Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa ahirisho la mwisho katika kesi ya kutumia
lugha ya matusi dhidi ya Rais John Magufuli inayomkabili mbunge wa
Kawe (Chadema), Halima Mdee.
Akizungumza
leo Ijumaa Juni 1, 2018 Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ametoa ahirisho
hilo la mwisho kwa upande wa mashtaka baada ya wakili wa Serikali
mwandamizi, Patrick Mwita kudai kesi ilipangwa kwa ajili ya kuanza
kusikilizwa, hawana shahidi ikiwa ni mara ya tatu.
Baada
ya kutolewa maelezo hayo, hakimu Simba alitoa ahirisho la mwisho na
kupanga kesi hiyo kusikilizwa tena Juni 29, 2018 kwa mashahidi wa upande
wa mashtaka kuanza kutoa ushahidi.
Katika
kesi hiyo Mdee anadaiwa kufanya kosa hilo Julai 3, 2017 Makao Makuu ya
Chadema yaliyopo mtaa wa Ufipa wilaya ya Kinondoni.
Anadaiwa kutamka “anaongea hovyo hovyo, anatakiwa afungwe breki” kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Halima
alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Julai 10, 2017. Katika
kesi hiyo mbunge huyo anatetewa na mawakili, Peter Kibatala, Jeremiah
Mtobesya na Hekima Mwasipu.
0 comments:
Chapisha Maoni