test

Ijumaa, 26 Mei 2017

Watu 4 wafariki kwa kufukiwa na kifusi Geita


Watu wanne wamepoteza maisha na wengine watatu kujeruhiwa baada ya kufukiwa na kifusi katika machimbo ya Nyamalinde kijiji cha Sobola nje kidogo ya wilaya ya Geita, mkoani Geita.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo amesema tukio hilo limetokea  jana majira ya saa mbili asubuhi katika machimbo hayo yanayomilikiwa na wananchi licha ya kuwa tayari yalishapigwa marufuku kuendelea kwa kazi hiyo.

Mponjoli amesema tukio hilo limetokea baada ya watu 7 kuingia ndani ya mgodi huo, lakini muda mfupi baadaye kifusi kikawaangukia na kusababisha vifo vya watu wanne kati yao huku watatu wakitoka salama licha ya kuwa na majeraha.

Amewataja watu waliopoteza maisha kuwa ni pamoja na Robert Kazegemwa, Jeremia Emmanuel, Makenya Mwita na Julius Timotheo.

Waliojeruhiwa ni pamoja na Mashaka Samuel, Justine Safari na Maneno Lusika ambao wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Katoro.

Katika tukio lingine, jana majira ya saa 7 mchana tetemeko dogo la ardhi limetikisa katika mkoa wa Geita ambapo licha ya kutokuwa na madhara yoyote, limezua taharuki katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika shule ya sekondari Nyang'wale.

Kamanda Mponjoli amesema katika shule hiyo, wanafunzi walikuwa katika mitihani na ndipo walipokimbia kutoka darasani ili kujiokoa ambapo kutokana na msukumano, mwanafunzi mmoja alijeruhiwa lakini tayari amekwishapatiwa matibabu na yuko salama

Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi

xxxxxxxxxxxxx

0 comments:

Chapisha Maoni