Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani DCP Mohamed Mpinga amesema jeshi hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi kavu SUMATRA wameanza mchakato wa kumtafuta mtoa huduma ambaye atafunga na kuanzisha mfumo maalum wa kupima mwendokasi wa magari tofauti na mfumo uliopo kwa sasa ambao unaonekana kuwa na mapungufu.
Kamanda Mpinga ameyasema hayo kwenye mahojiano maalum na East Africa na kuainisha changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa mfumo wa sasa ni pamoja na tatizo la kukosekana kwa mawasiliano ya Internet kwa baadhi ya maeneo na miundombinu mibovu ambayo inasababisha kifaa hicho kupoteza mawasiliano na mamlaka inayokisimamia.
Amesema kufuatia kukua kwa teknolojia katika ulimwengu wa sasa ofisi yake inatafuta pesa ambazo zitawezesha kununua na kufunga mfumo mpya wa 'Speed Radar' kila eneo linalopitiwa na barabara nchini lengo likiwa ni kutambua na kuzikamata gari zinazokiuka sheria za usalama barabarani, kukamata magari yaliyoibiwa na kudhibiti uhalifu mbalimbali ambao utamulikwa na kamera hizo.