Rais
Atengue Kauli Yake Kuhusu Watoto wa Kike Wanaopata Mimba Mashuleni
Maana ni Kinyume na Katiba, Sheria, Busara na hata Ilani ya Chama Chake.
Ngome
ya Wanawake ACT Wazalendo imeshtushwa na kusikitishwa sana na tamko la
kupiga marufuku wanafunzi waliopata ujauzito wakiwa shuleni kupata fursa
ya kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua lililotolewa na Rais
Magufuli Juni 22, 2017 katika hotuba yake kwa wananchi wilayani Bagamoyo
mkoani Pwani.
Ngome
ya Wanawake ya ACT Wazalendo inaiona marufuku hiyo kama hatua kali
inayomkandamiza na kumbagua mtoto wa kike kwa kumnyima haki yake ya
msingi ya kupata elimu, na kwahivyo inapinga amri hiyo ya marufuku.
Marufuku hii ni kinyume cha matakwa ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania ibara ya 11(2) inayosema:
"Kila
mtu anayo haki ya kujielimisha, na kila raia atakuwa huru kutafuta
elimu katika fani anayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na
stahili na uwezo wake".
ACT
Wazalendo inaamini kuwa licha ya kuzuia haki ya kikatiba ya
kujielimisha kwa mtoto wa kike lakini pia Rais ametumia mamlaka yake
kumbagua mtoto wa kike katika haki zake za msingi kinyume na Ibara ya
13(4) ya katiba inayosema kuwa "Ni marufuku kwa mtu yeyote kubaguliwa na
mtu au mamlaka yoyote inayotekeleza madaraka yake chini ya sheria
yoyote au katika utekelezaji wa kazi au shughuli yoyote ya Mamlaka ya
Nchi".
Marufuku
hii ni ubaguzi wa wa wazi dhidi ya watoto, na ni kinyume na Sheria ya
Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 (The Law of Child ACT, 2009) ibara 5 (1)
inayosisitiza kuwa "Mtoto ana haki ya kuishi huru bila kubaguliwa".
ACT
Wazalendo inamtaka Rais atambue kuwa Tanzania imeridhia na kusaini
maazimio mbalimbali ya kimataifa kuhusu haki za mtoto wa kike kama vile
Azimio la Dunia la Haki za Binadamu la mwaka 1948 (Universal Declaration
on Human Rights (1948) ibara ya 26(1), Tamko la Kimataifa la kupinga
aina zote za ukandamizaji dhidi ya Wanawake (Convention of the
Elimination of all forms of Discrimination Against Women - CEDAW) la
mwaka 1979 ambayo yote yameweka msisitizo wa kulinda haki za mtoto wa
kike.
Rais
alifanya kampeni mwaka 2015 Kwa kutumia ilani ya uchaguzi ya chama
chake cha CCM. Ilani hiyo iliahidi kuwa CCM ikifanikiwa kuunda Serikali
itaruhusu mtoto wa kike anayepata mimba kurudi shuleni baada ya
kujifungua. Kauli ya Mwenyekiti wa CCM na Rais inaonyesha kuwa CCM
iliwalaghai wananchi ili kupata kura.
ACT
Wazalendo inatambua uwepo wa changamoto mbalimbali za kiuchumi, kijamii
na kimazingira anazokabiliana nazo mtoto wa kike na zinachangia kwa
kiasi kikubwa kumuingiza bila kutarajia katika matatizo ya kupata
ujauzito akiwa shuleni.
Watoto
wengi wa kike hasa waishio maeneo ya vijijini na watokanao na familia
masikini ndio wamekuwa wahanga wakubwa wa matatizo ya kupata ujauzito
wakiwa shuleni kutokana na miundombinu isiyo rafiki ya elimu kama vile
ukosefu wa mabweni, kusafiri mwendo mrefu kwenda na kurudi shuleni,
kusaidia shughuli za nyumbani na shughuli za kuziingizia kipato familia
zao ambapo kote huko hukabiliana na changamoto kadha wa kadha zinazoweza
kuwasababishia ujauzito.
Sisi
tunaamini ni wajibu wa Serikali iliyopo madarakani, jamii pamoja na
familia kuhakikisha kuwa wanatengeneza mazingira rafiki na salama kwa
mtoto wa kike ili nae aweze kupata haki yake ya msingi ya elimu kama
ilivyo kwa watoto wengine na sio kumbagua, kumkandamiza na kumnyima haki
yake ya elimu. Zanzibar ni mfano hai kwenye hili kwa kuwalinda
wasichana wasipate ujauzito na kuwapa fursa ya kurudi shule hata pale
kwa bahati mbaya wanapopata ujauzito. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania iige jambo hili jema.
ACT
Wazalendo tunamtaka Rais Magufuli kutathmini upya msimamo wake na
kuzingatia mazingira, hali halisi, sera, sheria na maazimio mbalimbali
ambayo nchi imeyaridhia na kusaini kuhusu kulinda na kuhifadhi haki za
mtoto wa kike. Pia anapaswa kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto
zinazowakabili watoto wa kike badala ya kuwaongezea matatizo zaidi.
Hivyo ni muhimu atengue kauli yake hii.
Dhana
ya elimu kwa ujumla sio zawadi kwa watiifu na wale wanaoonekana na
nidhamu (hapa tukirejea sera ya elimu ya 2014) ambayo imeelezea vema juu
ya dhima na dira ya elimu). Kupata elimu ni haki ya kila mtoto.
Esther Kyamba,
Katibu, Ngome ya Wanawake,
ACT Wazalendo
Juni 24, 2017
Tanzania
0 comments:
Chapisha Maoni