Mawakili
wa utetezi katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara tajiri wa madini ya
tanzanite ‘Bilionea’ Erasto Msuya (43), jana walitumia saa nne na nusu
kuwasilisha hoja tisa za majumuisho kwa lengo la kuonyesha mahakama kuwa
wateja wao hawana hatia.
Hoja
hizo zilizowasilishwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi chini ya Jaji
Salma Maghimbi anayesikiliza shauri hilo namba 12 la mwaka 2014,
zilijikita zaidi kuhoji utaratibu mzima wa ukamataji washtakiwa.
Jaji
Maghimbi alianza kusikiliza hoja za upande wa utetezi jana saa 4:08
asubuhi hadi saa 7:32 mchana alipoahirisha kwa muda usikilizaji wake
hadi saa 7:45.
Washtakiwa
walioonekana wana kesi ya kujibu ni mshtakiwa wa kwanza Sharif Athuman
(35), ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mchimbaji mdogo, mkazi wa
Kimandolu mkoani Arusha, mshtakiwa wa pili Shaibu Saidi maarufu kama
Mredii (42), mkazi wa Songambele, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara na
mshtakiwa wa tatu Mussa Mangu (34), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu.
Wengine
ni mshtakiwa wa tano Kihundwa, mkazi wa Lawate, Wilaya ya Siha,
mshtakiwa wa sita Sadiki Jabir a.k.a Msudani (36), mkazi wa Dar es
Salaam na Lang’ata, Wilaya ya Hai, na mshtakiwa wa saba Alli Musa
maarufu Majeshi, mkazi wa Babati, mkoani Manyara.
Aliyekuwa
mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo iliyobaki na washtakiwa sita, Jalila
Said (32) mkazi wa Babati aliachiwa huru Mei 14 baada ya Jaji Maghimbi
kuona ushahidi uliotolewa dhidi yake haumgusi kiasi cha kufanya awe na
kesi ya kujibu.
Msuya,
aliuawa kwa kupigwa risasi 22, Agosti 7, 2013, majira ya saa 6:30
mchana katika eneo la Mijohoroni, kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi,
karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Mawasilisho
ya uchambuzi wa hoja hizo yaliyofanywa na Wakili Majura Magafu katika
waraka wenye kurasa 34, ulijikita zaidi kwenye uchambuzi wa mkanganyiko
wa tarehe halisi za ukamataji wa watuhumiwa, utata wa tarehe za
kupatikana vielelezo muhimu vya ushahidi kama bunduki aina ya SMG,
pikipiki mbili zinazodaiwa kutumiwa na wauaji, maelezo yanayodaiwa ni ya
kukiri kosa na ripoti ya DNA.
Hoja
nyingine ni mateso ya washtakiwa, umiliki wa namba ya simu
iliyosajiliwa kwa jina la Motii Mongululu inayodaiwa kutumika kumvuta
marehemu kwenda eneo la tukio na kama ushahidi uliotolewa na mashahidi
wa upande wa mashtaka ni ushahidi wa moja kwa moja au ni wa ushahidi wa
kimazingira.
Akichambua
hoja hizo, Wakili Magafu alidai hakuna ubishi kwamba Msuya alikufa kifo
ambacho si cha kawaida cha kupigwa risasi na kuvuja damu nyingi, lakini
pia hakuna ubishi kwamba shahidi pekee aliyeshuhudia mauaji hayo ni
kijana wa miaka 19, Noel Thomas, mkazi wa Kijiji cha Ormelili, Wilaya ya
Siha aliyekuwa akichunga mifugo lakini hakuweza kumtambua aliyefyatua
risasi kumuua.
“Mheshimiwa
Jaji (Maghimbi), kumekuwa na utata kuhusu ukamataji wa watuhumiwa,
washtakiwa waliopo mbele yako wanasema tarehe zilizotajwa katika maelezo
yao sizo tarehe walizokamatwa," alidai wakili Magafu na kueleza zaidi:
"Swali
la kujiuliza ni hili je, hiyo caution statement (maelezo ya onyo)
iliyokuwa admitted (pokelewa) hapa mahakamani na kusajiliwa kama Exhibit
P.II (kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka namba II) kina sifa
ya kuitwa confession statement (maelezo ya kukiri kosa)?
"Ni
lazima confession statement iweze kukutia kwanza wewe hatiani na vile
vile tunasema haiwezi kutumika kuwatia wenzako hatiani. Hakuna ushahidi
uliotolewa hapa mahakamani ukionyesha Musa Mangu alihusika kununua na
kuchonga laini za simu zilizotumika katika mauaji hayo zaidi ya maelezo
ya wapelelezi.
"Mtu pekee ambaye angeweza kuisaidia mahakama na hakuletwa mahakamani kutoa ushahidi wake ni Adam Leyani.”
Wakili
Magafu aliendelea kudai kwamba mshtakiwa wa kwanza, Mussa Mangu
anadaiwa alikamatwa kati ya Agosti 11 na 13, 2013 na mkanganyiko huo
umeletwa na shahidi wa 27 wa upande wa Jamhuri ambaye anakinzana na
shahidi wa 18 na wote ni maofisa wa polisi.
Aidha,
aliendelea kudai kuwa katika ukamataji wa bunduki upande wa mashtaka
umedai kuwa ilikamatwa Septemba 11, 2013 lakini ushahidi huo huo
unaonyesha kwamba watuhumiwa walikamatwa Septemba 13, 2013.
“Swali
tunalojiuliza na ambalo mahakama inapaswa ilizingatie ni kwamba ni nani
kati ya washtakiwa waliopo mbele ya mahakama alitumia bunduki hiyo
(SMG) kumfyatulia risasi marehemu Msuya? Ushahidi huo haupo," alidai
Wakili Magafu.
"We
submit the gun was planted by the police (tunasema bunduki ilibambikwa
na polisi) kwa sababu ilipatikana kabla ya watuhumiwa kukamatwa.
Kukosekana kwa chronological events (mtiririko wa matukio) kunaacha
utata.”
Aidha,
wakili huyo aliyekuwa akiwasilisha hoja hizo kwa niaba ya wenzake
watatu alidai kwamba hakuna ushahidi wa kuonyesha kwamba miongoni mwa
watuhumiwa hao alikuwapo anayemiliki pikipiki aina ya King Lion na
kutumia SMG hiyo kumuua Bilionea Msuya na kwamba ni jukumu la upande wa
mashtaka kuthibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka.
Wakili
Magafu aliendelea kudai kuwa kwa mshtakiwa wa pili Athuman ushahidi wa
Jamhuri una mkanganyiko kwa vile shahidi wa 27, Mkaguzi wa Polisi Damian
Chilumba alidai alikamatwa Agosti 12, 2013 lakini shahidi wa tisa,
Mkaguzi wa Polisi Samuel Maimu akaieleza mahakama kwamba alikamatwa
Agosti 13 mwaka huo.
Zaidi
aliendelea kudai kwamba kwa 'Mredii’ ushahidi wa shahidi wa upande wa
mashtaka alidai mahakamani hapo kwamba Mredii alikamatwa Agosti 16,2013
lakini shahidi wa utetezi ambaye ni yeye Mredii alidai kwamba
hakukamatwa na polisi isipokuwa aliitwa kwa wito na Mkuu wa Kituo cha
Polisi Mirerani na alitii na kwenda siku ya Agosti 17, 2013.
Kuhusu
ushahidi wa uchunguzi wa DNA, Wakili Magafu alidai kwamba ushahidi wa
shahidi wa 25 wa upande wa mashtaka, Gloria Omari (55) aliyekuwa
akifanya kazi za kemia na utafiti kwenye Maabara ya Idara ya Sayansi ya
Jinai ya Vinasaba katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali mwaka 2013,
ushahidi wake hauungi mkono ushahidi wa shahidi wa 26, Kaijunga Brassy
(35) ambaye alikuwa Mkemia kutoka Makao Makuu ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa
Serikali, Kanda ya Kaskazini.
Wakati
anahitimisha uwasilisha hoja hizo, Wakili Magafu aliieleza mahakama
hiyo kwamba hakuna ushahidi wa moja kwa moja katika kesi hiyo na kwamba
mahakama imebaki na ushahidi mmoja ambao ni wa kimazingira.
"Mheshimiwa
Jaji na waungwana wazee wa mahakama ili ushahidi wa circumstantial
uweze kutumika ni matakwa ya sheria kwamba mnyororo wa ushahidi haupaswi
kukatika," alidai.
"Ushahidi
wa prosecution (Jamhuri) unakatika mno na ushahidi huo wa kimazingira
wanaojaribu kuuleta mnyororo wake umekatika. Mahakama inastahili iwaone
washtakiwa hawana hatia, prosecution wameshindwa kuthibitisha kesi yao
na washtakiwa waachiwe huru."
Upande
wa mashtaka katika kesi hiyo ambayo ni gumzo katika mikoa ya Kanda ya
Kaskazini, unaongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Abdala Chavula,
akisaidiwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Omari Kibwana na Wakili wa
Serikali, Kassim Nassir.
Mawakili
wanaounda jopo la utetezi katika kesi hiyo ni Hudson Ndusyepo
anayemtetea mshtakiwa wa kwanza, Magafu anayemtetea mshtakiwa wa pili na
wa tano, Emmanuel Safari anayemtetea mshtakiwa wa tatu na John Lundu
anayemtetea mshtakiwa wa nne, sita na saba.
0 comments:
Chapisha Maoni