WAZIRI MKUU AMUAGIZA MKURUGENZI WA MISUNGWI AITISHE KIKAO KESHO SAA 4
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Misungwi, Bw. Eliud Mwaiteleke aitishe kikao na wananchi wa Kigongo na
kutafuta ufumbuzi wa tatizo la eneo la kujenga soko.
Ametoa
agizo hilo leo jioni (Jumatano, Juni 21, 2017) wakati akizungumza na
mamia ya wakazi na wajasiriamali wanaotumia kivuko cha feri cha Kigongo
waliokuwa wakimsubiri avuke kwenda Busisi, wilayani Sengerema.
"Mkurugenzi
haya mambo ya mipango, mipango na kupanga hayaleti tija kwa wananchi.
Hivi hamjui kuwa wananchi wanahitaji kuwa na soko katika eneo hili ili
waweze kuuza mazao yao au samaki?"
"Ninakuagiza
Mkurugenzi, kesho Alhamisi, saa 4 njoo na Afisa Biashara wako,
Mwenyekiti wa kijiji na watu wako pamoja na Diwani wa hapa, itisheni
kikao na muonyeshwe eneo la soko ili mliingize kwenye mipango yenu,"
alisema.
Waziri Mkuu alisema Serikali ya awamu ya tano haitaki kusikia lugha za michakato wakati wananchi wanaendelea kuteseka.
Awali,
Waziri Mkuu alimwita Mkurugenzi huyo ili aeleze amejipanga vipi kwenye
Halmashauri yake kutatua tatizo la soko kwa wananchi wa Kigongo.
Akitoa
majibu mbele ya Waziri Mkuu, Bw. Mwaiteleke alisema hawajawahi kupata
mpango kutoka kwenye kata hiyo na kwa hiyo akawasihi wananchi waibue
mpango huo na kuuwasilisha kwenye Halmashauri ili wao waweze kutenga
fedha za kujenga soko.
Mapema,
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigongo, Bw. Sebastian Kisumo alimweleza
Waziri Mkuu kwamba eneo hilo linakabiliwa na tatizo la soko pamoja na
uhaba wa maji.
Kuhusu
maji, Waziri Mkuu alisema Serikali imetenga sh. bilioni 2.5 kwa ajili
ya mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria eneo la Itelele ambao
utasambaza maji kwenda Misungi, Usagara hadi Kigongo Feri.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, JUNI 21, 2017.
0 comments:
Chapisha Maoni