Mchanga
wa dhahabu uliozuiwa katika makontena Bandari ya Dar es Salaam, umezua
mjadala bungeni baada ya wabunge wa CCM na Chadema kupingana juu ya
uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli kuyazuia kusafirishwa nje ya nchi.
Hayo
yalitokea jana wabunge walipokuwa wakichangia hotuba ya mapato na
matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje, Kikanda na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki kwa mwaka wa fedha 2017/18, iliyowasilishwa na Waziri Balozi
Augustine Mahiga.
Wakichangia
bajeti hiyo, wabunge wawili wa Chadema, Tundu Lissu (Singida Mashariki)
na Godbless Lema (Arusha Mjini), walisema uamuzi wa Rais Magufuli
utalisababishia taifa hasara na kuwafukuza wawekezaji wa nje.
Naye
Lema alisema amepata taarifa kwamba wamiliki wa mgodi wa Acacia ambao
makontena yao yamezuiwa, wamefungua kesi katika Mahakama ya London,
Uingereza, kulalamikia uamuzi huo wa Serikali.
“Katika
hatua ya kulinda rasilimali ya nchi, ni mwendawazimu anayeweza
asipongeze, lakini lazima tujue ni namna gani unalinda rasilimali hizo
bila kuligharimu taifa.
“Wote
tunafahamu taifa letu lina mgogoro na Acacia Minning ambao kwa sura ya
kwanza, mgogoro huo unajenga hisia za siasa ndani ya nchi na sura ya
pili ya mgogoro huo unapunguza kasi ya wawekezaji wa nje kuja kuwekeza
nchini.
“Leo
(jana) tunapongeza alichokifanya Rais, tuelewe wakati Rais Robert
Mugabe wa Zimbabwe anaanza sera ya kunyang’anya watu mashamba na
kuwakandamiza wawekezaji, alipigiwa makofi na watu wake kama ambavyo
sisi tunapiga makofi leo.
“Matokeo yake leo Zimbabwe hawana noti yao, hawana fedha yao na ni taifa ambalo halina ‘identity’.
“Katika
suala hili ni muhimu mumshauri Rais kwa sababu gharama za uamuzi wake
ni kubwa, ikizingatiwa Acacia leo wamekwenda mahakamani London na kwa
hali ya kawaida, taifa hili litaingia kwenye gharama kubwa kama
tulivyoingia kwenye minofu ya samaki,” alisema Lema.
Tundu
Lissu alisema amekuwa akipinga sera mbaya za uwekezaji tangu mwaka 1999
na kwamba uamuzi alioufanya Rais Magufuli si mzuri na ataupinga kama
ambavyo amekuwa akipinga sera zote ambazo zimelifikisha taifa pabaya.
Alisema uamuzi wa kuzuia makontena hayo unalichafua taifa kimataifa na kuwaogopesha wawekezaji wa nje.
“Suala
siyo Acacia watafanya nini, suala ni watu wote tunaohusiana nao kwenye
uchumi kama Wachina ambao ndiyo taifa kubwa duniani kwa uwekezaji
watafanya nini.
“Fikiria, Jumuiya ya Ulaya, Japan na Marekani watafanya nini kwa sababu ya kuwanyang’anya mchanga wa dhahabu Acacia.
“Sisi
tunazungumza masuala ya diplomasia ya uchumi wakati hatujui lolote
kuhusu diplomasia ya uchumi, ndiyo maana tunafanya haya tunayoyafanya.
Kwa hiyo, waziri nakuomba usikubali hizi kelele kwa sababu hivi sasa
nchi yetu ina hali mbaya kwenye diplomasia.
“Tulichokifanya
ni makosa katika sheria, mikataba ni makosa kwa mujibu wa sheria za
mataifa. Kwa taarifa yenu, gharama tutakazolipa katika jambo hili ni
kubwa kuliko huo mchanga wa Acacia.
“Tutakuwa na kesi kama Zimbabwe, tusishabikie uamuzi uliofanyika kwa sababu tu umefanywa na Rais,” alisema Lissu.
Hatua
hiyo ilimfanya Mnadhimu Mkuu wa Serikali, Jenister Mhagama, aombe
mwongozo kwa mwenyekiti wa Bunge kutokana na lugha kali aliyokuwa
akitumia mbunge huyo (maneno hayo makali hatukuyaandika).
Akijibu
mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, alimtaka Lissu afute
maneno hayo makali, jambo ambalo alilikubali ingawa alisisitiza
kupingana na uamuzi wa Rais Magufuli.
Wabunge wa CCM nao waliamua kujibu mapigo kwa kusema uamuzi uliofanyika ni sahihi kwa kuwa nchi ilikuwa ikiibiwa.
Mbunge
wa Viti Maalumu, Juliana Shonza, aliwashamnbulia Lema na Lissu akisema
hawaaminiki kwa kuwa walikuwa wakimsema vibaya Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa kuwa ni fisadi, lakini alipohamia Chadema wakampigia
kampeni wakati wa Uchaguzi Mkuu.
“Wewe Lissu na Lema, mlikuwa mkimsema vibaya Lowassa ni fisadi, alipokuja kwenu mkaanza kumsafisha. Je, huo siyo uamuzi mbaya?
“Yaani
nyie kila kinachofanywa na Serikali mnaponda kwa sababu mmejipa vyeo
vya mtoto wa kambo. Eleweni nchi hii inahitaji Rais kama Magufuli, nyie
wenzetu endeleeni kutetea wezi, sisi tumeshawazoea.
“Tunamuomba Mheshimiwa Rais aendelee kuchapa kazi, nyie wenzetu muendelee kulalamika, sisi hapa kazi tu,” alisema Shonza.
Mbunge
wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba, alisema uamuzi uliofanywa na Rais
Magufuli ni sahihi na utaigwa na mataifa mengine duniani.
Alisema kuna haja ya Watanzania kushirikiana katika uamuzi huo kwa masilahi ya taifa.
Mbunge
wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi, aliwatoa hofu Watanzania kwa kusema
kama Acacia watakwenda mahakamani, Serikali itakwenda pia kwa kuwa jambo
hilo linawezekana.
“Tutabishana
hapa kutafuta umaarufu kwa sababu kama ni mahakamani tutakwenda pia.
Hata mtu wa kawaida ukimwambia jambo hilo alilofanya Rais atakuunga
mkono na nawaomba tusipinge kila kitu kwa sababu ya itikadi zetu,” alisema Chumi.
Wengine
waliounga mkono uamuzi wa Serikali huku wakitaka Watanzania
washirikiane katika jambo hilo, ni Mbunge wa Viti Maalumu, Mary
Mwanjelwa, Ester Mahawe na Rose Tweve.
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, George Masaju, aliwataka wabunge wasishabikie suala
la wawekezaji hao kwenda mahakamani kwa sababu wakienda huko
hawataishtaki CCM bali wataishtaki Tanzania.
“Nawaomba waheshimiwa wabunge muiunge mkono Serikali katika jambo hili kwa masilahi ya Taifa, nchi ikishtakiwa, haitashtakiwa CCM.
“Kilichofanyika
hakina makosa kwa mujibu wa sheria kwa sababu mkataba una kipengele
kinasema unaweza kupitiwa upya baada ya miaka mitatu, kwa hiyo nawaomba
tushirikiane,” alisema Masaju.
0 comments:
Chapisha Maoni