Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Amon Mpanju amesema
kuwa mapenzi ya jinsia moja hayakubaliki na Serikali ilishaweka msimamo
wake katika hilo.
Akizungumza
mapema leo katika mkutano wa wadau wa haki za binadamu uliofanyika
katika hoteli ya Blue Pearl wa kujadili mapendekezo ya tathmini ya
utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu (Universal Periodic Review), Mhe. Mpanju ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika
mkutano huo alisema mapendekezo yaliyowasilishwa Mwezi Mei mwaka huu
katika mkutano wa Baraza la haki za binadamu uliofanyika Geneva,
serikali ilikubali mapendekezo Mia thelathini (130) na mengine 72
iliyakataa.
“Sehemu
ya mapendekezo hayo serikali iliyakataa kwa sababu kuna mengine yapo
kinyume na katiba, sheria, mila na desturi zetu, kwani katika
mapendekezo hayo yapo yanayotaka mapenzi ya jinsia moja jambo ambalo
haliwezi kukubalika”, Mhe. Mpanju alisema
“Hivyo
wakati mkijadili namna ya kupanga mikakati ya utekelezaji ili serikali
ione umuhimu wa kukubali sehemu ya mapendekezo hayo naomba msijielekeze
kwenye yale yaliyo kinyume na imani”, Mhe. Mpanju alisisitiza
Aidha,
Mhe. Naibu Katibu huyo alisema serikali imefungua milango kwa
kushirikiano na tume, wadau wa haki za binadamu wapeleke serikalini
sababu zenye mantiki ili kuona ni mambo gani ambayo serikali inaweza
kuyashugulikia na kuyatekeleza.
Akizungumza
katika Mkutano huo, Bwana Onesmo Olengurumwa kutoka taasisi ya watetezi
wa haki za binadamu (THRDC) alisema kuwa wadau wamekutana katika
mkutano huo kujadili ni kwa namna gani wataishawishi serikali ili
iweze kuyakubali mapendekezo yaliyobakia na kuyaweka katika utekelezaji.
Akifungua
mkutano huo kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi, Makamu Mwenyekiti wa
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mhe. Iddi Mapuri alisema kuwa
mkutano huo umelenga katika kuweka mikakati ya ufuatiliaji wa
utekelezaji wa mapendekezo hayo na alipongeza mchango mkubwa unaotolewa
na wadau wa haki za binadamu katika kuhakikisha masuala ya haki za
binadamu yanapata msukumo mkubwa hapa nchini.
Bwana Onesmo Olengurumwa
(aliyevaa koti la Drafti) kutoka taasisi ya watetezi wa haki za binadamu
(THRDC) akijadiliana jambo na Mkurugenzi wa Idara ya huduma za sheria
wa Tume ya Haki za Binadamu, Bwana Nabor Assey( aliyevaa shati la bluu).
Nyuma yao ni Bwana Laurent Burilo burilo, Mratibu wa Mpango kazi wa
Haki za Binadamu(katikati) na Bwana Deugratius Bwire kutoka (THRDC
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Katiba na Sheria, Mhe. Amon Mpanju (aliyevaa miwani) akiteta jambo na
Bwana Onesmo Olengurumwa (aliyevaa koti la Drafti) kutoka taasisi ya
watetezi wa haki za binadamu (THRDC) katika mkutano huo wa kujadili
mapendekezo ya tathmini ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu na
kuweka mikakati ya kuishawishi serikali kukubali mapendekezo mengine
ambayo iliyakataa.
Sehemu ya wadau wa haki za
binadamu wakifuatilia majadiliano katika mkutano huo wa kujadili
mapendekezo ya tathmini ya utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu.