Saturday 23rd July 2016
Chanzo :Ikulu
Ndugu Mwenyekiti Mstaafu, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete;
Mzee Ali Hassan Mwinyi na Mzee Benjamini William Mkapa, Wenyeviti Wastaafu wa CCM;
Makamu Wenyeviti wa CCM, Dkt. Ali Mohamed Shein (kwa upande wa Zanzibar) na Mzee Philip Japhet Mangula (upande wa Tanzania Bara);
Makamu Wenyeviti Wastaafu mliopo hapa, Waasisi/Wazee Wastaafu wa CCM;
Katibu Mkuu, Ndugu Abdulrahman Kinana;
Wajumbe wa Kamati Kuu;
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa;
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa;
Viongozi wa Jumuiya mbalimbali za Chama;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa mliopo;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi mbalimbali za Kimataifa mliopo;
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana:
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI!
Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima na kutukutanisha hapa tukiwa na afya njema. Leo ni siku muhimu na ya kihistoria katika maisha yangu na kwa Chama chetu kwa ujumla. Ni siku ambayo wanaCCM kwa mara nyingine mmedhihirisha imani yenu kwangu kwa kunichagua kwa kura za kishindo kuwa Mwenyekiti wa Tano wa Chama chetu. Nawashukuru sana kwa heshima kubwa mliyonipatia na nawathibitishia kuwa nimeipokea heshima hii kwa moyo mkunjufu na unyeyekevu mkubwa.
Natambua kuwa jukumu mlilonipa siyo rahisi. Ni jukumu kubwa na zito. Lakini nina imani nitaliweza. Nitaliweza kwa sababu kwanza siko peke yangu. Nipo na ninyi wanaCCM wenzangu. Kwa kushirikiana nanyi tutatekeleza jukumu hili kwa pamoja. Pili, naamini nitaweza kwa sababu, uzuri wa Chama chetu ni kuwa kinaendeshwa kwa mujibu wa Katiba, Sheria, Kanuni na Taratibu. Hivyo, kwa kutumia miongozo hiyo nina imani kubwa kuwa kazi yangu haitakuwa ngumu. Jambo la muhimu itakuwa ni kufuata miongozo hiyo. Tatu, naamini nitaweza kwa sababu mimi siyo mgeni katika Chama. Nimekuwa mwanachama mwadilifu na mwaminifu wa CCM kwa takriban miaka arobaini, kipindi ambacho kimeniwezesha kukijua Chama. Najua kilikotoka, kinavyoendeshwa na wapi kinapaswa kuelekea. Hivyo basi, naahidi kutumia uwezo na uzoefu wangu wote kutekeleza majukumu yangu ya Chama na kamwe sitawaangusha.
Ndugu Mwenyekiti Mstaaf;
Ndugu Viongozi na WanaCCM wenzangu;
Sisi binadamu tumeumbwa kuwa watu wa kushukuru hasa tunapotendewa mambo mema na mazuri na wenzetu. Tukio hili la leo linatokea takriban mwaka mmoja tangu mliponichagua na kuniteua kuipeperusha Bendera ya Chama chetu katika kinyang’anyiro cha Urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Hata baada ya kunichagua, hamkuniacha peke yangu. Mliambatana na mimi bega kwa bega katika kipindi chote cha kampeni ili kuhakikisha Chama chetu kinaibuka na ushindi. Sote tunafahamu, Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulikuwa na ushindani na changamoto nyingi. Hata hivyo, tulishirikiana na kushikamana na hatimaye Chama chetu kilipata ushindi mkubwa na mimi kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hakika ushindi tulioupata ni matokeo ya juhudi za pamoja za wanaCCM wote. Binafsi najiona kuwa ni mwenye deni kubwa sana kwenu wanaCCM na Watanzania kwa ujumla. Sina cha kuwalipa. Lakini itoshe tu kusema kuwa nawashukuru sana, tena sana, kwa ushirikiano mkubwa mlionipa wanaCCM wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Kupitia kwenu, nawashukuru Watanzania wote wa vyama vyote, dini zote na makabila yote kwa kunichagua kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa nchi yetu.
Nafahamu wakati wa kutoa shukrani si vizuri sana kutaja majina au kumshukuru mtu mmoja mmoja. Hii ni kwa sababu unaweza kumsahau mtu muhimu akajisikia vibaya. Hata hivyo, naomba mniruhusu niwashukuru angalau wachache kwa kuwataja majina.
Katika maisha yangu siwezi kusahau mchango mkubwa wa Mzee Ali Hassan Mwinyi. Mzee Mwinyi akiwa Mwenyekiti wa CCM ndiye alisimamia kikao cha Chama kilichoniteua mimi kwa mara ya kwanza kugombea Ubunge wa Jimbo la Biharamulo Mashariki mwaka 1995. Kama Mzee Mwinyi angekata jina langu siku ile, huenda leo mimi nisingekuwa hapa. Nakushuruku sana Mzee wangu Mwinyi maana huo ulikuwa ndiyo mwanzo wa safari yangu ya uongozi. Pili, ninamshukuru pia Mzee Benjamini William Mkapa ambaye aliniteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi mwaka 1995 mara tu baada ya kuchaguliwa kuwa Mbunge. Mwaka 2000 akiwa Mwenyekiti wa CCM aliniteua kugombea Ubunge na nilipochaguliwa alinifanya kuwa Waziri kamili wa ujenzi hadi mwaka 2005. Nashukuru kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kugombea Ubunge na kuniteua kwa nafasi ya Uwaziri tena bado nikiwa na umri mdogo. Mzee Mkapa ahsante sana.
Ninamshukuru Mzee Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ambaye aliendelea kunilea katika uongozi kwa kuniteua kuwa Waziri wa Wizara mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Wizara ya Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi pamoja na Wizara ya Ujenzi. Kwa Mzee Kikwete mbali ya kupitisha jina langu kugombea Ubunge wakati akiwa Mwenyekiti wa CCM mwaka 2010 aliamua kujitishwa mzigo mzito wa kusimamia mchakato wote wa kumpata Mgombea Urais 2015, akaniamini hadi kuteuliwa na mikutano husika ya CCM. Kwa Mzee Kikwete pia nimejifunza mambo mengi lakini kubwa zaidi ni uvumilivu na ustamilivu. Nasema kwa dhati kabisa kuwa Mzee huyu ni mvumilivu na mstamilivu sana. Amesemwa mambo mengi kwa ajili yangu. Nakumbuka mara kadhaa aliniomba kunikabidhi Uenyekiti wa Chama lakini mimi nilikataa. Baadhi ya watu wakamzushia maneno kuwa ameng’ang’ania Uenyekiti lakini alibaki kimya. Binafsi sitasahau siku ile ya uteuzi wangu kuwa Mgombea Urais wa Chama chetu. Nakumbuka namna ambavyo baadhi ya wanachama walionesha utovu mkubwa wa nidhamu kwake lakini alibaki kuwa mtulivu na akashirikiana na viongozi wa Chama hatimaye mchakato wa kupata mgombea Urais ulikamilika kwa amani. Ni viongozi wachache wenye uvumilivu na ustahimilivu wa namna hii. Binafsi sina cha kumlipa zaidi ya kutoa ahadi ya kufanya kazi kwa bidii ili kumuenzi.
Mbali na viongozi hawa wakuu watatu, napenda pia kuwashukuru Makamu Mwenyekiti (Bara) Mzee Mangula; Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Dkt. Shein; Katibu Mkuu Mzee Kinana; Manaibu Makatibu Wakuu kwa upande wa Bara na Zanzibar; Wazee Waasisi wa CCM upande wa Tanzania Bara na Zanzibar, Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu; Wajumbe wa Mkutano Mkuu na WanaCCM wote kwa kuonesha imani mkubwa kwangu. Naahidi nitaendelea kuwaenzi na kutafuta ushauri wenu katika uongozi wangu. Wazee pamoja na viongozi wengi wa CCM wameishi na kuona mengi katika uongozi. Sisi viongozi wa leo hatuna budi kuiga na kudumisha mambo mema kutoka kwenu. Ahsanteni sana WanaCCM wenzangu.
Ndugu Mwenyekiti Mstaafu;
Ndugu WanaCCM wenzangu;
Chama chetu ni kikongwe siyo tu hapa nchini bali pia Barani Afrika na duniani kwa ujumla. Mwakani kitafikisha miaka arobaini (40) tangu kilipozaliwa kufuatia kuunganishwa kwa vyama mama vilivyopigania uhuru wa nchi yetu vya TANU na Afro Shiraz Party. Mtakubaliana nami kuwa katika kipindi cha takriban miaka 40 ya uhai wake, Chama chetu kimepata mafanikio mengi. Kwa haraka haraka, nitaje baadhi ya mafanikio ya chama chetu, mengine yametajwa na Mwenyekiti Mstaafu:
- Kwanza, tumeendelea kuongoza dola ambalo ni lengo kuu la chama chochote cha siasa. Watanzania wameendelea kutuamini kwa kutupa dhamana kubwa ya kuongoza nchi yetu tangu mwaka 1977 wakati nchi yetu ilikuwa ikiendeshwa kwa mfumo wa chama kimoja hadi sasa katika mfumo wa vyama vingi ulioanza mwaka 1992;
- Pili, Chama chetu kimeendelea kuwa chama kinachoaminiwa katika Afrika na duniani kote kama chama kinachotetea na kinachoendelea kutetea uhuru, umoja na mshikamano kwa vyama vingine vya ukombozi katika Afrika na duniani kote.
- Tatu, Chama chetu kimeendelea kulinda na kudumisha Muungano wa nchi yetu. Muungano wetu upo tena ni imara na umebaki kuwa imara na mfano wa kuigwa duniani. Nitaendelea kuulinda Muungano huu kwa nguvu zangu zote;
- Nne, tumelinda na kudumisha amani na utulivu pamoja na umoja na mshikamano wa nchi yetu. Tanzania imeendelea kuwa kisiwa cha amani na watu wake ni wamoja licha ya tofauti za kisiasa, dini, kabila au maeneo wanakotoka;
- Tano, tumeendelea kuwaongoza Watanzania katika harakati za kuleta maendeleo katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii kufuatana na mabadiliko mbalimbali yanayojitokeza ndani na nje ya nchi. Hali ya maisha ya Watanzania hivi sasa ni bora Zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 1977; na
- Sita, tumelea na kukuza demokrasia nchini. CCM kimeendelea kuwa babu na bibi, baba na mama, lakini pia kaka na dada wa vyama vyote nchini.
Kwa hakika haya ni mafanikio makubwa ya wanaCCM na Watanzania kwa ujumla. Wahenga husema “usione vyaelea, vimeundwa”. Hivyo basi, kila mwanaCCM hana budi kutembea kifua mbele na kujivunia mafanikio tuliyoyapata. Lakini hatupaswi kubweteka kwa vile bado tuna kazi kubwa ya kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo zaidi. Moja ya azimio la Mkutano Mkuu wa Taifa wa Pamoja wa TANU na Afro Shiraz Party uliofanyika mjini Dar es Salaam tarehe 21 Januari, 1977 wakati wa kuunganisha vyama vya TANU na Afro Shiraz Party na kuzaliwa kwa CCM lilikuwa, napenda kunukuu “Chama tunachokiunda tunataka kiwe chombo madhubuti katika muundo wake na hasa katika fikra zake na vitendo vya kimapinduzi vya kufutilia mbali aina zote za unyonyaji nchini, kupambana na jaribio lolote lile la mtu kumwonea mtu au shirika au chombo cha nchi kuonea na kudhalilisha wananchi, kudhoofisha uchumi au kuzorotesha maendeleo ya Taifa”, mwisho wa kunukuu. Endapo tukitathmini na kutafakari kwa kina azimio hili la tarehe 21 Januari, 1977, bila shaka mtakubaliana nami kuwa, licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana, bado Chama chetu na nchi yetu inakabiliwa na changamoto.
Changamoto hizo ni pamoja na kuendelea kwa tatizo la umaskini; ukosefu wa ajira; kuendelea kwa vitendo vya dhuluma, ufisadi, rushwa, ubadhirifu wa mali za umma; na pia kukosekana kwa huduma bora zaidi za kijamii, ikiwemo elimu, afya, maji na umeme. Hivyo basi, Chama chetu hakina budi kujipanga vizuri na kuchukua hatua mahsusi za kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na taifa letu kwa ujumla. Tukishindwa kutatua changamoto hizo na kutimiza matarajio ya wananchi, tutapoteza mvuto na Watanzania watakosa imani na sisi. Hatupaswi kuruhusu hali hii kujitokeza. Tanzania imara na yenye mafanikio inatutegemea sisi.
