Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amedai kuwa
waliokuwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA)
wameficha zaidi ya viwanja 34,000.
Lukuvi
ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa CDA kwa miaka kadhaa, pia amesimulia
jinsi wabunge wanne walivyotapeliwa na wafanyakazi wa mamlaka hiyo.
Hivi karibuni, Rais Dk. John Magufuli aliifuta mamlaka hiyo na shughuli zake kuhamishia Manispaa ya Dodoma.
Akizungumza
mjini hapa jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Chama cha Wapima Ardhi
Tanzania (IST), Lukuvi alisema viwanja vilivyopimwa Manispaa ya Dodoma
vilikuwa 60,000, lakini vilivyoonekana ni 26,000 tu huku 34,000 vikiwa
vimefichwa na wafanyakazi wa mamlaka hiyo.
Alisema baada ya kufanya uchunguzi, Serikali imegundua wafanyakazi wengi wameiba viwanja na kuviuza kwa watu wengine.
Lukuvi
alisema kulikuwa na utaratibu wa wafanyakazi wa CDA kuuza viwanja kwa
njia za panya kwa Sh milioni 5, kisha mhusika kupelekewa nyaraka mahali
alipo.
Alisema
kuna wabunge wanne waliuziwa viwanja kwa kutoa Sh milioni 5, lakini
kesho yake rais akaivunja mamlaka hiyo na kujikuta wakitapeliwa.
Lukuvi
alisema wabunge hao walikwenda kumlilia wakitaka kurudishiwa fedha
hizo, lakini jambo la kushangaza hawakuwa na ‘invoice’ ya aina yoyote.
“Sasa wapo watu ambao wamewalipa hizo milioni tano, halafu
kesho yake ikala kwao, Mheshimiwa Rais kaifuta CDA, ndiyo wanakuja
kusema kwangu, watalipwaje? Nimewaambia nipeni risiti wanasema hawana.
Nitawapa kitu gani? Majina ninayo,” alisema.
Alisema wale wote walioiba viwanja hivyo vitawatokea puani, kwani Serikali tayari inayo ripoti nzima juu ya wizi huo.
“Serikali inakosa mapato, sasa tunataka viwanja vipimwe vingi ili tuweze kujiingizia mapato,” alisema.
Aidha
Lukuvi alimbana aliyekuwa Mpimaji Mkuu wa CDA, Frank Mkomochi ambaye
alikuwapo katika mkutano huo, akidai kuwa ni mmoja ya watu waliohuka
kusimamia uuzwaji wa viwanja maeneo mengi.
“Viwanja Itega vilikuwa vinauzwa milioni tano, sasa vinauzwa milioni 25, hili hujalisikia wewe mtu wa CDA?” alimuhoji.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa IST, Martin Chodota, aliomba Serikali kutoa
kipaumbele kwa kampuni za wazawa na kuacha kuwapa nafasi zaidi wapimaji
wanaotoka nje.
0 comments:
Chapisha Maoni