KESI
inayomkabili mkazi wa mtaa wa Ng’ong’ona Manispaa ya Dodoma Tito
Machibya, maarufu kama ‘Nabii Tito’ (45), ya kujaribu kujiua kwa kutumia
wembe, imeahirishwa tena kuanza kusikilizwa hadi Machi 19, mwaka huu
kutokana na ripoti ya vipimo vya akili kutokamilika.
Akiahirisha
kesi hiyo jana, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, Mwajuma
Lukindo, alisema kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe hiyo kutokana na
ripoti ya vipimo hivyo kutokamilika.
Kwa
mujibu wa chanzo kutoka katika Taasisi ya Afya ya Akili Mirembe Isanga
kwa kawaida ripoti ya vipimo huchukua siku 42, hivyo kutokana na hali
hiyo vipimo vya nabii huyo havijakamilika.
Februari
5, mwaka huu mahakama hiyo iliagiza kutekelezwa kwa amri iliyotolewa na
Mahakama hiyo ambayo iliamuru jana, kupelekwa kwa vielelezo
vinavyoonyesha Nabii Tito ana matatizo ya akili na kufanyiwa vipimo
katika Taasisi ya Afya ya Akili Mirembe Isanga.
Akitoa
maelezo ya kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
James Karayemaha, Wakili wa Serikali, Beatrice Nsana, aliiomba mahakama
kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuwasilishwa kwa taarifa
kutoka Isanga.
Hata
hivyo, Hakimu Karayemaha alisema mshtakiwa huyo amewasilisha vielelezo
vyake kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na mahakama inahitaji
taarifa kutoka Taasisi ya Mirembe Isanga kama ilivyoagiza.
“Mahakama
ilitoa amri apelekwe Taasisi ya Mirembe Isanga kwa mujibu wa kifungu
namba 219 (2) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai,” alisema Hakimu
Karayemaha.
Kifungu
hicho kinasema kama mshtakiwa atabainika kuwa kweli ana matatizo ya
afya ya akili, mahakama itaamua kuwa alivyofanya tukio hilo hakuwa na
akili timamu, hivyo hana hatia.
Kutokana
na hali hiyo, Hakimu Karayemaha alimuamuru Mkuu wa Magereza ya Isanga
kutekeleza amri ya mahakama iliyotolewa ya kumpeleka kufanyiwa vipimo
mshtakiwa huyo.
“Namuamuru
Mkuu wa Magereza Isanga atekeleze amri ya mahakama, ili taarifa za
mshtakiwa ziletwe Machi 5, mwaka huu, tutataja kesi na kupokea taarifa
ya vielelezo vya vipimo vyake kutoka Isanga na mshtakiwa ataendelea
kukaa rumande,” alisema hakimu huyo.
Nabii
Tito anashtakiwa kwa kosa la kutaka kujiua kwa kujikata na wembe na
kujijeruhi kwenye maeneo ya tumbo Januari 25, mwaka huu katika mtaa huo
wa Ng’ong’ona.
0 comments:
Chapisha Maoni