Ndugu WanaCCM wenzangu;
Katika kipindi changu cha uongozi nimedhamiria kushirikiana na viongozi, watendaji na kila mwanachama katika ngazi zote ili kuhakikisha Chama chetu kinakuwa imara zaidi. Kwa kushirikiana nanyi, nitafanya kila jitihada kuhakikisha Chama chetu kinakwenda sambamba na hali ya sasa lakini bila kuathiri misingi madhubuti iliyojengwa na waasisi na viongozi wetu waliotangulia, yaani Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Abeid Amani Karume. Ili kutekeleza azma hiyo natarajia kufanya mambo yafuatayo kwa kushirikiana nanyi:
Kwanza, Kuimarisha utendaji kazi wa Chama. Suala la kuimarisha utendaji wa chama ni muhimu sana. Kama alivyokuwa akisema Baba wa Taifa letu Mwalimu Nyerere kuwa “Chama legelege huzaa Serikali legelege”. Nitashirikiana nanyi kujenga Chama madhubuti chenye uwezo wa kuisimamia vizuri Serikali ili itekeleze ipasavyo majukumu yake, ikiwezekana tutapitia upya Katiba na Kanuni zetu ili kukidhi mazingira ya sasa na kuweza kuwatumikia wananchi ipasavyo. Sisi wanaCCM ndiyo tumepewa dhamana na Watanzania kuongoza nchi yetu hivyo tunao wajibu wa msingi wa kuisimamia vizuri Serikali ili itatekeleza majukumu yake ipasavyo. Tutahakikisha pia tunakuwa na safu bora ya uongozi katika ngazi zote kuanzia Shina hadi Taifa. Tutaangalia muundo (structure) wa Chama chetu katika ngazi mbalimbali na kuondoa vyeo visivyokuwa na tija katika Chama na hasa wakati huu wa mfumo wa vyama vingi. WanaCCM ni lazima tujiulize je ni kweli katika zama hizi bado tunahitaji mtoto wa miaka 8 hadi 15 kuwa chipukizi kwa ajili ya kumtumia kwenye siasa badala ya kumwacha asome? Kama akiwepo chipukizi wa CCM, chipukizi wa NCCR au Chadema ama TLP tutakuwa tunajenga nchi ya namna gani? Je bado kuna umuhimu wa kuwa na Makamanda wa Vijana ambao mara nyingi wenye kupewa vyeo hivyo ni wale wenye uwezo wa kifedha pekee? Je walezi kwenye Umoja wa Wanawake (UWT) bado wanahitajika? Je Washauri ndani ya Jumuiya ya Wazazi wanahitajika? Hii ni mifano tu. Tujiulize vyeo hivi vinawasaidiaje wananchi wa kawaida vijijini katika kutatua kero za ukosefu wa maji, barabara, madawati, huduma za afya n.k. Je si kweli vyeo hivi badala ya kutatua migogoro ya wananchi vimekuwa vyanzo vya migogoro ndani ya Chama hasa nyakati chaguzi zinapokaribia? Ni vyema basi wanaCCM tukatafakari na kujipima upya. Ni vyema sisi tuwe mfano wa kuongoza mabadiliko katika nchi yetu. Tutaziimarisha Jumuiya zetu za Chama yaani Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), na Jumuiya ya Wazazi kwa nguvu zote. Tutahakikisha tunakuwa na watendaji wenye sifa zinazohitajika sasa, wachapakazi na waadilifu. Nafahamu ili watendaji wafanye kazi vizuri wanahitaji maslahi bora na mazingira mazuri ya kufanya kazi. Nataka niwahakikishie kuwa tutafanya hivyo. Sitapenda kuona watendaji wetu wanakuwa ombaomba. Kwa bahati nzuri, Chama chetu kina rasilimali nyingi. Tutahakikisha rasilimali hizo zinatumika kwa manufaa ya Chama. Na hapa napenda kusema kuwa tutaunda kikosi kazi maalum kwa ajili ya kutambua na kuhakiki mali zote za Chama, tujue zinatumikaje, kina nani wanazitumia na mapato yanayoingia kwenye Chama ni kiasi gani. Hivyo, nitoe wito kwa Katibu Mkuu (CCM) nitakayemteua, Makatibu wote wa Mikoa, Wilaya, Kata hadi vijiji pamoja na viongozi wote wa Jumuiya za Chama kuorodhesha mali za Chama katika maeneo yao. Aidha, tutawahimiza wanachama wetu kulipa ada zao za kila mwaka tena kwa njia ya kieletroniki. Nina imani, tukiwa na safu bora ya uongozi, watendaji wa chama wachapakazi na waadilifu pamoja na rasilimali za kutosha, Chama chetu kitaweza kutekeleza majukumu yake vizuri, ikiwa ni pamoja na kuisimamia vyema Serikali.
Pili, Kuongeza idadi ya wanachama, wapenzi na mashabiki. Siasa ni mchezo wa idadi (Politics is a game of numbers). Nawapongeza Wenyeviti wa CCM wastaafu kwa jitihada kubwa mlizozifanya ya kuongeza wanachama, ambapo hivi sasa idadi yake inakaribia kuwa milioni 8.7. Chini ya uongozi wangu pia tutajitahidi kuongeza idadi ya wanachama, wapenzi na mashabiki. Tunahitaji kuwa na idadi kubwa ya watu kwenye upande wetu kwa ajili ya kuongeza idadi ya wanachama. Tunahitaji watu kwa ajili ya kupiga kura. Lakini kubwa zaidi, tunawahitaji watu kwa ajili ya kushiriki kwenye shughuli mbali za kimaendeleo. Hivyo basi, nitashirikiana nanyi katika kuhakikisha idadi ya wanachama, wapenzi na washabiki wa Chama chetu inaongezeka, hususan kwa kuvutia kundi la vijana. Na njia bora na rahisi ya kuwavuta watu kwenye Chama chetu ni kuhakikisha tunatekeleza ahadi zetu na wakati huo huo sisi viongozi na wanachama tujitahidi kuwa mfano bora wa kuigwa kwenye maeneo yetu, kwa maneno na vitendo vyetu.
Tatu, kuzidisha mapambano dhidi ya Rushwa, Ufisadi na upungufu wa maadili ya uongozi. Rushwa ni adui wa haki. Kwa kutambua hilo, Ibara ya 9 (h) na Ibara 132 (5)c ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania imekataza vitendo vya rushwa. Aidha, Ahadi namba 3 ya Mwanachama wa CCM inasema “Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa”. Vilevile, Kifungu Na. 18 (2) cha Katiba ya CCM inaeleza kuwa “itakuwa mwiko kwa kiongozi kupokea mapato ya kificho, kutoa au kupokea rushwa”.
Licha ya kuwepo kwa makatazo hayo ya kisheria na maadili, tatizo la rushwa bado ni kubwa hapa nchini. Cha kusikitisha zaidi ni kwamba Chama chetu CCM ni miongoni mwa taasisi ambazo tatizo la rushwa ni kubwa. Ni lazima niseme ukweli. Sisi sote ni mashahidi wa jinsi ambavyo tatizo hilo limekuwa likikiathiri Chama chetu na hasa nyakati za chaguzi mbalimbali ndani ya Chama. Mara nyingi fedha imekuwa kigezo cha mtu kupata uongozi. Mimi binafsi nilishuhudia hili wakati wa kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya kuwa Mgombea Urais kupitia Chama chetu mwaka jana. Vitendo vya rushwa vilikithiri sana. Vitendo vya rushwa vimesababisha Chama chetu kupoteza nafasi za Ubunge kwenye baadhi ya majimbo. Waingereza wana msemo usemao “You can’t give what you don’t have” (Huwezi kutoa usichokuwa nacho). Hii maana yake ni kwamba hatuwezi kuondoa tatizo la rushwa nchini kama sisi wenyewe wanaCCM tutakuwa tukiikumbatia rushwa. Hivyo basi, katika kipindi cha uongozi wangu wa Chama nimedhamiria kushirikiana nanyi katika kuhakikisha tunalikomesha tatizo hilo. Mtu yeyote atakayetumia rushwa kutafuta uongozi hataupata kamwe. Kwa bahati nzuri, Chama chetu kinazo Kanuni za Uongozi na Maadili ambazo zinaelekeza hatua za kuchukua kwa wanachama watakaokiuka maadili ya Chama. Mathalan, katika kupambana na rushwa wakati wa chaguzi mbalimbali za Chama, Kifungu Namba 6 (1) cha Kanuni za Uongozi na Maadili Toleo la Mwaka 2012 zinaelekeza kuwa Kiongozi yeyote atakayethibitika kuwa ameshinda uchaguzi kutokana na kitendo chochote cha rushwa atanyang’anywa ushindi alioupata na pia atazuiwa kugombea tena uchaguzi mwingine wowote kwa muda utakaoamuliwa na Halmashauri Kuu ya Taifa. Hivyo basi, kwa kuwa mwakani Chama chetu kitafanya Uchaguzi wa Viongozi wa ngazi mbalimbali, niwaombe wanaCCM wenzangu tuoneshe mfano kwenye uchaguzi huo kwa kujiepusha na vitendo vya rushwa, ikiwemo kutoa na kukusanya michango, misaada na zawadi kinyume cha taratibu za Chama; kununua kadi za wanachama; kuanza kampeni kabla ya muda uliowekwa rasmi, kutoa takrima n.k. Kwa atakayefanya vitendo hivyo, Chama chini ya uongozi wangu hakitamwonea aibu wala huruma. Nitahakikisha tunasimamia Katiba, Kanuni na Maadili ya Chama chetu ukurasa kwa ukurasa; kifungu kwa kifungu na kipengele kwa kipengele lengo likiwa ni kuhakikisha tunaendelea kuaminiwa na Watanzania.
Nne, Kukomesha Usaliti ndani ya Chama. Katika uongozi wangu nitahakikisha kuwa suala la usaliti ndani ya Chama linakomeshwa. Ndani ya Chama chetu pamekuwa na tabia kwa baadhi ya wanaCCM kusaliti Chama, asubuhi anakuwa CCM, usiku yuko Chama kingine. Wasaliti wa namna hii hawatakuwa na nafasi wakati wa uongozi wangu. Kama wapo wenye tabia wenye tabia hii ni vyema wakajirekebisha na kutubu kuanzia leo. La sivyo watupishe na kuondoka hata leo. Ni vyema kuishi na mchawi kuliko kukaa kuwa na msaliti. Tunahitaji kuwa na wanachama waadilifu wanaofuata Katiba, Kanuni na Maadili ya Chama chetu na siyo kuwa na wanachama ndumilakuwili. Hatuwahitaji wanachama ndumilakuwili ndani ya CCM. Hatuhitaji CCM pandikizi na wanaCCM maslahi ambao wapo CCM kwa sababu wanamwabudu mtu fulani kwa maslahi yao binafsi. Ninahitaji wanaCCM ambao siku zote, usiku na mchana; mvua na jua; njaa na shibe watabaki CCM bila kuyumba. Hiyo ndiyo CCM ya waasisi wetu Mwalimu Nyerere na Mzee Karume ninayoijua mimi.
Mimi ninaamini kama tukishirikiana katika kutekeleza mambo yote haya na mengineyo ambayo sikuyataja, Chama chetu kitaimarika na Watanzania wataendelea kutuunga mkono na kutuamini. Binafsi nataka kuona CCM inakuwa ya watu hasa wanyonge na si CCM ya viongozi pekee. Nataka CCM inayoaminika na si CCM inayodharaulika. Nataka CCM ya kufanya kazi na si CCM ya kuomba omba. Na pia nataka CCM inayojitegemea na si CCM inayotegemea wafadhili. Na kwa kuwa ninyi Wajumbe wa Mkutano Mkuu (chombo cha juu kabisa cha uamuzi katika Chama) mmenipa kazi hii, ninakwenda kufanya haya yote kwa niaba yenu.
Ndugu Viongozi na Ndugu WanaCCM wenzangu;
Wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana tulinadi Ilani yetu ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020. Kwenye Ilani yetu tualiahidi mambo mengi. Tuliwaahidi Watanzania kuwa tutadumisha Muungano, amani na mshikamano wa nchi yetu. Tuliwaahidi kuboresha maisha yao. Tuliahidi kuboresha huduma za jamii, hususan afya, elimu na maji. Tuliwaahidi kujenga uchumi wa viwanda ili kukabiliana na tatizo la umaskini na ukosefu wa ajira. Tuliwahidi kuwaondolea kero mbalimbali ikiwemo rushwa, uonevu na dhuluma. Tuliwaahidi kuwa tutasimamia vizuri rasilimali za nchi. Tuliwaahidi kuimarisha miundombinu, hususan ya barabara, reli, bandari, nishati, usafiri wa anga, usafiri wa meli n.k. Watanzania walituamini na wakatupa tena ridhaa ya kuongoza nchi. Ndugu zangu wanaCCM ahadi ni deni. Ni lazima tutekeleze yale yote tuliyowaahidi kwenye Ilani yetu ya uchaguzi ili tuweze kujihakikishia tena ushindi kwenye Uchaguzi wa Mwaka 2020. Rais Mstaafu Mzee Mkapa alipata kusema “Mwisho wa Uchaguzi mmoja ndio mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi mwingine”. Hivyo, ni lazima tujiandae.
Tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani mpaka sasa imepita takriban miezi nane. Nafarijika kuwa katika kipindi hicho, tayari tumeanza kutekeleza baadhi ya mambo ambayo tumewaahidi Watanzania. Mambo hayo ni pamoja na utoaji wa elimu bure ambapo kila mwezi tunatenga bilioni 18.77. Hii imewezesha kuongeza wanafunzi waliojiandikisha darasa la kwanza kufikia milioni 1.9 mwaka 2016 kutoka milioni 1.02 mwaka 2015. Tumenunua ndege mpya mbili kutoka nchini Canada na zinatarajiwa kuwasili nchini mwezi Sepemba 2016. Tumeingia makubaliano na Serikali ya Uganda kujenga Bomba la Kusafirisha mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga lenye urefu wa takriban kilometa 1,400 na linatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 20,000 wakati wa ujenzi. Tumetangaza zabuni ili kuanza ujenzi wa reli mpya ya kisasa ya kiwango cha kimataifa (standard gauge) kutoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Mwanza na Kigoma na baadaye kuunganika na nchi za Rwanda na Burundi, ambapo katika bajeti ya mwaka huu (2016/2017) tumetenga Shilingi trilioni 1 kuanza ujenzi. Tumeongeza fedha za bajeti ya maendeleo kutoka asilimia 26 mwaka wa fedha 2015/2016 hadi asilimia 40 katika mwaka huu wa fedha (2016/2017). Tumeimarisha nidhamu ya watumishi wa umma, tumewaondoa watumishi hewa takriban 12,500 na bado tunaendelea kuwaondoa. Tumedhibiti matumizi ya Serikali na kuongeza ukusanyaji wa mapato hadi kufikia wastani wa shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi. Licha ya hatua hizo tulizozichukua, ni dhahiri kuwa bado tuna safari ndefu katika kutimiza yale tuliyowaahidi Watanzania. Hivyo basi, napenda kutumia hadhara hii kuwaomba wanaCCM wenzangu kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kuhakikisha ahadi zote tulizowaahidi wananchi wakati wa kipindi cha kampeni zinatekelezwa.
