test

Ijumaa, 12 Mei 2017

Waziri Mwakyembe aipongeza Klabu ya Afrika Lyon kwa kuwa Wazalendo



 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akifafanua jambo wakati wa kikao na uongozi wa Klabu ya michezo ya Afrika Lyon katika  ukumbi wa Idara ya Habari maelezo leo Jijini Dar es Salaam, kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Patrick Kipangula na kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Klabu ya afrika Lyon Bw.Rajuu Kagenzi.
 Mtendaji Mkuu wa Klabu ya afrika Lyon Bw.Rajuu Kagenzi (kushoto) akiongea wakati wa kikao na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) na kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Patrick Kipangula  .

 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akipokea jezi kwa niaba ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya afrika Lyon Bw.Rajuu Kagenzi (kushoto) mara baada ya kikao na uongozi huo leo Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akionyeshwa michora ya ramani za viwanja vya michezo vinavyotarajiwa kujengwa kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya afrika Lyon Bw.Rajuu Kagenzi (kushoto) leo Jijini dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa uongozi wa Klabu ya michezo ya Afrika Lyon katika  ukumbi wa Idara ya Habari maelezo leo Jijini Dar es Salaam. (Picha na Lorietha Laurence-WHUSM)



Na Lorietha Laurence

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe  ameupongeza uongozi wa Klabu ya michezo ya Afrika Lyon kwa kutumia  mchezo wa mpira wa miguu kuelimisha jamii kupambana na ujangili wa tembo.

Waziri Mwakyembe ametoa pongezi hizo leo Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na uongozi wa klabu hiyo katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO.

Katika kikao hicho uongozi wa timu hiyo ulimueleza Waziri kuwa timu yao imeamua kushiriki vita dhidi ya vitendo vya mauaji ya tembo kwa kuandika ujumbe maalum katika jezi za timu hiyo kuelimisha jamii dhidi ya vitendo hivyo.  

“ni jambo zuri kuhakikisha jamii inapata burudani ya mpira wakati huo huo inaelimika kupitia ujumbe unatolewa na wachezaji katika jezi zao”Dkt Mwakyembe alisema.

Kwa hivyo, aliushukuru uongozi wa timu hiyo kwa juhudi zao hizo na kukieleza kitendo hicho kuwa ni “cha mfano na kujivunia”.
Aliongeza kuwa Serikali inajivunia na kuthamini mchango wa wananchi wazalendo wanaojitolea kujenga taifa na kulinda rasilimali zake kama timu ilivyofanya timu hiyo.

Aidha Waziri  Dkt. Mwakyembe aliongeza kuwa ni jambo jema linalofanywa na klabu hiyo katika kuhakikisha  inakuza  na kuendeleza vipaji kwa vijana mbalimbali nchini jambo ambalo linasaidia kuinua sekta ya michezo.

Pia aliwapongeza kwa kupata fursa ya kutembelea nchi ya China kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu michezo na kuwataka kuitumia fursa hiyo ipasavyo kwa kujifunza kwa bidii ili watakaporejea waweze kufundisha vijana wengine wa kitanzania.

Naye Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Afrika Lyon Bw. Rajuu Kangezi ameeleza kuwa mkakati wa klabu hiyo ni kuhakikisha kuwa inajenga viwanja vya michezo vya kisasa kwa matumizi ya jamii ili kuendeleza michezo nchini  hivyo ameomba ushirikiano na serikali katika kufanikisha mikakati hiyo.

“Tuna mipango mingi ya kuhakikisha tunakuwa na viwanja vizuri vya michezo na hili haliwezi kufanikiwa bila kuishirikisha serikali na viongozi wake hivyo tunaomba ushirikiano wa serikali katika kuhakikisha tunafanikisha jambo hili”

Katika kikao hicho uongozi wa klabu hiyo ulimkabidhi Waziri Mwakyembe jezi namba tano “5” ya klabu hiyo kwa ajili ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

MKUU WA WILAYA AONGOZA KILELE CHA SIKU YA WAUGUZI KISHAPU

 Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba akiwa amembeba mtoto aliyezaliwa katika Hopsitali ya Wilaya (Dk. Jakaya Kikwete) wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani kiwilaya.
 Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabaganga Talaba akimpa msaada mmoja wa mama anayeuguza mtoto katika hopsitali ya wilaya.
 Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba akizungumza na wauguzi (hawapo pichani) katika sikukuu ya Wauguzi Duniani viwanja vya hospitali ya wilaya.
 Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kangese akitoa neno kumkaribisha mgeni rasmi mkuu wa wilaya
 Wauguzi wakila kiapo cha utii wakati wa sikukuu hiyo.

Wauguzi wilayani Kishapu wamepongezwa kwa kazi nzuri na kutakiwa kuendelea kuipenda kazi yao kuchapa kazi katika mazingira yoyote waliopo kwani wao ni chachu ya afya katika jamii.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabaganga Talaba wakati kwenye kilele cha Siku ya Wauguzi Duniani iliyofanyika katika viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya DK. Jakaya Kikwete.  
Talaba ambaye aliwaongoza wauguzi hao na watumishi wa halmashauri kutoa misaada na kufariji wagonjwa hospitalini hapo aliwapongeza kwa huduma nzuri kwa wagonjwa.

Alisema kuwa bila ya wauguzi afya haijakamilika na kuwa uuguzi ni zaidi ya wito na ni huduma inayohitaji upendo na huruma kwa wale unaowahudumia.

“Kama huna upendo na ukarimu basi wewe siyo muuguzi na ukionesha ukarimu na upendo ndiyo mwanzo wa kupona kwa mgonjwa ukifika tu pale mgonjwa anapona hata kabla hujampa dawa,” alisisitiza.
Aidha, aliwataka wauguzi waendelee kuwa na ushirikiano baina yao huku akiwapongeza kwa mafanikio katika sekta ya afya pamoja na kuwa wana changamoto ya mazingira ya kazi.

Mkuu huyo wa wilaya aliwaomba kuendelea kutimiza wajibu na kuzingatia viapo vyao vya uuguzi na kanuni za utumishi huku akionya kushindwa kufanya hivyo ni kukiuka taratibu za kazi na hivyo kutengeneza migogoro isiyo ya lazima.

Kwa upande wake, Kaimu Muuguzi Mkuu Hospitali ya wilaya hiyo ya Dk. Jakaya Kikwete, Rehema Jumanne akisoma risala alitaja mafanikio yaliyopatikana kuwa ni mafunzo kazini.Alisema mafunzo hayo yamesaidia wauguzi kuboresha huduma za jamii zikiwemo uzazi wa mpango, huduma za dharura kwa wajawazito na kusaidia wachanga kupumua.

Pia alitaja mafanikio mengine ni kuendeleza wauguzi katika ngazi za juu za elimu na hivyo kutoa huduma kwa kiwango cha juu pamoja na kutoa huduma bora tofauti na mazingira yao.

Hata hivyo alisema kuna changamoto ya uhaba wa watumishi hiyo husababisha kutokuwepo kwa uwiano sawia wa watumishi katika kutoa huduma katika vituo vya afya na zahanati mbalimbali katika wilaya hiyo.
Siku ya Wauguzi Duniani huadhimisha kila Mei 12 ikiwa ni kumuenzi  muuguzi mwanzilishi Florance Nightingale aliyoanzisha mwaka 1844 ambapo kaulimbiu ni Wauguzi, mbiu ya kuyafikia malengo endelevu ya millennia.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx