Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa ametaka viongozi wa chama
hicho kuitisha kikao cha Kamati Kuu ili kujadili namna ya kudhibiti
vitendo vya kuwakamata viongozi wa chama hicho vinavyofanywa na wakuu wa
mikoa na wilaya.
Lowassa
ambaye alikuwa waziri mkuu kati ya mwaka 2005 na 2008, alisema hayo
juzi wakati wa futari aliyoindaa kwa madiwani na viongozi wa Chadema na
wakazi wa Dar es Salaam iliyofanyika Mikocheni.
Mwanasiasa
huyo alisema hayo wakati viongozi wa Chadema, akiwamo Waziri Mkuu wa
Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye walizuiwa kutembelea miradi
ya maendeleo kwa madai kuwa kabla ya ziara hiyo, Meya wa Ubungo,
Boniface Jacob alifanya kikao cha chama katika jengo la Serikali.
Meya huyo alikamatwa kwa amri ya mkuu wa Wilaya ya Ubungo na kukaa mahabusu kwa saa 48.
Mbali
na Jacob, Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Viola Likindikoki, diwani wa
viti maalumu Kata ya Ngarenaro, Happiness Charles na diwani wa viti
maalumu Kata ya Olorieni, Sabrina Francis walikamatwa na polisi kwa
sababu ambazo hadi sasa hazijawekwa wazi.
Calist
Lazaro ambaye ni meya wa Jiji la Arusha naye alijikuta akisekwa rumande
kwa amri ya mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo kwa madai ya kufanya
mkusanyiko usio halali wakati akijiandaa kupeleka rambirambi Shule ya
Lucky Vincent iliyopoteza wanafunzi 32, walimu wawili na dereva wa gari
katika ajali iliyotokea wilayani Karatu.
“Hili
ni vyema likajadiliwe na kikao na tuwaulize na tuwashirikishe wananchi
wetu kwenye uamuzi tutakaouchukua na baada ya hapo tuseme ‘imetosha, na
tuchukue hatua’,” alisema.
Lowassa
alisema ni lazima Kamati Kuu ikutane na kujadaliana kuhusu tabia hiyo
aliyoiita ya kubughudhiwa kwa viongozi wa Chadema, hasa wa kuchaguliwa
jambo ambalo si jema.
Pia,
mwanasiasa huyo ambaye alikuwa akivuta hadhira kubwa wakati wa kampeni
za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, alisema kuzuia mikutano ya hadhara imetosha
kwa kuwa wanasiasa wengine, kama Rais John Magufuli wanazunguka sehemu
mbalimbali na kuzungumza na wananchi.
Alisema
mkuu wa wilaya anateuliwa na rais wakati meya wa manispaa anachanguliwa
na wananchi, hivyo mwenye wajibu mkubwa wa kuongoza manispaa ni
kiongozi anayechaguliwa na wananchi.
“Kitendo
cha kuwakamata na kuwaweka ndani viongozi wetu si kizuri, ni
kuwadhalilisha na hili halijafanyika Ubungo hata Arusha limetokea.
Hatuwezi kuruhusu jambo hili likaendelea na likiendelea ni makosa,”
alisema.
“(Jacob) Nakupa pole ya dhati na masikitiko kwa yaliyokupata juzi,” alisema akigeukiwa kwa meya huyo wa Ubungo.
Kuhusu
katazo la mikutano ya hadhara, Lowassa alisema wapinzani wananyimwa
fursa hiyo lakini akadai upande wa pili wanafanya na kasi yao imezidi
kuongezeka.
“Rais
anazunguka na viongozi wa chama. Pia nimewasikia wanafanya maandamano
nchi nzima kumuunga mkono rais. Wao kufanya ni halali sisi ni haramu
katika nchi hii na watu walewale, (hiyo) si demokrasia,” alisema.
Akipewa
nafasi ya kutoa neno la shukrani kwa niaba ya madiwani wenzake, Jacob
alielezea kwa kina alivyowekwa mahabusu kwa 48, akisema alikuwa na
hasira, lakini busara zilimuongoza na kuamua kumsamehe mkuu wa Wilaya ya
Ubungo, Kisare Makori kwa sababu tatu.
“Sababu
ya kwanza nimepokea pole na masikitiko yake wakati nikiwa mahabusu;
pili hakuwa na namna na siyo kosa lake. Najua kuna mtu alimtuma kufanya
hivyo na kama asingefanya kibarua chake kingekuwa mashakani,” alisema.
“Tatu
ni muungwana na ninaahidi kufanya naye kazi bega kwa bega, ila naomba
mtambue taarifa nilizozipata ni kwamba DC alipata maagizo na sina haja
ya kumtaja hapa,” alisema Jacob.
Meya
huyo alisema ana taarifa nyingine kwamba kazi ya kumkamata na kumuweka
mahabusu ilitakiwa ifanyike siku nyingi, lakini alikuwa makini.
Alisema kuna watu wana lengo la kumrudisha nyuma kutokana na kazi nzuri anayoifanya.
Pia,
alisema hana sababu ya kumlaani wala kumtenga Makori kwa kuwa alipewa
amri na kwamba haikuwa kosa kwake kufanya mkutano na viongozi wa Chadema
katika ukumbi wa halmashauri.
“Nikiwa
diwani wa Manispaa ya Kinondoni nilibahatika kupata kalenda tano ambazo
zipo nyumbani kwangu na baadhi ya picha zilizomo katika kalenda hizo
zinaonyesha meya na viongozi wa CCM wakikagua miradi mbalimbali ikiwamo
ya shule na madaraja,” alisema Jacob.
Alisema
tatizo ni kuonekana kwa Sumaye katika eneo hilo, hali ambayo ingewapa
wakati mgumu viongozi wa wilaya hiyo ambao wangeshindwa kuwaeleza
wakubwa wao.
“Mimi
ni shujaa na ngangari katika masuala ya mahabusu. Ile mahabusu ya saa
48 ilikuwa soft (laini) kwangu. Katika safari yangu ya kisiasa nimekaa
jela mara nne na mahabusu 16, ikiwamo ya Stakishari ila ya Mbezi
sikuwahi kukaa kwa sababu ni mpya,” alisema na kuongeza kuwa: “Msinipe
pole nipeni hongera na kituo hiki cha polisi wa Mbezi nimeahidi
kukipelekea rangi na vifaa vya usafi kwa ukarabati zaidi,” alisema Jacob
ambaye ni diwani wa Ubungo (Chadema).
Hata
hivyo, Jacob aliungana na Lowassa kuhusu kuitishwa kwa kikao cha Kamati
Kuu na kuwaeleza Watanzania kwamba yeye atakuwa mwanasiasa wa mwisho
kuwekwa ndani kwa amri ya wakuu wa mikoa na wilaya.
Alisema
atahakikisha anaipingania kwa nguvu zote ikiwamo kisheria amri ya wakuu
wa mikoa na wilaya ya kuwaweka ndani baadhi ya watu wakiwamo viongozi
wa upinzani kwani jambo hilo likiachwa litawaathiri wananchi wengine.
0 comments:
Chapisha Maoni