test

Jumanne, 12 Mei 2015

Watuhumiwa wa UGAIDI Wagoma Kula Gerezani .....Watoa siku Saba Kesi Yao Isikilizwe, Vinginevyo Watafanya Wanavyojua Wao


Jungukuu leo
KIONGOZI wa Uamsho na Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, Sheikh Faridi Hadi Ahmed na wenzake 22 wanaokabiliwa na tuhuma za ugaidi wamegoma kula  gerezani.

Washtakiwa hao wamegoma kula na wamedai mahakamani kwamba hata waitwe wahaini hawawezi kugeuza madai yao ya kutaka Zanzibar ipate mamlaka yake kamili.

Hayo yalidaiwa jana na washtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi, Renatus Rutta, wakati kesi yao ilipokuwa inatajwa.

Upande wa Serikali ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Janeth Kitali ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo ukaomba kesi iahirishwe  huku ukisubiri kumbukumbu za mahakama kwa ajili ya kukata rufaa.

Mshtakiwa Sheikh Farid, alidai chanzo cha kushtakiwa katika kesi hiyo ni madai yao katika mchakato wa katiba ya kuhakikisha Zanzibar inapata mamlaka sahihi.

“Sisi wote ni viongozi wa jumuiya, baada ya yote hayo ndiyo misukosuko ikaanza kwetu, kesi ya ugaidi ni bandia, madai yetu hatuwezi kuyageuza hata watuite wahaini.

“Tulifanyiwa mambo mengi ya ukatili, sisi tunadai heshima ya nchi yetu, tulitamka wazi hatutaki Muungano tunataka Rais wetu apewe heshima yake kama Rais wa Zanzibar,” alidai.

Alidai hawana ajenda ya siri, walifanya mihadhara zaidi ya 200 na walitakiwa kushtakiwa Zanzibar kwa hiyo kutengeneza mazingira hayo ni kutaka kuwadhulumu haki zao.

Sheikh Faridi alidai  Serikali iliyopo madarakani imezeeka na ni kikongwe.

Mshtakiwa huyo na wenzake 22 waliomba siku saba kesi yao isikilizwe na endapo zitaisha hatua watakayochukua itaonekana.

Alisema  hawawezi kukubali kudhulumiwa  huku wakikaa kimya.  Walimtaka Kamishna wa Zanzibar ajieleze kwa nini aliamua kuwaleta Tanzania Bara kuwashtaki.

Hakimu Rutta alisema ni haki kwa waliopo gerezani kutembelewa, waliogoma kula waambiwe wale kwa sababu rai yake ni kutaka wafike mahakamani na  wanafuatilia kwa karibu.

Baada ya Hakimu kusema hayo kesi iliahirishwa hadi Mei 25  mwaka huu.
 
Mshtakiwa Salum Ally  aliomba wapigwe risasi kichwani wamalizwe kwa sababu wamechoka.

Washtakiwa hao wanadaiwa kula njama kufanya ugaidi, kuwawezesha watu kufanya ugaidi na kuwahifadhi magaidi. 
 
Uhalifu huo unadaiwa ulifanyika sehemu mbalimbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni