test

Jumatano, 21 Septemba 2016

Wanachama wa CUF Waonyesha Jeuri ya Pesa


Wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF)  wamesema wapo tayari kugharamia matibabu ya Katibu Mkuu wa chama chao, Maalim Seif Sharif Hamad.

Tamko hilo limetolewa siku chache baada ya kuibuka taarifa kuwa  kiongozi huyo amesusa gharama za matibabu zinazotolewa na Serikali ingawa ni haki yake kwa mujibu wa sheria kama kiongozi mstaafu.

Akizungumza   kwa niaba ya wanachama wenzake kisiwani Unguja jana, mmoja wa wanachama wa CUF, Ali Abdallah Issa, alisema wanashangazwa na baadhi ya watu kumpiga na kumsema kiongozi huyo ambaye alidai ni kiungo muhimu katika kuwaunganisha Wazanzibari.

“Maaalim ana haki zote za kuhudumiwa na Serikali na si vinginevyo. Lakini kwa manyanyaso na kusimangwa  kila kukicha sisi wanachama wa CUF tupo tayari kugharamia matibabu ya kiongozi wetu.

“Na hili si jambo geni, Maalim alikamatwa na kuwekwa kuzuizini.  Je, alipotoka  alikuwa akitibiwa na SMZ? Jibu ni hapana ni fedha zake mwenyewe binafsi pamoja na wana CUF ambao walikuwa mstari wa mbele kumhudumia kiongozi wetu nasi sasa tutafaya hivyo ikiwa SMZ imeshindwa,” alisema Ali.

Alisema kitendo cha Maalim Seif kusafiri nje ya nchi kwa matibabu bila ya huduma za Serikali hakileti picha nzuri.

Kuna hatari visiwa vya Zanzibar vikaingia katika mgogoro na kujengeka   chuki hasa kati ya CUF na CCM, alisema.

‘’Iwapo Maalim Seif amekwenda kwenye matibabu kwa gharama zake binafsi basi inasikitisha sana kuona ni jinsi gani Katiba inavyoanza kukiukwa na kwa kweli si jambo jema na halifai,” alisema.

Naye Is-hak Said Makame, alisema   Zanzibar imepita katika wakati mgumu hasa baada ya kutokea   migogoro ya siasa iliyotokana na Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana  na ule wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu.

“Maalim hawezi kusemwa na hata kuonekana ni kiongozi anayetibiwa kwa fadhila kama alivyotaka Rais Magufuli alipokuja hapa Unguja kwenye mikutano yake. Sasa tunasema sisi CUF tutamlinda kiongozi wetu kwa hali na mali,”alisema Makame.

Alipotafutwa  Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa CUF, Salim Biman  kujua  Maalim Seif  amepata wapi fedha kwa ajili ya safari ya nje ya nchi kutibiwa.

Alisema  hajui ni wapi kiongozi huyo alipopata fedha za matibabu.

“Katibu Mkuu amekwenda India kwa ajili ya uchunguzi wa kawaida wa afya yake lakini nasi hatujui ni wapi amepata fedha. Ila atakaporejea nchini itatolewa taarifa kwa kina kuhusu suala hili,” alisema Biman.

Maalim Seif yuko   India na anatarajiwa kujerea nchini siku chache zijazo.

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx