Ujanja wa kisheria uliosababisha mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kukaa mahakamani kwa saa 10, umemfanya kada huyo wa Chadema kukosa tena dhamana.
Jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi ilishatupilia mbali hoja za Serikali za kupinga dhamana ya mbunge huyo, lakini mawakili walitumia silaha nyingine ya kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa kumpa dhamana Lema.
Jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi ilishatupilia mbali hoja za Serikali za kupinga dhamana ya mbunge huyo, lakini mawakili walitumia silaha nyingine ya kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa kumpa dhamana Lema.
Mawakili wa Serikali walifanya hivyo muda mfupi baada ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Desderi Kamugisha kutupa hoja za kuzuia dhamana ya Lema na hivyo kumzuia hakimu kuendelea na utaratibu wa kumwachia mbunge huyo kusubiri uamuzi wa rufaa hiyo, hali iliyoibua vilio mahakamani.
Kutokana na maamuzi hayo, hatma ya Lema kupata dhamana inasubiri Mahakama Kuu kupanga jaji wa kusikiliza shauri hilo.
Lema, ambaye alifikishwa mahakamani saa 2:00 asubuhi, alirudishwa mahabusu akiwa kwenye basi la magereza lililokuwa na ulinzi mkali saa 11:00 jioni.
Katika uamuzi wake uliotupilia hoja za awali za Serikali kupinga dhamana, Hakimu Kamugisha alisoma maamuzi kwa saa 2:35 na kutoa dhamana kwa Lema.
Hakimu Kamugisha alisema upande wa mashtaka uliwasilisha hoja tatu za kupinga dhamana ya Lema katika kesi za uchochezi namba 440 na 441/2016 na hati ya kiapo ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha(RCO).
Alisema hoja ni kuwa mshtakiwa ametenda makosa hayo, wakati akiwa nje kwa dhamana kwa kesi namba 351 na 352 za mwaka 2016, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Hakimu Kamugisha alisema hoja nyingine ni kutaka Lema anyimwe dhamana kwa ajili ya kulinda usalama wake, hasa kwa kuwa kauli zake za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli zimewaudhi wananchi.
Hoja ya tatu kujali maslahi ya Taifa. Hoja hizo ziliandamana na hati hiyo ya kiapo cha RCO.
Hata hivyo, hakimu alisema mawakili wa utetezi waliokuwa wanaongozwa na John Mallya walipinga hoja hizo, wakisema dhamana ni haki ya mshitakiwa na kuwa nje kwa dhamana katika mashauri mengine ambayo hayajamtia hatiani mtuhumiwa, hayawezi kuwa sababu ya kumnyima dhamana.
Alisema mawakili hao, pia walipinga hoja za kutokutolewa dhamana kutokana na usalama wake na maslahi ya Jamhuri na pia wakakosoa hati ya kiapo kuwa ina mapungufu, hasa ya kutokuwa na uthibitisho wa mambo yaliyoelezwa.
Hakimu Kamugisha alisema msingi wa haki ya dhamana ni wa Katiba ibara ya 15(1) na (2) ambayo inaelezea uhuru wa mtu.
Alisema pia ibara ya 17 ya Katiba inatoa haki ya mtu kutembea popote na kuongeza ibara ya 16(6) B inaeleza mahakama inamchukulia mtuhumiwa yeyote kuwa hajafanya kosa hadi anakapotiwa hatiani.
Alisema washitakiwa hupelekwa mahabusu ili iwe lazima mtuhumiwa kufika mahakamani.
Hakimu Kamugisha alisema, siku zote dhamana haitolewi ikiwa tu kuna mazingira ya kisheria ambayo yameelezwa na kuwekewa masharti na utaratibu wake.
Alitolea mfano kesi ya Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP) dhidi ya Daudi Beda ambapo ilielezwa haki za mshtakiwa na sababu ambazo zinaweza kuzuia dhamana.
Alisema katika kesi hiyo, mahakama iliamua kuwa ili kunyimwa dhamana lazima kuwepo mazingira yaliyoanishwa kisheria na utaratibu ulioanishwa kisheria.
“Nimeshindwa kupata kifungu chochote cha sheria ambacho kinazuia kutoa dhamana kwa mtuhumiwa aliye nje kwa dhamana ambaye ametenda makosa mengine ambayo hayahusiani na masharti ya dhamana ya awali,” alisema.
Alisema hata maelezo kuwa watu waliohudhuria mkutano hawakuridhishwa na kauli za Lema na kwenda kulalamika kwa RCO, hayana panapoonyesha usalama wa mtuhumiwa upo mashakani.
Alisema ili hoja ya dhamana izuiwe kwa maslahi ya Jamhuri, inakuwa na hati ya maombi hayo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP) na si RCO hivyo haoni msingi wa kutotoa dhamana hiyo “Hivyo kwa uchambuzi huu wa kisheria natoa dhamana kwa mshitakiwa,” alisema.
Hata hivyo, wakati anajiandaa kuandika masharti ya dhamana, ndipo wakili mwandamizi wa Serikali, Paul Kadoshi aliwasilisha notisi za kupinga uamuzi wa dhamana hiyo.
Alisema anawasilisha notisi hiyo chini ya kifungu cha 379 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 ya mwaka 2002.
Alisema nia ya kuwasilisha notisi hiyo inatokana na mabadiliko ya Sheria za Makosa ya Jinai namba 27 ya mwaka 2008.
Alisema kifungu cha 31 aya G katika sheria hiyo kifungu 379(1 ) (a) kwa kuongeza maneno kuwa notisi ya kukata rufaa inaweza kujulikana kama ni rufaa.
Alisema mabadiliko ya sheria hiyo yalimpa hadhi DPP anapoeleza notisi ya rufani kuwa tayari ni rufani kamili na hivyo notisi hiyo ikitolewa mwenendo wa kesi nzima unapaswa kusimama.
Kadoshi alisema maamuzi hayo, yamefikiwa katika kesi ya Jamhuri dhidi ya Harry Kitillya na wenzake wawili, pale DPP alipowasilisha notisi na rufani na kesi kusimama.
Hata hivyo, licha ya mawakili wa utetezi, Sheki Mfinanga na Richard Shediel kupinga hoja hiyo, Haklimu Kamugisha, ambaye aliomba dakika 10 kutafakari suala hilo, alikubaliana na hoja za upande wa Serikali za kumkatalia Lema dhamana.
Kutokana na maamuzi hayo Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu amesema chama hicho kimewataka wanasheria wake, Tundu Lissu na Peter Kibatala kwenda Arusha kuongeza nguvu katika kudai haki ya Lema kuwa huru.
Mke wa Lema, Neema Lema aliwataka wakazi wa Arusha kuwa watulivu, akisema mbunge huyo anapigania uhuru wa wananchi.