Hakimu Mkazi, Desderi Kamugisha, amejitoa kuendelea kusikiliza moja ya
kesi za uchochezi zinazomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
(Chadema).
Katika kesi hizo, Lema anadaiwa kutoa matamshi yenye chuki na kuibua nia ovu kwa jamii.
Hakimu Kamugisha amejitoa katika kesi ya jinai namba 441/2016 ambayo
Lema anadaiwa kutoa matamshi hayo Oktoba 23, mwaka jana wakati wa
mkutano wa hadhara viwanja vya Shule ya Sekondari Baraa.
“Kiburi cha Rais kisipojirekebisha, Rais akiendelea kujiona yeye ni
Mungu, mwaka 2020 haitafika Mungu atakuwa ameshamchukua maisha yake.
“Rais ana kiburi, Rais kila mahali watu wanaonewa, wafanyakazi wa
Serikali hawana amani, wafanyabiashara hawana amani, watu
wananyanyaswa,” Lema alinukuliwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali,
Martenus Marandu.
Hakimu huyo sasa ataendelea kusikiliza kesi nyingine ya jinai namba
440/2016 ambayo pia inamhusu Lema anayedaiwa kutoa maneno ya uchochezi
yenye kuleta tabaka miongoni mwa jamii Oktoba 22, mwaka jana maeneo ya
Kambi ya Fisi, Kata ya Ngarenaro wakati wa mkutano wa hadhara.
Miongoni mwa maneno ambayo Lema anayodaiwa kuyatoa ni: “Rais Magufuli
akiendelea na tabia ya kudhalilisha demokrasia na uongozi wa upinzani,
iko siku taifa litaingia kwenye umwagaji wa damu.
“Rais yeyote ambaye haheshimu mipaka ya sheria, mipaka ya katiba,
ataingiza taifa katika majanga na umwagaji damu, watu watajaa vifua,
wakiamua kulipuka polisi hawa wala jeshi halitaweza kudhibiti uhalifu
utakaojitokeza.”
Jana kesi hizo mbili zilipangwa kutajwa mbele ya Hakimu Kamugisha
katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, lakini Wakili wa Serikali, Alice
Mtenga, alidai mahakamani hapo kuwa upelelezi umekamilika, hivyo
wanaomba kupangiwa tarehe ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.
Lakini Hakimu Kamugisha alisema haoni busara kuendelea kusikiliza kesi zote wakati kuna mahakimu wengine.
“Nilikuwa na kesi nne za mshtakiwa huyu huyu, sasa zimebaki mbili.
Kwangu sioni kama itakuwa busara kusikiliza kesi zote wakati kuna
mahakimu wengine wanaweza wakasikiliza, najiondoa kwenye kesi namba 441,
nitaendelea na kesi moja namba 440.
“Ukiangalia nature ya kesi ni ile ile moja, mshtakiwa yule yule, kwa
hiyo tutaenda kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi ili apangiwe hakimu mwingine wa
kusikiliza kesi hiyo ili tarehe ya kusomwa maelezo ya awali
itakayopangwa, asikilize hakimu mwingine,” alisema.
Katika kesi hizo, Lema anawakilishwa na Wakili Sheck Mfinanga.
Hata hivyo, mshitakiwa huyo hakuweza kufika mahakamani hapo jana kwa madai kuwa hawakuwa na taarifa za kesi hizo kupangwa.
“Nilikuwa nimesimama kwenye korido ya mahakama asubuhi nikamuona RCO,
nikamuuliza kuna nini akanijibu amekuja kwenye hizi kesi, ndipo nikaamua
kuja mahakamani ila Lema au wadhamini wake hawakufika,” alisema
Mfinanga.
Lema alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Kamugisha Novemba 8, mwaka jana, akikabiliwa na kesi hizo.
Novemba 11, mwaka huo huo, alishindwa kupata dhamana baada ya mawakili
wa Serikali kuwasilisha kwa njia ya mdomo kusudio la kukata rufaa
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kupinga uamuzi wa dhamana uliotolewa na
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.
Lema alikaa mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo kwa zaidi ya miezi minne
kutokana na kukosa dhamana kuanzia Novemba 11 mwaka jana kabla ya
kuachiwa kwa dhamana Machi 3, mwaka huu na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
0 comments:
Chapisha Maoni