Mkurugenzi
wa Idara ya Huduma za Sheria wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Marlin Komba
amesema hamtambui mtu anayejiita nabii Tito na kwamba hajasajili kanisa
lake katika ofisi ya msajili wa taasisi za dini.
Komba amesema Serikali imeona vitendo anavyovifanya ‘nabii’ huyo kupitia mitandao ya kijamii na imeanza kuchukua hatua.
“Ninachoweza
kusema ni kwamba hakuna mtu anayezuiwa kuongea hapa nchini, mwache
aongee anavyoweza ila Serikali imeshaona anachokifanya na yanayoendelea
mitandaoni hatua zinachukuliwa dhidi yake,” amesema Komba.
Kwa
upande wao viongozi wa dini wameonyeshwa kukerwa na kulaani vitendo
anavyovifanya mtu huyo anayejiita nabii na kusisitiza kuwa hakuna dini
inayoruhusu hayo.
Msaidizi
wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Dayosisi ya
Mashariki na Pwani, Mchungaji Chediel Lwiza amesema kwa vitendo
anavyofanya mtu huyo hapaswi kujiita mtumishi wa Mungu.
“Huyo
hawezi kuwa mtumishi wa Mungu na wala hafanyi huduma ya kanisa ni vyema
watu kama hawa wafuatiliwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Natumaini Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo ndani yake ina ofisi ya
msajili wa taasisi za dini itafanya kazi yake.”
Lwiza ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Watanzania kwenda kwenye makanisa ya kweli yanayozingatia neno la Mungu.
Amesema,
“Hakuna sababu ya kutangatanga, Watanzania mkasali kwenye makanisa
yanayotambulika na yanayosimamia na kufundisha neno la Mungu. Kuhangaika
ndiko kunakowafanya wengine waangukie kwa watu kama hao. Wapo
wanaojaribu kupotosha neno la Mungu lakini ukweli ni kwamba neno la
Mungu halipotoshwi.”
0 comments:
Chapisha Maoni