Chama
cha Mapinduzi (CCM) kimelaani vikali mauaji ya baadhi ya viongozi, raia
na askari polisi, waliouawa kwa kupigwa risasi katika wilaya za Rufiji,
Kibiti na Mkuranga mkoa wa Pwani, na kutoa pole kwa familia zilizoguswa
na mauaji hayo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi na
Uenezi CCM, Humphrey Polepole alisema chama hicho kwa niaba ya
wananchi kinawataka viongozi wenye dhamana na usalama wa wananchi
kujitafakari, huku akisisitiza kuwa ikiwa mauaji hayo yataendelea, chama
hicho kitaielekeza serikali kuwachukulia hatua.
“Sasa
imetosha, yeyote mwenye dhamana ajitafakari.Hatupendi kusema hali hii
ikiendelea watu wawajibike, ingawa kuwajibika kwa sababu ya watu
kupoteza maisha ni ustaarabu wa kiungozi. Viongozi wote na wenye dhamana
mchukue hatua, sitaki tufike pahala niseme, CCM tutaielekeza serikali
kuchukua hatua kwa walio na dhamana kwa kutowajibika katika majukumu
yao,” alisema na kuongeza Polepole.
“Tunaamini
demokrasia ya vyama vingi ni mshikamano tunahisi kama tumeachwa
wenyewe, tumevunjika moyo sana , sielewi mshikamano wa kuweka Tanzania
moja, unakuja wakati wa uchaguzi au kugawana ruzuku? tumesikitishwa,
nimeona wenzangu wametingwa na kufanya siasa za madaraka kuliko siasa za
maendeleo zinazohusu shida za watu wetu.”
Aidha,
Polepole alisema anasikitishwa na ukimya wa vyama vya upinzani kuhusu
mauaji hayo, ambapo ameeleza kipindi hiki vyama vyote pasina kujali
itikadi za kisiasa vingeungana kutetea uhai wa wananchi wa maeneo hayo
ambao ndiyo wapiga kura wao.
Alisema
CCM wangependa kuona vyama vyote kwa sasa vinaungana hasa katika
kipindi hiki ambacho wananchi wana hofu na maisha yao kutokana na mauaji
hayo lakini jambo hilo limekuwa tofauti kwa wapinzani wao kuwa kimya na
kutoonyesha kuumizwa na mauaji hayo.
“Hakuna
namna bora ya kuwahudumia wananchi kama kuwa na mshikamano, wale
wananchi wakienda kwenye kura wanachagua vyama vyote, wale wenzetu
wamekuwa kimya, wametusikitisha, na hata wale walioongea wamecheza
maneno, tusicheze maneno wakati uhai wa wenzetu upo hatarini,
“Sisi
kama Chama cha Mapinduzi tukikaa kimya tutakuwa hatuwatendei haki
watanzania ambao wakati kama huu wanapitia wakati mgumu, ninawaomba
viongozi wote wenye dhamana wachukue hatua,” alisema Polepole.
0 comments:
Chapisha Maoni