test

Jumamosi, 6 Agosti 2016

TRA kuanza kukusanya kodi kwenye nyumba za kupanga



MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kuanza kutembelea nyumba hadi nyumba kuhakiki gharama za upangishaji ili kukokotoa na kukusanya kodi sahihi ambayo ilikuwa haifiki serikalini. 

Hivyo, wamewataka wananchi kutunza kumbukumbu za mikataba ya pango ili itakapohitajika na maofisa wa mamlaka hiyo wawapatie.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati akielezea kuhusu makusanyo ya kodi kwa mwezi Julai, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema hatua hiyo ni moja ya mikakati ya kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Alisema kwa Julai, TRA imekusanya Sh trilioni 1.055 sawa na asilimia 95.6 ya lengo la kukusanya Sh trilioni 1.103 iliyopangiwa na serikali kwa mwezi huo.

Alisema ikilinganishwa na kipindi kama hiki kwa mwaka jana, TRA ilikusanya Sh bilioni 914 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.43 ya makusanyo ya mwezi huu huku kwa mwaka wa fedha 2016/2017, TRA imepewa lengo la kukusanya Sh trilioni 15.1 ikilinganishwa na lengo la mwaka jana la Sh trilioni 13.32.

“Natoa wito kwa wapangaji na wapangishaji kujiepusha na aina yoyote ya udanganyifu katika suala zima la kodi halisi ya pango kwa kuwa inaweza kuwasababishia kushtakiwa endapo udanganyifu huo utabainika,” alieleza Kayombo.

Kwa sasa, wapangaji wengi hawalipi kodi serikalini baada ya kupanga nyumba, na badala yake wamekuwa wakilipa fedha za pango kwa wamiliki wa nyumba ambao wengi wao pia hawalipi kodi serikalini zaidi ya kulipia kodi za majengo.

Wapangaji wamekuwa wakilipishwa kodi ya pango kuanzia ya miezi sita hadi mwaka moja na kodi hizo zimekuwa zikitofautiana kutokana na hadhi ya nyumba, eneo ilipo, ukubwa wake na huduma ilizonazo kama maji na umeme.

Aidha, Kayombo alisema pia mamlaka hiyo itatembelea waajiri katika maeneo mbalimbali kuhakiki na kukagua usahihi wa orodha na malipo ya ajira ili kujiridhisha kama kodi za ajira zinakokotolewa na kulipwa serikalini inavyostahili.

Alisema mbali na mkakati huo, TRA imeweka mikakati ya kuhakikisha walipakodi wapya wanasajiliwa zaidi pamoja na kuhuisha taarifa za walipakodi kwa kuhakikisha Namba za Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) zisizotumika zinafutwa katika mfumo wa mamlaka.

“Maandalizi ya kuhuisha taarifa za walipakodi yako katika hatua za mwisho yakihusisha upigaji picha, kuchukua alama za vidole pamoja na vielelezo muhimu vya mlipakodi ili kuhakikisha kila biashara inakuwa na TIN moja tu yenye taarifa sahihi na za uhakika,” alifafanua.

Alisema TRA imeboresha mifumo yake ili kupunguza au kuondoa changamoto za kutopatikana kwa mtandao ambayo mara nyingi huathiri makusanyo ikiwa ni pamoja na kuunganisha mifumo ya TRA na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ili kuhakikisha mapato ya serikali yanakusanywa kwa usahihi na wakati.

Pia wanaendelea kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato kwa kuhakikisha wafanyabiashara wote wanaostahili kutumia mashine za kielektroniki za kodi (EFDs) wanazitumia ipasavyo pamoja na kuwakagua wanunuzi wanapotoka madukani kwa lengo la kuhakikisha wana risiti halali na sahihi kwa manunuzi yao. 
Kayombo alisema TRA inawaasa wananchi kuhakikisha wanakagua risiti zao za manunuzi na kuangalia usahihi wa fedha walizolipa na uhalali wa risiti yenyewe.

“Tunatoa wito kwa umma kutoa risiti wakati wa kuuza na kudai risiti wakati wa manunuzi ya bidhaa au huduma kwani sheria ya fedha ya mwaka huu imerekebisha sheria ya usimamizi wa kodi na wasiodai risiti kwa manunuzi yoyote watapata adhabu ya Sh elfu thelathini hadi Sh milioni moja na nusu,” alisema.

Alisema kwa sheria hiyo kutotoa risiti na kutodai ni makosa kwa mujibu wa sheria na hatua zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kutotoa risiti au kutodai risiti wakati wa mauzo na manunuzi.

Alisema wanaendelea kukusanya mapato na kutoa elimu kwa wananchi hasa mabadiliko ya sheria mbalimbali za kodi kama Sheria ya Fedha ya mwaka 2016 iliyopitishwa hivi karibuni ili kujenga uelewa na kukuza ridhaa ya kulipa kodi kwa hiari.

Tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano, Rais John Magufuli amekuwa akisisitiza Watanzania kujenga tabia ya kutoa na kudai risiti kwa kusisitiza ‘ukinunua dai risiti na ukiuza toa risiti.’

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx