Siku moja baada ya kutangazwa kuzuka kwa ugonjwa wa ebola katika nchi ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,
Dk Mpoki Ulisubisya amewatoa hofu Watanzania akisema imechukua tahadhari
kuhakikisha hauingii nchini.
Dk Ulisubisya alisema jana kuwa hadi sasa hakuna taarifa za kuwapo kwa
mgonjwa yeyote wa ebola nchini na uangalizi wa uhakika umewekwa mipakani
kuzuia mtu aliyeathirika kuingia.
“Mara zote tumekuwa tukichukua hatua stahiki kwa magonjwa ya mlipuko
kama haya, maandalizi ya kutosha yamefanyika kuhakikisha tunakabiliana
nao kama utafika na tahadhari pia zinaendelea kuchukuliwa ikiwa ni
pamoja na kutoa matangazo,” alisema Dk Ulisubisya.
Alisema eneo lililotajwa kuwa na mlipuko wa ugonjwa huo ni la Kaskazini
mwa DRC ambalo ni nadra kufikiwa na wafanyabiashara na madereva wa
malori kutoka Tanzania.
Kwa mujibu wa mtandao wa Aljazeera, eneo hilo ni Likati ambalo lipo kilomita 1,300 kutoka mji mkuu wa DRC, Kinshasa.
Juzi, Waziri wa Afya wa DRC, Oly Ilunga Kalenga alitangaza kuwapo kwa
ugonjwa huo na kwamba umesababisha vifo vya watu watatu tangu ulipoanza
mwishoni mwa mwezi uliopita.
Waziri huyo alieleza kuwa licha ya ugonjwa huo kuwa janga la kitaifa, hakuna sababu ya watu kupata taharuki.
“Si mara ya kwanza kwa nchi yetu kupata janga hili, hatuna sababu ya
kushtuka sana, wizara ya afya inachukua hatua za haraka kukabiliana
nalo,” alisema Kalenga wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari
kuhusu ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu tisa walipimwa na kukutwa na homa kali
iliyoambatana na viashiria vya ugonjwa huo. Msemaji wa Shirika la Afya
Duniani (WHO), Christian Lindmeier aliiambia Aljazeera kuwa kati ya watu
hao tisa, watatu wamefariki na mmoja amethibitika kuwa na ebola.
“Tunatakiwa kuchukua hatua stahiki na za haraka zaidi kuhakikisha
tunawafikia watu walioathirika na kupunguza uwezekano wa ugonjwa huo
kusambaa. Kwa kuwa si mara ya kwanza kwa DRC kufikwa na ugonjwa huu, ni
matumaini yangu kuwa mfumo wa afya wa nchi husika unafahamu kwa kina,
namna ya kukabiliana na janga hilo,” alisema.
Mwakilishi wa WHO huko DRC, Dk Allarangar Yokouide amesema tayari hatua
za awali zimeanza kuchukuliwa na timu ya kwanza ya wataalamu wa afya
imewasili eneo la Likati ambalo ugonjwa huo umeanzia.
Hii ni mara ya nane kwa DRC kukumbwa na ebola, mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2014 na kusababisha vifo vya watu 49.
Tangu mwaka 2013 ugonjwa huo umesababisha vifo vya watu 11,300 na
kuathiri wengine 28,600. Afrika Magharibi, hususan nchi za Guinea,
Sierra Leone na Liberia ndiyo upande uliothiriwa zaidi na ugonjwa huu.
Hadi sasa ugonjwa huo hauna tiba lakini mwishoni mwa mwaka jana, chanjo
ya rVSV-ZEBOV ndiyo iliyoonekana kuwa kinga thabiti ya ebola.
Utafiti uliofanywa na wanasayansi na kuchapishwa kwenye jarida la Lancet
ulionyesha kuwa majaribio ya chanjo hiyo yalikuwa na matokeo chanya kwa
asilimia 100.
Majaribio yalifanyika Guinea, moja ya nchi iliyoathiriwa kwa asilimia kubwa na ebola na chanjo hiyo ni ya kwanza kutoa kinga.
0 comments:
Chapisha Maoni