Wabunge ‘wamewaka’ kuhusu makosa yaliyopo kwenye vitabu vya kujifunzia
na kushauri kuzuia matumizi ya vitabu hivyo ili kuepuka kuendelea
kuwaharibu wanafunzi shuleni.
Makosa yaliyobainika katika vitabu hivyo ni ya kisarufi, mpangilio wa kurasa, tafsiri sisisi na kimantiki.
Wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
kwa mwaka wa fedha 2017/18 bungeni mjini Dodoma jana, walisema vitabu
hivyo vina makosa mengi ya lugha ya Kiswahili na Kingereza jambo ambalo
linaua elimu nchini.
Akisoma maoni ya kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Mbunge wa Viti Maalumu
(Chadema), Suzan Lyimo alisema pia makosa hayo yamekithiri katika
herufi kubwa na ndogo na matumizi ya nukta pacha. “Matatizo hayo yamo
kwenye vitabu vyote hasa kujifunza kusoma, kuandika, kuhesabu, afya na
mazingira, michezo na sanaa,” alisema.
Alitoa mfano wa Kitabu cha Najifunza Kusoma, darasa la Kwanza, ukurasa
wa 99 kinataja kucha kikimaanisha ukucha. Pia kitabu hicho kinaeleza
kumjulisha bila kubadili kwa wima (baada ya kumjumulisha kwa wima bila
kubadili) ukurasa 93 na 94 maneno chupa/ chupa ya chai (yakichanganywa).
Lyimo alisema kitabu cha I Learn English Language, kina matatizo ya
matumizi ya herufi kubwa na ndogo mengi mno karibuni kila ukurasa.
“Inaelekea pia mwandishi hana uwezo wa kutosha wa lugha yenyewe kwani kuna makosa mengi.”
Alitoa mfano wa sentensi ambazo zimekosewa kuwa ni These are my parent,
which is long between a pen and ruler? The driver is taken the police
station, a boy is on bed at hospital na which is the big city of
Tanzania (meaning Capital City).
“Vitabu vya darasa la kwanza vilichelewa kuchapishwa na kuwasilishwa
shuleni. Hata hivyo, baada ya hekaheka nyingi za kuchoma nakala
zilizokuwa na makosa ya mchapishaji, baadhi ya vitabu vya darasa la
kwanza vilitoka Juni, 2016 na baadhi ya Januari mwaka 2017,” alisema.
Alisema kitabu kimoja tu cha darasa la pili kimetoka mwaka huu wa 2017
na kingine cha Kingereza darasa la tatu, I learn English Language.
“Kwa hali hiyo ya utoaji wa vitabu vipya na ucheleweshaji, walimu na
wanafunzi watapata shida kubwa kuutumia mtaala mpya,” alisema.
Lyimo aliitaka Serikali kuzuia matumizi ya vitabu hivyo vyenye makosa
shuleni na pia kuiagiza taasisi elimu kufanya marekebisho ya makosa
yaliyopo kwenye vitabu hivyo na kuvichapisha upya.
Aidha, aliitaka Serikali kufanya uhakiki wa taaluma na weledi wa
watumishi wa Taasisi ya Elimu Tanzania ili kujiridhisha kama wana sifa
stahiki, uwezo na weledi katika kufanya kazi utunzi wa vitabu.
Awali, katika hotuba yake ya bajeti Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema, “Uchambuzi wa kina
unafanyika kwa vitabu vyote vilivyochapishwa mwaka 2016/17 ili kubaini
endapo kuna dosari zilizobainika...”
Alisema mchakato wa kuchukua hatua za kinidhamu kwa mujibu wa taratibu
za utumishi umekwishaanza kwa watumishi ambao vitabu walivyoidhinisha
vimebainika kuwa na makosa.
“Napenda kulihakikishia Bunge lako tukufu kuwa hatua kali zitachukuliwa
dhidi ya wahusika ili kukomesha tabia ya uzembe kwenye kazi muhimu za
Taifa,” alisema.
Alisema baada ya uchambuzi wa vitabu vyote vilivyochapwa kukamilika,
wizara itaamua hatua za kuchukua dhidi ya vile ambavyo vitabainika kuwa
na dosari.
“Nawahakikishia wabunge kuwa wazembe wote waliokuwa sio makini katika
hili kuangalia vitabu hivi tutawaadhibu. Nawahakikishia tutasafisha
taasisi hii (Taasisi ya Elimu Tanzania - TIE),” alisema.
Alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17, wabunge walishika
shilingi katika mshahara wake kutokana na makosa katika vitabu vya
kujifunzia.
0 comments:
Chapisha Maoni