Sakata
la madalali kuendelea kukusanya kodi za Halmashauri ya Jiji la Arusha
kutoka kwa wapangaji wa vibanda vinavyomilikiwa na jiji hilo, limezidi
kuchukua sura mpya huku, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
(Chadema), akimwomba Rais Dk. John Magufuli kuunda tume ya uchunguzi au
avunje halmashauri.
Kauli
ya mbunge huyo imekuja baada ya hivi karibuni kikao cha Baraza la
Madiwani katika Jiji la Arusha kupitisha azimio la kodi za vibanda
vilivyojengwa stendi ndogo mjini Arusha kutakiwa kulipia halmashauri
moja kwa moja na si kupitia madalali.
Jana
Lema alisema kwa muda mrefu kumekuwa na hali ya kutoheshimiwa kwa
maazimio yanayotolewa na Baraza la Madiwani jambo ambalo halileti picha
nzuri kwa jamii.
Alisema
jiji liliingia mkataba wa miaka 10 na waliojenga vibanda hivyo tangu
mwaka 1994 na baada ya hapo vitarudi chini ya umiliki wa halmashauri ya
jiji lakini tangu wakati huo hadi sasa kumekuwa na kutoelewana na
Serikali imekuwa ikikosa mapato yake.
“Tunajua
huenda ni mkakati maalumu unaofanywa na Mkurugenzi wa Jiji (Athuman
Kihamia) kupitia Mkuu wa Mkoa wa Arusha (Mrisho Gambo).
“Ni
wazi huu ni mkakati wa kudhoofisha halmashauri ambazo zipo chini ya
upinzani hasa Chadema ili zionekane zimeshindwa kusimamia rasilimali
ikiwemo ukusanyaji wa mapato.
“Kutokana
na hali hii ninamwomba sana Rais Dk. John Magufuli, kama aliweza kuunda
tume na ikachunguza suala la mchanga wa dhahabu na akawafukuza kina
Acacia basi afanye hivyo na kwa jiji la Arusha na kama itaonekana
vinginevyo avunje Baraza la Madiwani nasi tutarudi mtaani na kuwa
madiwania wa wananchi kuliko kutoheshimiwa maamuzi ya vikao.
“Mtu
amejenga kibanda miguu mitatu kwa mitano tangu mwaka 1994 anakusanya
kodi je hadi leo hajarudisha fedha zake? Kuna nini kinachoendelea na
kwanini madiwani wanadharauliwa? Nakuombas Rais Magufuli tupia jicho
lako Arusha,” alisema Lema
Mbunge
huyo alikwenda mbali na kudai kwamba wapo baadhi ya viongozi wa
Serikali wamekuwa wakiandaa mikakati kwa kushirikiana na viongozi wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) yenye lengo la kudhofisha maeneo yanaongozwa
na wapinzani.
“Tunaona
wazi huu huenda ni mkakati wa kudhofisha upinzani kwani hata kauli ya
CCM kupitia kwa Katibu Mwenezi wake, Humphrey Polepole kwamba viongozi
wa Serikali kupelekwa kwenye maeneo ya upinzani. Kauli hii aliitoa akiwa
Arusha na kilio chetu hiki tumekifikisha hadi kwa Waziri wa Tamisemi,
George Simbachawene naye anajua kila kitu,” alisema
Alisema
suala la malipo hayo awali wafanyabiashara walikubaliana na uamuzi wa
jiji lakini baada ya kuteuliwa kwa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Arusha
ambaye kwa sasa ni mkuu wa mkoa, Mrisho Gambo aliingia suala hilo na
kumpa maagizo kwa kuwakingia kifua watu waliojenga vibanda hivyo.
0 comments:
Chapisha Maoni