Saa
chache baada ya kuachiwa huru kutokana na amri ya Rais John Magufuli,
Rapa Nay wa Mitego amesema kuwa atayafanyia kazi maoni ya Rais kuhusu
kuboresha wimbo wake kwa namna ya pekee.
Rapa
huyo alitiwa nguvuni wikendi iliyopita kwa tuhuma za kusambaza wimbo
wake wa ‘Wapo’ ambao Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) liliweka wazi
kuwa haufai na una lugha za matusi, lakini mambo yalibadilika baada ya
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe
kueleza kuwa amezungumza na Rais Magufuli na amesema anaupenda wimbo huo
na kwamba ameagiza aachiwe huru na aufanyie maboresho kwa kuongeza
mambo mengine bila kupunguza alichokiimba.
Akizungumzia suala hilo, Nay wa Mitego amesema kuwa ataufanyia marekebisho wimbo huo lakini atahakikisha havuki mipaka.
“Ninalifanyia
kazi, mheshimiwa amesema anaupenda wimbo wangu na anausikiliza, yeye
mwenyewe amewekwa kwenye huu wimbo ni jambo ambalo hawezi kupuuzia na
hiki kinachoendelea labda amefurahishwa, hivyo nitaifanyia kazi kwa
kuongeza mengi makubwa na kwa mapana zaidi bila kuvuka mipaka,” Nay wa
Mitego anakaririwa.
Msanii huyo aliwataka wananchi na vyombo vya habari kuendelea kuzungumza ukweli na kutoa maoni yao lakini wazivuke mipaka.
‘Wapo’
haukuwa wimbo wa kwanza kumuweka matatani Nay wa Mitego kwani baadhi ya
nyimbo zake kama ‘Pale Kati Patamu’ na ‘Shika Adabu Yako’ ziliwahi
kufungiwa na Basata na kupewa onyo kali.