MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, hawakutokea kwenye mkutano ulioandaliwa na Tume ya Haki na Utawala Bora jijini Dar es Salaam jana.
Mkutano uliokuwa na lengo la kumaliza mvutano ulioibuka kati ya vyombo vya dola na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mvutano
huo unatokana na amri ya Rais John Magufuli, ya kupiga marufuku
kufanyika kwa maandamano na mikutano ya vyama vya siasa hadi mwaka 2020.
Rais
Magufuli, hata hivyo, ameruhusu viongozi waliochaguliwa kama madiwani
na wabunge kufanya mikutano kwenye maeneo waliyopigiwa kura.
Kupinga
amri hiyo, Chadema kimeamua kuitisha maandamano na mikutano ya
wanachama na wafuasi wao nchi nzima yatakayofanyika, Septemba mosi,
mwaka huu katika operesheni waliyoipa jina la `Umoja wa Kupinga Udikteta
Tanzania’ (Ukuta).
Baada
ya kuibuka kwa mvutano huo, uliosababisha Mwanasheria Mkuu wa Chadema,
Tundu Lissu kukamatwa na Jeshi la Polisi na kufunguliwa mashtaka ya
uchochezi, tume hiyo iliwaita IGP Mangu, Kinana, Masaju, Msajili wa
Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Katibu Mkuu wa Chadema, Vincent
Mashinji na Mkurugenzi wa Taasisi ya Demokrasia (TCD), Daniel Loya.
Hata hivyo, IGP Mangu, Kinana na Masaju hawakuhudhuria mkutano huo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa walitoa udhuru.
Mwenyekiti
wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga, alisema
jijini jana kuwa wametoa mapendekezo matatu ambayo yanapaswa kufuatwa na
pande zote zinazovutana.
Alisema mapendekezo yao yamelenga kutoa nafasi kwa mahakama kuamua kesi zilizofunguliwa.
Nyanduga
aliyataja mapendekezo hayo kuwa ni Jeshi la Polisi na Chadema kusitisha
matumizi ya lugha au maneno yenye viashiria vya uvunjifu wa amani, haki
za binadamu na utawala bora kwa kuwa lugha hizo hazikidhi matakwa ya
sheria.
Alisema
wamependekeza Jeshi la Polisi linapaswa kutokutumia maneno
"tutawashughulikia wote watakaokaidi amri" kwa kuwa tume inaamini kuwa
matumizi ya maneno hayo yanaweza kusababisha matumizi mabaya ya mamlaka
ya jeshi hilo.
“Ni
katika mazingira haya, tume imepata wasiwasi kuwa endapo matamko haya
yataachiwa yaendelee, yana viashiria vya machafuko na uvunjifu mkubwa wa
haki za binadamu unaoweza kutokea,” alisema Nyanduga.
Alisema
pendekezo lingine ni Chadema kurekebisha msamiati wa mikutano
wanayopanga na kuondoa neno udikteta katika mikakati yao ya kisiasa.
Akifafanua
kuhusu pendekezo hilo, Nyanduga alisema Tanzania ni nchi yenye taasisi
za kidemokrasia na inaheshimu utawala wa sheria na ndiyo sababu Chadema
wamekwenda mahakamani.
Alisema
Chadema na Jeshi la Polisi wanapaswa kuheshimu mahakama na kuacha kutoa
matamko ambayo yanaendelea kuongeza joto kuhusu uwapo au kutokuwapo
maandamano na mikutano ya Septemba Mosi, mwaka huu.
Nyanduga
alisema pendekezo la tatu ni Chadema kusitisha maandamano yake ili
kutoa nafasi kwa mahakama kufanya kazi yake kwa umakini bila shinikizo
la muda kuanzia sasa hadi Septemba Mosi.
Alisema
kutozingatiwa kwa mapendekezo hayo kutasababisha kutokea kwa uvunjifu
wa haki za binadamu na jambo hilo likitokea, wahusika wote
watawajibishwa.
Alisema
tume ina mamlaka ya kujadili hoja hizo mbili kwa kuzingatia mamlaka
iliyonayo chini ya Ibara 130 (1) (g) na (h) ya Katiba ya nchi, kuhusu
kutoa ushauri na kutafuta maelewano kati ya viongozi wa serikali na
Jeshi la Polisi kwa upande mmoja na uongozi wa Chadema.
Nyanduga
aliongeza kuwa mkutano wa jana ulikuwa na lengo la kuzungumzia tamko la
Jeshi la Polisi la kuzuia mikutano na maandamano ya vyama vya siasa
isiyo ya kiutendaji na tamko la Chadema kuhusu Ukuta.
“Ofisi
ya AG, IGP na CCM tuliwaalika, lakini walitujibu kuwa hawataweza
kuhudhuria kwa kuwa wana udhuru, hivyo tulikutana na Chadema, Ofisi ya
Msajili na TCD (Kituo cha Demokrasia Tanzania), na kukubaliana
kutafanyika kikao kuhusu umuhimu wa kudumisha amani nchini,” alisema Nyanduga.
Julai
27, mwaka huu, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitangaza
kuzinduliwa kwa Operesheni Ukuta kwa lengo la chama hicho kufanya
mikutano nchi nzima ifikapo Septemba Mosi mwaka huu, baada ya amri ya
Rais Magufuli na Jeshi la Polisi kuzuia kufanyika kwa mikutano ya
kisiasa na maandamano nchini.
Mashinji Afunguka
Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk. Mashinji, alipotafutwa ili kueleza juu ya
mapendekezo ya tume, alisema anashangaa kuambiwa kwamba kuna masuala
yaliyojadiliwa kwa kuwa kikao hakikufanyika jana.
“Mbona hicho kikao hakijafanyika? "alihoji.
"Kulikuwa na mvutano kwamba kifanyike ama kisifanyike kwa sababu akidi
haikutimia, nashangaa kusikia kuna maazimio yamepitishwa.
“Hiyo
inaonyesha kabisa ni njama za hao watu ili ionekane kuna kikao
kilifanyika, kikao kisingeweza kufanyika kwa sababu hawakuwapo Kinana,
IGP, wala AG,” alisema Dk. Mashinji.
Alisema
anachojua yeye ni kwamba, wao wanaendelea kama kawaida na maandalizi
yao ya mikutano ya hadhara na maandamano nchi nzima hiyo Septemba 1,
mwaka huu.