Rais
Mstaafu Ali Hassan Mwinyi amesema kama si matakwa ya Katiba ya nchi,
uongozi wa Rais John Magufuli ulipaswa kuendelea kuwapo miaka yote.
Alisema
laiti ingelikuwa Katiba iliyopo haikufupisha muda wa uongozi wa rais,
angeshauri Rais Dk Magufuli awe Rais wa Tanzania wa siku zote.
Alikuwa akizungumza katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Dar es Salaam jana, alipokuwa akitoa salamu za Eid El Fitri.
Mzee Mwinyi alisema mambo anayoyafanya Rais Dk Magufuli ni mazuri na yanalipeleka Taifa mbele.
Hii ni mara ya pili kwa kiongozi huyo kutamka hadharani namna anavyokunwa na utawala wa sasa wa Rais Magufuli.
Mwinyi
alisema Magufuli ameweza kufanya mambo mengi mazuri kwa kipindi
kifupi kuliko yaliyowahi kufanywa na watangulizi wake akiwamo yeye
(Mwinyi).
Katika
kauli yake ya jana, Mzee Mwinyi alisema Rais Magufuli amefanikiwa
kulipeleka Taifa mahali pazuri na amerejesha nidhamu katika maeneo
mbalimbali ya kazi nchini.
“Nchi imetulia, leo mnakwenda madukani, hospitali, ofisini unapata huduma nzuri.
“Hayo
ndiyo tuliyoyataka, kupata Serikali itakayokuwa na watumishi ambao
watawatumikia watu na hivyo ndivyo inavyofanyika sasa kwa sababu
tumempata kiongozi tuliyenaye leo (Rais Magufuli),” alisema na kuongeza:
“Huyu
kiongozi ni wa kumuenzi sana, ni wa kumsaidia sana, ni wa kumsifu sana…
si kumsifu kwa uongo, uongo, ni kumsifu kwa kazi nzuri anayoifanya si
kwa manufaa yake bali kwa manufaa ya Watanzania wote pamoja na mimi
niliyesimama hapa.
“Raia
anataka nini tena baada ya haya? Analindwa, anashughulikiwa,
anayoyataka raia ndiyo anayoyataka Rais wetu… lakini kwa kuwa tuna
Katiba basi twende na Katiba yetu.
“Husia
wangu kwenu Watanzania wote, tumtii na kumsaidia Rais wetu ili mambo
yaende vizuri kama yalivyo sasa. Wazee wanasema hivi. ‘kidole kimoja
hakivunji chawa’. Tumsaidie ili mambo yaende hivi kama yanavyokwenda”.
Akizungumzia
alipokutana na Rais Dk. Magufuli Ikulu baada ya mwaka mmoja wa uongozi
wake, alisema yako baadhi ya maeneo ambayo aliyafanya kwa mafanikio
makubwa ikilinganishwa na wakati uliopita.
Aliyataja
baadhi ya maeneo hayo kuwa ni mapambano dhidi ya rushwa akisema hatua
zilizochukuliwa katika mwaka mmoja zimedhihirisha kasi kubwa ya
kukabiliana na tatizo hilo ikilinganishwa na wakati uliopita.
“Rushwa
ilikuwapo tangu enzi ya Hayati Mwalimu Nyerere … aliipondaponda kabisa
lakini hakuimaliza, na sote tuliosalia ni hivyo hivyo, kila mmoja
amefanya kwa kiasi chake, lakini Rais Magufuli kwa mwaka mmoja ameleta
‘surnami’, nafurahi sana,” alisema Alhaji Mwinyi.
Eneo jingine ni kuimarisha utendaji kazi Serikalini akisema hatua zilizochukuliwa na Serikali ya sasa zimeongeza kasi.
Aliwataka viongozi na wananchi kuunga mkono juhudi hizo.
“Tuliobaki tumsaidie, tumsaidie kwa kumuombea dua, tumsaidie kurekebisha kwa kusema ukweli pale ambako watu wanapotosha.
“Tusiwaache
watu wakapata nafasi ya kuongea uongo, kila mtu anaweza kuwa anasema
kutokana na nia yake na lengo lake, lakini hakuna asiyejua kuwa kazi
aliyoifanya mwenzetu ni nzuri nzuri, nzuri ya ajabu,” alisisitiza.
0 comments:
Chapisha Maoni