Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harisson Mwakyembe (Mb) ametangaza
rasmi kanuni mbili za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA)
ya Sura namba 306 ya mwaka 2010, katika gazeti la Serikali namba 133 (GN.No.133)
na 134 (GN.No.134) zilizochapishwa tarehe 16/03/2018.
Kanuni
za Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Habari za
Mtandaoni) ya mwaka 2018 ijulikanayo kama The
Electronic and Postal Communications
(Online Content) Regulations, 2018 zimetangazwa kupitia Tangazo la Serikali Namba 133 (GN.No.133).
Kanuni
nyingine ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya
Utangazaji katika Redio na Runinga) ya mwaka 2018 ijulikanayo kama The Electronic and Postal Communications (Radio and Television Broadcasting Content)
Regulations, 2018 ambazo zimetangazwa kupitia tangazo la Serikali namba 134 (GN.No.134).
Kanuni
hizi kwa pamoja zimetengenezwa chini ya Kifungu cha 103 cha
sheria ya EPOCA na zimetiwa saini na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ambaye ndiye mwenye dhamana na Maudhui ya
Habari na Utangazaji.
Kwa
ujumla kanuni hizi zinalenga kuongeza ufafanuzi wa mambo muhimu katika Sekta ya
Habari, kwa ajili ya kuongoza vyombo vyenye mamlaka ya kusimamia pamoja na
kurahisisha utekelezaji kwa watumiaji mbalimbali wa huduma ya Sekta hiyo.
Mchakato
wa kuandaa Kanuni hizi ulihusisha wadau mbalimbali wa Habari wakiwamo wamiliki
wa vyombo, watoa huduma za mawasiliano ya mtandaoni, watumiaji wa mtandao, waandishi
wa habari, pamoja na wanaharakati na watetezi wa haki za walaji wa huduma za
sekta hii pamoja na Wizara ikisaidiana na wataalamu wa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA).
Kanuni
za Maudhui ya Utangazaji wa kwenye redio na kwenye runinga pamoja na mambo
mengine zimefafanua juu ya dhana kuu mbili ambazo zimekuwa katika mijadala ya
watoa huduma na watumiaji wengi, mambo hayo ni kuhusu Chaneli ambazo ni lazima
kubebwa na anayemiliki miundombinu ya kurushia matangazo hata kama hazijalipiwa
kwenye king’amuzi cha mlaji wa mwisho ( free
to air channels).
Aidha, Kanuni zinawaelekeza wamiliki wa mitambo ya kurushia
matangazo kulazimika kurusha hewani Chaneli ya umma (must carry public broadcaster channel) pasipo chombo cha umma
kinachorusha chaneli hiyo au mwananchi anayemiliki king’amuzi kulipia chochote.
Vilevile
Kanuni hizo zimeeleza juu ya taratibu za utoaji wa leseni za maudhui kwa vyombo
vya habari, aina za leseni, masharti ya utoaji wa maudhui kwa vyombo vya
habari, masharti ya urushaji vipindi, masharti ya jumla kwa leseni za huduma za
maudhui.
Pia,
Kanuni hizo zimeeleza juu ya viwango vya kitaalamu na kiufundi katika huduma za
utangazaji, utoaji wa vibali vya ujenzi wa miundombinu ya utangazaji, aina za
huduma na leseni za maudhui, wajibu wa vituo vya umma, wajibu wa vituo vya
kibiashara, wajibu wa vituo vya kijamii, wajibu kwa utangazaji wa maudhui
yanayolipiwa pamoja na masharti kwa kampuni za miundombinu ya maudhui.
Kanuni hizi
pia zimezingatia kuwalinda watoto dhidi ya maudhui yasiyofaa, muda kwa vipindi
ambavyo watoto hawaruhusiwi kuona kama vile utangazaji wa maudhui yenye vitendo
vya ngono au maudhui yanayoonesha vurugu.
Mambo mengine ni masharti ya kutangaza
mwenendo wa Mahakama au Bunge, masuala ya uchaguzi, masharti ya kutangaza
maudhui kwa watu wenye mahitaji maalum, masharti kwa utangazaji wa vipindi vya
mahojiano, lugha ya kutumia katika utangazaji.
Zimeelezea
pia juu ya utangazaji wa maudhui ya ndani ya nchi na vipindi vyenye maslahi ya
Kitaifa, vipindi vya taarifa za kiuchunguzi au masuala ya watu binafsi
(Faragha), Utangazaji wa vipindi vya moja kwa moja.
Vilevile
kumewekwa utaratibu wa kupokea na kusikiliza malalamiko ya walioathiriwa na
habari za mtandaoni pamoja na adhabu kwa wanaofanya makosa kupitia mawasiliano
ya mtandaoni.
Kanuni
hizi zitafanya kazi chini ya Kamati ya Maudhui ambayo nayo imeundwa chini ya
Sheria hiyo. Wadau mbalimbali wa vyombo vya habari na utangazaji pamoja na
watumiaji wa mawasiliano ya habari kwa njia ya mtandao wanashauriwa kuzipitia
kanuni hizo na kuzisoma kwa kina ili kuelewa mambo yaliyofafanuliwa.
Kanuni hizi zinapatikana katika Tovuti ya Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo (www.habari.go.tz)
kisha ingia sehemu ya machapisho bofya kipengele cha Sera, sheria na kanuni, pia waweza
kutembelea tovuti ya TCRA (www.tcra.go.tz)
0 comments:
Chapisha Maoni