Mojawapo ya njia ya kuhakikisha ahadi zetu zinatekelezwa ni kwa sisi wanaCCM kujitahidi kufahamu mipango na mikakati mbalimbali ya Serikali. Mathalan, hivi karibuni tumepitisha Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano utakaotekelezwa kuanzia Mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021. Mpango huu umejumuisha masuala yote tuliyoahidi kwenye Ilani yetu na umeainisha maeneo ya kipaumbele ya Serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo. Utekelezaji wa Mpango huu wa Maendeleo umeanza mwaka huu wa fedha ambapo Serikali imepanga kutumia kiasi cha Shilingi trilioni 29.5. Katika fedha hizo, asilimia 40 tumezielekeza kwenye shughuli za maendeleo, ikiwemo kujenga miundombinu wezeshi ya uchumi (miundombinu ya usafiri na nishati), kuboresha huduma za jamii, kama vile afya, elimu na maji n.k.
Naamini kama tutaifahamu na kuilewa vizuri mipango ya Serikali itakuwa rahisi kwetu kuwahamasisha wananchi wetu kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za maendeleo, kama vile kilimo na ujenzi wa viwanda. Tutaweza pia kuwahamasisha kulipa kodi kwa ajili ya kugharamia mambo mbalimbali ya maendeleo ambayo Serikali imepanga kutekeleza. Bila kulipa kodi itatuwia vigumu kutekeleza ahadi tulizowaahidi wananchi. Aidha, kama tunaifahamu vizuri mipango ya Serikali tutaweza kufuatilia kwa karibu utekelezaji wake kwenye maeneo yetu, hususan kwenye halmashauri ambako fedha nyingi za Serikali zinaelekezwa. Hivyo basi, niombe kila mmoja wetu awe mtekelezaji wa kwanza wa Ilani ya Uchaguzi 2015 kwa kufanya kazi na pia kuwahamasisha Watanzania katika shughuli za maendeleo.
Ndugu Mwenyekiti Mstaafu;
Ndugu WanaCCM;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Leo tupo Dodoma kushiriki kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa CCM. Napenda kutumia mkutano huu kueleza masuala mengine mawili ya ziada. Jambo la kwanza. Hapa Dodoma ndio Makao Makuu ya Chama chetu pamoja na Serikali. Dodoma pia ni mji uliopo katikati ya nchi yetu. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekuwa likifanya vikao vyake hapa. Hata Chuo Kikuu kikubwa zaidi nchini kipo hapa Dodoma. Aidha, nimeamua maadhimisho ya Sherehe za Mashujaa mwaka huu yafanyike hapa Dodoma.
Hivyo basi, kwa kutambua umuhimu wa Dodoma na pia katika kutekeleza ndoto ya Baba wa Taifa letu, Hayati Mwalimu Nyerere ya kuhamishia Makao Makuu ya Serikali hapa Dodoma, napenda kutamka mbele ya Mkutano huu kuwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wangu, nitahakikisha kuwa Serikali inahamia hapa Dodoma. Nitoe wito kwa Mawaziri na watendaji wengine wa Serikali kujipanga kuhamia Dodoma. Hapa Dodoma kuna miundombinu ya kutosha hivyo naamini hapatokea visingizizio vya aina yoyote.
Jambo la pili ambalo napenda kulieleza ni kwamba leo hii nimepokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chama chetu, Mzee Kinana. Barua hiyo imeeleza azma ya Mzee Kinana pamoja na wajumbe wote wa Sekretarieti ya sasa kutaka kujiuzulu ili kunipa nafasi ya kuunda Sekretarieti mpya. Baada ya kutafakari kwa kina maudhui ya barua hiyo na kuangalia majukumu makubwa yaliyopo mbele yetu, nimeamua kuwa Sekretarieti ya sasa chini ya Mzee Kinana iendelee. Kama kutakuwa na haja ya kufanya mabadiliko, nitaitisha Kikao cha Halmashauri Kuu kujadili suala hilo. Kwa sababu hiyo, kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichopangwa kufanyika kesho kujadili suala hili hakitafanyika.
