Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo
Jumatatu Januari mbili, 2017 amemaliza ziara yake ya siku mbili Mkoani
Kagera kwa kuwatembelea baadhi ya wananchi walioathiriwa na tetemeko la
ardhi pamoja na kukagua baadhi ya miundo mbinu iliyoathiriwa na tetemeko
hilo na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo ya shule ya
sekondari ya Ihungo Omumwani iliyobomolewa na tetemeko la ardhi la
Septemba 10,2016.
Mara
baada ya ukaguzi huo Rais Dkt Magufuli akazungumza na wananchi wa Mkoa
huo wa Kagera katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Ihungo na kuagiza
kuvunjwa kwa kamati ya maafa ya Mkoa huo iliyokuwa ikiratibu utoaji wa
misaaada na kufanya tathmini ya athari ya tetemeko hilo.
”Kila
kitu huwa kina mwanzo na mwisho wake ukiwa na harusi huwa kuna kamati
ya harusi,ukishamaliza kufunga ndoa kamati ya harusi huwa inavunjwa,na
ukiwa kwenye msiba huwa kuna kamati ya msiba na msiba mkishazika kamati
ya mazishi huvunjwa,kamati ya maafa ya Kagera huu ni mwezi wa tano na
inawezekana hata kwenye kamati huwa wanalipana posho,sasa nataka hii
kamati nayo iishe,yalishapita yamepita”
Aidha
Dkt Magufuli amewataka wote walioahidi kuchangia katika kamati ya
tetemeko la ardhi ya mkoa wa Kagera ambao bado hawajatekeleza ahadi zao
ambazo ni jumla ya shilingi bilioni nne nukta tano wakamilishe ahadi
hizo ili ziweze kumalizia miundombinu ya Serikali iliyoathiriwa na
tetemeko hilo.
Ameongeza
kuwa wale wote wanaoendelea kuguswa kusaidia wapeleke michango yao moja
kwa moja kwa wananchi badala ya kuipeleka serikalini kwa kuwa hakuna
mchango mwingine utakaopokelewa katika Ofisi ya Waziri Mkuu.
Pia
Rais Dkt Magufuli ameagiza shule ya Sekondari ya Omumwani iliyokuwa
inamilikiwa na Jumuia ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi CCM imilikiwe na
Serikali kutaka wanafunzi wote wanaosoma katika shule hiyo kutolipa ada
kama zilivyo shule nyingine za serikali.
Dkt
Magufuli ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kagera kupunguza utitiri wa kodi
katika zao la kahawa ili bei ya zao hilo ipande na kuwanufaisha wakulima
Balozi
wa Uingereza hapa Nchini Bi Sarah Cooke ambaye nchi yake imechangia
kiasi cha shilingi bilioni sita kwa ajili ya ujenzi wa shule ya
Sekondari ya Ihungo, amempongeza Rais Dkt Magufuli na serikali yake kwa
jitihada za kupambana na rushwa suala ambalo nchi yake ya Uingereza
inalipa kipaumbele sambamba na kutoa elimu bila malipo jambo
linalowawezesha watoto wengi wa kitanzania kupata elimu bure
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kagera.
02 Januari, 2017