WIZARA
ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi imetoa ufafanuzi
kwamba haijapiga marufuku watu wenye Stashahada wenye sifa kujiunga na
vyuo vikuu badala yake walichokataza ni wanafunzi waliofeli kidato cha
nne na cha sita kujiunga na vyuo vikuu bila kuwa na vyeti vyenye sifa.
Aidha,
imesema kwa waliomaliza kupitia mfumo huo na wapo kazini ni wajibu wa
waajiri wao kuhakikisha wana sifa za kazi wanazofanya na kutumia fursa
hiyo kufanya mitihani ili kuwa na sifa zinazohitajika.
Naibu
Waziri wa wizara hiyo, Stella Manyanya alitoa ufafanuzi huo jana Dar es
Salaam kutokana na taarifa za upotoshaji zilizoenea mitandaoni kwamba
serikali imepiga marufuku watu wenye Stashahada kujiunga na vyuo vikuu
badala yake watakaoingia ni wenye sifa za kidato cha sita.
Manyanya
alisema kwa waliopo vyuoni kwa sasa wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa na
sifa za shahada kwa kusafisha vyeti vyao na wapewe fursa ya kufanya
mitihani hiyo waliyofeli na kama wamefaulu kozi hiyo, pia wataweza
kufaulu mitihani hiyo itakayowapa sifa ya kusoma vyuo vikuu.
“Ni
vitu tunavyovifanya wenyewe ila vina madhara makubwa, unakuta mtu
anakaa nafasi kwa sababu ana vyeti, lakini uwezo hana… uhakiki
utafanyika kwa vyeti na wanaofanya hivyo ni Utumishi,” alisema Naibu
Waziri.
Alisema
kwa watakaobainika pia kuingia vyuoni kwa sifa ambazo zilikuwa
hazitakiwi kwa wakati huo ni batili zitafutwa na kwa watakaoingia kwa
sasa vyuoni kwa kutumia njia zisizo rasmi na kubainika hata ikifika
mwaka 2020 watafutwa kwa kuwa taarifa tayari wanayo.
“Kilichoongelewa
siku ile ni kuruhusu kidato cha nne na kidato cha sita waliofeli
kuingia kwenye ‘foundation course’ na diploma haikutajwa pale kwa kuwa
haikuulizwa na hakuna kauli iliyotajwa pale kukataza watu wa diploma
kwenda chuo kikuu,” alieleza Manyanya akirejea kauli ya Waziri wake,
Profesa Joyce Ndalichako hivi karibuni katika mahafali ya Chuo Kikuu
Huria Tanzania (OUT) yaliyofanyika mkoani Pwani.
Profesa Ndalichako alikaririwa akisema vigezo vya udahili vinatakiwa kuzingatiwa.
“Nami
ningependa nizungumzie kwamba foundation course hazimuongezei mtu sifa.
Kama sifa ya kujiunga na chuo kikuu ni kufaulu kidato cha sita, kama
amefeli Baraza la Mitihani linaruhusu kurudia mtihani, kwa nini anakwepa
kule? Kwa nini? Kwa nini tunataka tuendeleze uchochoro,” alieleza
Waziri Ndalichako.
Naibu
Waziri alisema kuna njia mbili za kwenda chuo kikuu ikiwemo njia ya
moja kwa moja na njia ya mbadala ya kuwa na vyeti vinavyotambulika na
kinasimamiwa na mamlaka husika ambayo ni Baraza la Taifa la Elimu ya
Ufundi (NACTE) na wawe na ufaulu mzuri.
“Tanzania
imejiwekea mifumo yake ya elimu ambayo inaendana na ngazi za kimataifa
katika utoaji wa elimu na hapo awali tulikusudia kuhakikisha elimu
inatolewa kwa watu wengi zaidi na hizo fursa zinawafikia wadau wote
katika ngazi mbalimbali kwa kupanua elimu ya msingi hadi vyuo vikuu,”
alieleza Naibu Waziri.
Alisema
walitambua kuna wadau mbalimbali walitamani kusoma vyuo vikuu, lakini
hawapati hiyo fursa na ndiyo wakaanzisha mfumo huo wa Chuo Kikuu Huria
na mtu anaweza kusoma alipo na mfumo umekuwa ukiboreshwa siku hadi siku.
Alisema
iliwekwa mifumo ya vyeti na ngazi zake kulingana na vigezo na hivyo
siyo kila cheti kinachotolewa kinaruhusu mtu kwenda ngazi nyingine na
kila mamlaka imepewa jukumu ili kulinda ubora wa elimu unaotolewa
nchini.
Naibu
Waziri alisema kutokana na uanzishwaji wa vyuo mbalimbali kumejitokeza
changamoto na watu kutoka katika mfumo rasmi uliopangwa na kujiwekea
mifumo binafsi ambayo imeingiza hata wanafunzi wa kidato cha nne ambao
hawana sifa kuingia vyuo vikuu.
“Jambo
hilo limesababisha kuwepo kwa msuguano, haiwezekani mtu afeli kidato
cha nne bila kuwa na cheti kingine chochote anaingizwa katika kozi hiyo
halafu anaingizwa chuo kikuu, sisi hatujarasimisha mfumo huo wa
‘foundation course’ na hatuna vipimo vyake,” alieleza.
Alisema
kwa kawaida mwanafunzi mwenye diploma inayotambulika wamewekewa usawa
wa alama fulani na kidato cha sita hivyo wanakuwa na sifa ya kuingia
vyuo, lakini siyo waliofeli hivyo wanatakiwa kufanya utafiti zaidi
katika kozi hiyo.
“Haiwezekani
kila mtu akajianzishia mfumo wake tu, tulifikia eneo ambalo si zuri
kama nchi na sasa tutaimarisha ubora…ukifeli kidato cha nne unatakiwa
kwenda kusoma na kupata cheti kwenye mtaala unaotambulika na ukaenda
diploma na unapofaulu unaweza kwenda chuo kikuu,” aliongeza.
Naye
Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Simon Msanjila alisema suala
la ‘Foundation course’ limelenga kumuandaa mtu mwenye sifa ambaye
amekuwa nje ya mfumo kwa muda mrefu ili kuingia chuo kikuu, lakini
walichokuwa wakikifanya wengi ni kuwachukua waliofeli kidato cha nne na
sita na kuwaingiza katika kozi hiyo na hatimaye kuwaingiza chuo kikuu.