Ndugu Mwenyekiti Mstaafu;
Ndugu Viongozi;
Ndugu Wajumbe wa Mkutano Mkuu Taifa;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nafasi niliyopewa leo ni ya kutoa shukrani. Nafahamu tutapata fursa nyingine ya kuzungumza nanyi kwenye vikao na mikutano yetu kwa ajili ya kupeana mipango na mikakati mbalimbali ya kuimarisha Chama chetu na kuleta maendeleo kwa nchi yetu. Kwa sababu hiyo ningependa kuishia hapa. Hata hivyo, nitakuwa ni mnyimi wa fadhila kama nitahitimisha hotuba yangu bila kuwashukuru wageni wetu. Kwanza kabisa nawashukuru wawakilishi wa vyama vya siasa vya hapa nchini mliopo. Mmeonesha ukomavu mkubwa wa kisiasa. Siasa siyo uadui. Sisi sote ni Watanzania hivyo hatuna budi kudumisha umoja na mshikamano wa nchi yetu. Tuweke kando tofauti zetu za kisiasa na tushirikiane kwa pamoja kujenga nchi yetu. Maendeleo hayana vyama.
Nawashukuru pia wawakilishi wa vyama rafiki kutoka nje pamoja na Mabalozi mnaowakilisha nchi na taasisi mbalimbali za kimataifa mliopo hapa. Nawashukuru sana kwa kuja kujumuika nasi kwenye tukio hili la kihistoria. Napenda kuwahakikishia kuwa Chama cha Mapinduzi chini ya uongozi wangu, kitaendelea kushirikiana nanyi katika ngazi ya Chama na Serikali.
Aidha, napenda kuwashukuru watumishi wote wa Sekretarieti ya Chama chini ya kiongozi imara, mahiri na shupavu, Mzee Kinana, kwa kufanikisha mkutano huu. Mzee Kinana wewe kweli ni kiongozi. Sote tunafahamu kazi kubwa na nzuri iliyofanywa na Mzee Kinana tangu alipopewa nafasi ya Ukatibu Mkuu. Mara hii tena ameingoza Sekretarieti na kufanikisha Mkutano Mkuu huu Maalum. Nawashukuru pia Manaibu Makatibu Wakuu wa Bara na Zanzibar. Aidha, nazishukuru Kamati mbalimbali zilizoratibu maandalizi ya mkutano huu. Mmefanya kazi kubwa na nzuri.
Kwa namna ya pekee kabisa navishukuru vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kuhakikisha Mkutano huu unafanyika katika mazingira ya amani na usalama. Vilevile, nawashukuru ndugu zetu waandishi wa habari kwa kazi kubwa mliyoifanya ya kuripoti Mkutano wetu. Katibu Mkuu alipokuwa akitoa taarifa jana wakati wa Mkutano wa Halmashauri Kuu alisema waandishi wa habari walioomba kuripoti Mkutano huu ni 200 lakini nimeambiwa walijitokeza ni takriban 400. Hii inadhihirisha ukongwe na ukubwa wa Chama Cha Mapinduzi.
Halikadhalika, nawashukuru watoa huduma mbalimbali wa kwenye mkutano huu wahudumu, madereva pamoja na wenyeji wetu, wana-Dodoma kwa ukarimu wenu mkubwa mliotuonesha katika kipindi chote cha mkutano. Ahsanteni sana. Ninawashukuru pia Watanzania wote wakiwemo viongozi wa dini mbalimbali kwa kuendelea kuniombea mimi na taifa kwa ujumla. Navishukuru vikundi vya burudani vikiongozwa na Kikundi chetu cha Tanzania One Theatre (TOT) kwa kutuburudisha kwa nyimbo zenu maridadi.
Napenda kuhitimisha hotuba yangu kwa kurudia tena kutoa shukrani zangu nyingi kwa wanaCCM wenzangu kwa kunipa heshima kubwa ya kunichagua kwa kura nyingi kuwa Mwenyekiti wenu. Ombi langu kwenu, tuzidi kushirikiana katika kuimarisha Chama chetu ili Watanzania waendelee kutuamini. Uchaguzi uliopita umetudhihirishia kuwa penye umoja ushindi ni lazima. Hivyo, tuendeleze umoja wetu na tujiepushe kumtegemea mtu au kikundi cha watu wachache katika kufanya mambo yetu. Kila mara tukumbuke usemi wa Mwenyekiti wetu mstaafu, Mzee Kikwete, usemao: Chama kwanza, Mtu baadaye“. Chama chetu ni kikubwa. Tuna hazina kubwa ya viongozi wastaafu. Hivyo, tuendelee kushirikiana katika kuwatumikia Watanzania ili waendelee kutuamini.
Baada ya kusema hayo, namshukuru tena Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kumaliza Mkutano wetu salama na nawatakia kila mmoja wetu safari njema wakati tutakapokuwa tukirejea majumbani kwetu.
Mungu Kibariki Chama cha Mapinduzi
Mungu Ibariki Tanzania
Kidumu Chama Cha Mapinduzi“
“HAPA KAZI TU“
Ahsanteni kwa kunisikiliza“