Serikali
imekamata mali za wafanyabiashara Harbinder Singh Sethi na mwenzake
James Rugemalira wanaohusishwa na uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300
katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Mali
hizo zimekamatwa siku chache baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa Tanzania (Takukuru) kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani.
Kwa
mujibu wa gazeti la MTANZANIA Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo
Mganga hakuweza kupatikana kutoa ufafanuzi wa kina wa hatua ya ofisi
yake kushikilia mali za Sethi na Rugemalira.
Ofisi
ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), iliiambia MTANZANIA jana kuwa Serikali
imelazimika kukamata mali zote za wafanyabiashara hao kama hatua ya
kuzuia kuuzwa au kuhamishwa umiliki wake wakati wakiendelea kusota
rumande.
“Ni
jambo la kawaida katika kesi kama hii, huwezi kuacha mali ambazo ndizo
kielelezo katika suala hili. Hivyo hatua ya kwanza ni kumkamata
mshtakiwa na kisha ni lazima udhibiti mali zake kwani ndiyo kielelezo
muhimu kinachobishaniwa katika kesi husika.
“Unaweza
ukaiacha mali halafu mshtakiwa huku akiwa yupo ndani bado akaendelea
kutoa maelezo na mali kuhamishwa umiliki wake au hata kuuzwa, kwa hali
hiyo ndiyo hulazimika kushikilia mali hizo,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake .
Ofisi
ya DPP inaelezwa imezuia mali zote za Sethi na Rugemalira kwa kuziweka
chini ya ulinzi mkali pamoja na kufunga kwa muda akaunti zao za benki.
Sethi
ambaye ni Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Independent Power Tanzania
Limited (IPTL)/Pan Africa Power (PAP) na Rugemalira wa Kampuni ya VIP
Engineering and Marketing Ltd, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Juni 19.
Watuhumiwa hawa tayari wamesomewa mashtaka sita, yakiwamo ya uhujumu uchumi.
Mbali
na hayo imeelezwa kuwa orodha ya waliopata mgawo wa fedha hizo za
Escrow imezidi kuongezeka, wakiwamo vigogo kutoka wizara nyeti, taasisi,
viongozi wa dini na mashirika yasiyo ya kiserikali na tayari baadhi yao
wameanza kuhojiwa na Takukuru mapema wiki hii.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa idadi ya waliohojiwa imefika zaidi ya watu 30 hadi sasa.
Miongoni
mwa wanaotajwa kuhojiwa na Takukuru wamo baadhi ya mawaziri wa Serikali
ya Awamu ya Nne na mtoto wa kigogo wa Serikali, ambao inaelezwa kuwa
huenda wakafikishwa mahakamani Jumatatu, huku wengine wakiendelea
kuhojiwa zaidi.
0 comments:
Chapisha Maoni