Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Selemani
Jafo amewasimamisha kazi wakurugenzi wawili kati ya watatu wa
Halmashauri za Pangani na Kigoma baada ya kupata hati chafu katika
matokeo ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa
mwaka 2016/17.
Ripoti
hiyo iliyowasilishwa leo Machi 27, 2018 inaonyesha halmashauri 166
kupata hati safi, 16 hati zenye shaka na halmashauri tatu kupata hati
chafu.
Umauzi huo unafanyika ikiwa ni dakika chache baada ya Rais John Magufuli kutoa agizo hilo.
Halmashauri zilizopata hati chafu ni Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na Halmashauri ya Kigoma na Pangani.
Waziri
Jafo amesema baada ya kuwasimamisha, amemwagiza katibu mkuu wa wizara
hiyo kuunda timu ya watalaamu kuchunguza hati hizo na kutoa matokeo
ndani ya wiki tatu.
Amesema
wakurugenzi waliohusika katika hati chafu ni Daud Mlahagwa (Pangani),
aliyekuwa Mkurugenzi wa Kigoma Ujiji, Judethadeus Mboya ambaye amestaafu
kwa sasa.
“Amestaafu
lakini ameacha mambo yakiwa hayako sawa, wakati akiwa ‘account officer’
mambo yalikwenda kombo na halmashauri hiyo ilipata hati chafu kwa miaka
mitatu mfululizo,” amesema.
Mwingine ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Kigoma, Hanji Godigodi na Damian Chambasi wa Pangani.
“Wakurugenzi
hawa waliosababisha hati chafu nawasimamisha kazi kuanzia leo Machi 27,
2018 hadi hapo uchunguzi wa utendaji wao utakapokamilika, hawa wawili
nawasimamisha kazi, kutokana na hili namwagiza katibu Mkuu wa Tamisemi
kuunda timu ya watalaamu kwenda kuchunguza utendaji kazi wa wakurugenzi
hao na kunipatia taarifa ndani ya wiki tatu,”amesema.
Amesema
taarifa itakayopatikana itabainisha kiwango cha uchafu huo na Serikali
itachukua hatua nyingine za kisheria kadri uchunguzi utakavyoelekeza.
Pia,
amewataka wakurugenzi katika halmashauri zilizofanya vizuri katika
ukaguzi huo, waendelee kutekeleza na majukumu yao na kutoa majibu ya
hoja zote zilizobainishwa na ripoti ya CAG.
Amesema
Serikali imeanza kufanya vizuri katika ukaguzi huo baada ya kufikia
asilimia 90 na matumaini yaliyopo ni kuondokana na taarifa ya hati chafu
ili kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika kwa maendeleo ya wananchi.
0 comments:
Chapisha Maoni