Madalali wa Mahakama Kuu jana waliondoa na kukamata mali za Hospitali ya African Medical Investment Ltd (AMI) maarufu kama Trauma Center ya Msasani Jijini Dar es Salaam, baada ya kushindwa kulipa kodi ya pango kwa zaidi ya miezi 26, inayofikia zaidi ya dola za kimarekani milioni 1.6.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Mwakilishi wa kampuli ya MEM Auctioneers and
General Brokers Limited iliyopewa kazi ya kukamata mali hizo, Elieza
Mbwambwa alisema walikuwa wanatekeleza amri ya Mahakama Kuu, Kitengo cha
Biashara kilichoamuru mali hizo zikamatwe ili kupigwa mnada kwa ajili
ya kulipa deni lao la pango na kisha kuondolewa kwenye jengo na
kumkabidhi mmiliki ambaye ni Navtej Singh Bains.
Alitaja
mali zilizokamatwa kuwa ni pamoja na magari matatu ya kubebea wagonjwa,
vitanda maalum vya kulaza na kuwahudumia wagonjwa, gari ndogo aina ya
Mark II, mashine mbalimbali kama kompyuta, printa, microwave, viti,
meza, makochi na hata vitambaa na mashuka ya hospitali.
“Japokuwa
mahakama ilitoa amri ya kukamatwa mali zote baada ya kikomo cha notisi
ya siku 14, ambayo imeisha jana, mdai amefanya ubinadamu wa kutuomba
kama madalali wa mahakama, kuondoa na kukamata vitu ambavyo havitumiki
na wagonjwa waliolazwa.
“Tumewapa
hospitali ya AMI notisi nyingine ya kuwahamisha wagonjwa kabla ya Mei
22 mwaka huu, kisha tutaondoa kila kitu chao na kumkabidhi mwenye jengo,
jengo lake.
"Tulichofanya ni kuorodhesha mali zote ambazo bado zinatumika na wagonjwa hawa. Wagonjwa wapya hawataruhusiwa kupokelewa tena.
"Tulichofanya ni kuorodhesha mali zote ambazo bado zinatumika na wagonjwa hawa. Wagonjwa wapya hawataruhusiwa kupokelewa tena.
“Endapo hawa waliolazwa hawatahamishwa na hospitali, sisi tutafanya utaratibu wa kuwahamishia katika hospitali zingine,” alisema Mbwambwa.
Alitaja
mashine ambazo zimeachwa kwa ajili ya kuwapa huduma wagonjwa kuwa ni
City-Scan, X-ray na mashine nyingine ambayo ni muhimu katika kuchunguza
maendeleo ya afya ya mgonjwa.
Akizungumza
kwa niaba ya uongozi wa hospitali hiyo, Lawrence Ochola alisema bado
madaktari wanaendelea kuwahudumia wagonjwa waliolazwa na kwamba hawezi
akasema zaidi ya hayo.
Hatua
hii ya kufukuzwa kwenye jengo imefikiwa baada ya mabishano ya muda
mrefu ya kisheria baina ya AMI na mfanyabiashara ambaye pia ni mmiliki
wa jengo hilo, Navtej Singh Bains.
Taarifa
zaidi inasema kwamba akaunti za Benki za Hospitali hiyo ya AMI katika
Benki ya EXIM zilizoambatanishwa na Mahakama zilikutwa zikiwa zimefungwa
na fedha zote zikiwa zimetolewa.
Amri ya kufurushwa kwa AMI ilitolewa Mei 7 mwaka huu na kusainiwa na Makamu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Hatua
hii sasa inafanya kufungwa kwa Hospitali ya AMI, licha ya rufaa zake za
kujaribu kuzuia kufukuzwa, huku ikiwaacha wateja wake katika hali ya
sintofahamu.
Baadhi
ya ndugu na jamaa wa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo walionekana
wakifanya taratibu za kuanza kuwahamisha wagonjwa wao, huku uongozi wa
hospitali ukionekana kukaa kimya.
Hatua
hii ya kufukuzwa kutoka kwenye jengo inatokana na hospitali hiyo
kushindwa kutimiza amri ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania iliyoamuru
kulipwa kwa dola za kimarekani milioni 1.6 mahakamani pamoja na kodi ya
kila mwezi ya kiasi cha dola za kimarekani 64,000 kufuatia mgogoro wa
kodi ya jengo.
Ofisa
Mtendaji Mkuu wa AMI Plc, Theunis Botha, ambaye pia ni Mkurugenzi na
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya AMI Tanzania, aliwasilisha ombi
katika Mahakama Kuu ya Tanzania kuwa imefilisika.
Katika
shauri hilo la ufilisi lililofunguliwa wiki iliyopita kwa Msajili wa
Mahakama Kuu, kampuni hiyo inadai kuwa imekuwa ikikumbana na hasara za
mabilioni ya shilingi jambo lililofanya kuwepo kwa madeni yaliyokithiri
ambayo kwa sasa yako nje ya uwezo wa kampuni kulipa.
“Mlalamikaji
(AMI) anadai alipata hasara halisi ya Dola za kimarekani 1.146 katika
mwaka uliomalizika Februari 28, 2013, huku kwa mwaka uliomalizika
Februari 28, 2014, mlalamikaji alipata hasara ya Dola za Kimarekani
775,000,” inasomeka sehemu ya hati ya malalamiko.
AMI
Tanzania inamilikiwa na Kampuni mama ya AMI Plc ya London ambayo
iliondolewa kwenye Soko la Hisa la London Februari 2014 baada ya jaribio
la kuuza mali zake zilizopo Maputo, Msumbiji bila kibali kutoka kwa
wanahisa.
Inaelezwa
kuwa kampuni hiyo ilitakiwa pia kufanya malipo kwa taasisi mbalimbali,
zikiwemo Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA) na watu na kampuni binafsi.
Kwa
mujibu wa shauri hilo, ukichukulia thamani ya mali za kampuni na kiasi
cha fedha zinazodaiwa na wadai, kulikuwa hakuna njia ya kuweza kupata
fedha za kutosha kuwalipa sambamba na kutekeleza majukumu yake.
Pia
kuna kumbukumbu zinazoonesha kuwa Lancet Laboratory (T) Ltd
iliwasilisha ombi la dharura dhidi ya kufungiwa kwa Hospitali ya AMI
ikiwa inaidai hospitali hiyo zaidi ya Sh milioni 150.
Taarifa
za ndani zinaeleza kuwa wadai mbalimbali wako njia panda kutokana na
deni kubwa la Dola za Kimarekani milioni nne wanaloidai hospitali hiyo.
Wadai wakubwa ni pamoja na mmiliki wa jengo Bains, madaktari,
wafanyakazi, TRA, wasambazaji wa dawa na wasambazaji wengine.
0 comments:
Chapisha Maoni