Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene amemteua Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Davis Mwamfupe kuwa diwani
katika Manispaa ya Dodoma.
Juzi
Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Godwin Kunambi alimtaja Profesa
Mwamfupe pamoja na wenzake wawili Roze Nitwa (CCM) na Vicent Tibalindwa
(Chadema) kuwa waliteuliwa na Waziri kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo.
Kunambi
alisema Simbachawene aliteua majina sita kwa vyama vya Chadema na CCM
ndipo wakayapigia kura likiwamo jina la Mwamfupe aliyetokea CCM.
“Waziri
alitumia sheria namba 288 (24) (2d) ya Serikali za mitaa na kanuni za
uteuzi za mwaka 2010 sura ya 4 (1) na 5 (1) vinavyompa mamlaka ya
kufanya hivyo bila kuulizwa na humteua mtu ambaye ni mkazi wa eneo
husika,” alisema Kunambi.
Manispaa
ya Dodoma haina Meya baada ya Jaffary Mwanyemba kuondolewa na madiwani
Machi mwaka huu kwa madai ya matumizi mabaya ya madaraka.
Hata
hivyo, Mkurugenzi huyo alikana madai ya kumwandaa msomi huo wa uchumi
katika nafasi ya Umeya ingawa alisema kila mtu mwenye sifa za kuwa
diwani ana haki ya kugombea nafasi ya uongozi ikiwamo meya.
Mkurugenzi
huyo aliwaondoa hofu waliokuwa wamejenga nyumba zao katika maeneo
ambayo hayajapimwa kabla ya kuvunjwa kwa CDA akisema hawatasumbuliwa
badala yake watarasimishwa huku akitoa tahadhari kwa wavamizi wa maeneo
na viwanja kuwa lazima watavunjiwa.
Naibu
Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jumanne Ngede alisema baraza la madiwani
halina shaka na uteuzi huo na kwamba watapewa ushirikiano katika
kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ikiwamo mchakato wa makao makuu.
Alisema
mpango uliopo katika manispaa hiyo ni kujipanga kuwa na ugeni mkubwa
ambao umeingia mkoani hapo ikiwemo maofisa wa serikali.
Mmoja
wa madiwani ambaye hakupenda kutajwa jina lake alisema mpango wa uteuzi
wa msomi huyo unaweza kuwagawa madiwani kwani kuna kila dalili za
kuandaliwa kushika kiti hicho huku wengine wakitaka apewe nafasi katika
kamati ya uchumi na fedha tu ili akaonyeshe uzoefu wake huko.
0 comments:
Chapisha Maoni