
Ijapokuwa kima hicho cha chini cha mshahara hakitoshi hasa kwa mtumishi anayeishi katika miji mikubwa kama Dar es Salaam na Arusha, ambako maisha ya kila siku ni ghali kuliko mahala pengine popote, naamini wapo waliofarijika maana asilimia hiyo mbili inayorudi katika mshahara wao, itatosha japo nauli ya mtoto kwenda shule.
Taasisi na mashirika hayo ambayo Watanzania hawa wanafanya kazi, naamini nao kwa upande wao watafikiria kada hii na kuwapa nyongeza kidogo walau kupunguza machungu ya maisha, ambayo kwa uhakika ni makubwa mno.
Lakini Rais amewataka wafanyakazi nchini, kufanya kazi kwa bidii na weledi na kuepuka ubadhirifu na vitendo vya rushwa katika maeneo yao ya kazi. Jambo ambalo binafsi ningependa kulizungumza hapa ni hili la watumishi hewa.
Watumishi hewa ni tatizo kubwa, ambalo kusema ukweli limekuwa likimaliza fedha nyingi za serikali, ambazo huishia katika mifuko ya wajanja wachache. Hadi mwanzoni mwa Mei ilibainika kuwa kulikuwa na watumishi hewa 10,295, kati yao watumishi 8,373 ni wa Tamisemi na 1,922 wa Serikali Kuu.
Hao wote walikuwa wakilipwa fedha nyingi, ambazo zingeweza kurekebisha maslahi ya wafanyakazi halali na kutekeleza miradi ya maendeleo. Hata hivyo, kwa sasa idadi hiyo ya watumishi hewa imeongezeka hadi kufikia 12,000.
Rais Magufuli alisema watumishi hewa walikuwa wakilipwa kila mwezi zaidi ya Sh 11,603,273,799.41 na kwa mwaka wamelipwa zaidi ya Sh 139,239,239,285.92 na ukizidisha malipo hayo kwa miaka mitano utapata Sh 696,196,427,964.6 ambazo zililipwa kwa watumishi hao hewa.
Tukiangalia kwa undani, tunaona jinsi ambavyo fedha hizo nyingi zilikuwa zinaishia kwenye mifuko ya walafi na mafisadi wachache, ambao walikuwa wanatumikisha watumishi wengine na wao kufaidika.
Naamini watumishi hao wapo ambao waliandikiwa barua za kufukuzwa kazi kwa makosa mbalimbali ya kusingiziwa na mwisho wa siku hao wanaowafukuza, huamua kutumia mishahara yao hiyo.
Kwa hakika watu hao si wazuri kutokana na roho zao hizo za ubinafsi. Lakini kwa kuwa mamlaka zinazohusika hasa Rais na vyombo vyake vya utawala, vimebaini kuwapo kwa watumishi hewa katika ofisi nyingi za umma na Serikali Kuu, ni vyema wachukuliwe hatua kali za kisheria ili kutoa fundisho kwa watumishi wote ambao wanaiba fedha hizi za umma kwa njia hiyo.
Mtandao huu ni mkubwa na lazima utakuwa unahusisha kwa namna moja ama nyingine watu wengi katika ofisi, kama wahasibu, mameneja rasilimali watu na wakaguzi wa ndani. Jambo wanalotarajia Watanzania wengi ni kuona wote waliokuwa wakifaidi mishahara hewa, wanaendelea kusakwa kila kona na kukamatwa na kisha wafikishwe mahakamani.
Mwito wangu kwa watumishi wengine waliopo kazini katika sehemu mbalimbali ni kuwa wafanye kazi kwa bidii na kuleta maendeleo kwa taifa na kuisaidia Serikali katika kuinua uchumi wa Taifa na kuboresha maisha ya wananchi.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx