Mfalme Mohammed VI wa Morocco amekubali maombi ya Rais John Magufuli ya kujenga uwanja wa mpira mjini Dodoma ambao utakuwa mkubwa kuliko ule wa Taifa jijini Dar es Salaam sambamba na kujenga msikiti mkubwa jijini humo.
Rais Magufuli aliyasema hayo Ikulu Dar es Salaam jana wakati akitoa shukrani baada ya kukutana na kiongozi huyo, aliyeambatana na wajumbe 150 ambao pamoja na mambo mengine, nchi hizo mbili zilisaini Mikataba ya Makubaliano (MoU) 21.
Akitoa taarifa fupi ya mazungumzo baina yao, Rais Magufuli alisema Mfalme Mohammed VI amekubali kujenga msikiti mkubwa jijini Dar es Salaam sambamba na kujenga uwanja wa mpira mjini Dodoma wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 80 (zaidi ya Sh bilioni 160).
“Katika mazungumzo yetu, nimshukuru Mfalme Mohammed wa Morocco amekubali ombi langu la kujenga msikiti mkubwa hapa Dar es Salaam, na amekubali kwenye mji mkuu Dodoma, atajenga uwanja wa mpira utakaokuwa mkubwa kuliko wa Dar, na thamani yake ni zaidi ya Dola milioni 80,” alieleza Dk Magufuli.
Uwanja wa Taifa umejengwa na Wachina kwa gharama ya Sh bilioni 60 na una uwezo wa kuchukua watu 60,000 waliokaa. Dodoma ambayo ni Makao Makuu ya nchi na Serikali ya Awamu ya Tano imepanga yote kuhamia huko ifikapo mwaka 2020, inao Uwanja wa Jamhuri ambao unamilikiwa na CCM na unachukua watu 8,000.
Mbali na hayo, katika kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili kwenye nyanja ya usalama na ulinzi, Mfalme huyo amekubali kuanzisha programu ya kubadilishana mafunzo baina ya askari wa Tanzania na Morocco na kwa kuanza wiki ijayo askari 150 wa Tanzania watakwenda mafunzoni nchini Morocco.
Katika ziara ya siku tatu ya kikazi ya Mfalme Mohammed VI aliyewasili nchini juzi, akiwa na ujumbe wa wafanyabiashara pamoja na viongozi wengine, wamefanikiwa kufanya makubaliano ya mikataba 21 katika nyanja mbalimbali zikiwamo za kilimo, gesi, madini na na usafiri wa anga.
Mikataba hiyo ni pamoja na Makubaliano ya Jumla katika Ushirikiano wa Uchumi, Sayansi, Ufundi na Utamaduni baina ya Serikali ya Morocco na Tanzania yaliyosainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk Augustine Mahiga na Waziri wa wizara hiyo wa Morocco, Salahddine Mezouar.
Mwingine ni ule wa kuanzishwa kwa Jukwaa la Mashauriano ya kisiasa baina ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na wizara hiyo nchini Morocco, mkataba wa ushirikiano kwenye sekta ya gesi, nishati, madini na sayansi ya miamba, mkataba wa ushirikiano wa usafiri wa anga, mkataba wa ushirikiano kwenye mradi wa mtangamano wa kuwasaidia wakulima wadogo nchini.
Pia mkataba wa makubaliano kwenye sekta ya uvuvi, mkataba wa makubaliano baina na MASEN-Morocco na Wizara ya Nishati na Madini kwa ajili ya maendeleo ya nishati mbadala, mkataba wa ushirikiano baina ya Shirika la Mbolea la Morocco (OCP) na Shirika la Mbolea la Tanzania katika kuendeleza soko la mbolea na kilimo nchini.
Pia mkataba baina ya Bodi ya Utalii Tanzania na Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Ofisi ya Utalii ya Taifa nchini Morocco, Mkataba wa Kundi la Utoaji Mikopo la Morocco na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania, Mkataba baina ya Shirika la Bima la Taifa (NIC) na Shirika la Bima la Morocco.
Mingine ni Mkataba wa Maeneo Maalumu ya Uwekezaji (EPZA) na Kundi la SNTL la Morocco katika ubia wa uendelezaji na utangazaji wa viwanda, mkataba wa usafirishiaji kwenye reli kupitia Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RACO) kwa ajili ya ubia kuendeleza reli ya Mtwara-Mchuchuma/Liganga.
Aidha, mkataba mwingine ni ule wa kuanzishwa kwa Baraza la Biashara baina ya Shirikisho la Wafanyabiashara wa Morocco (CGEM) na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Mkataba wa Mkopo baina ya Benki ya Afrika (BOA) na Hospitali ya CCBRT na mkataba wa mkopo wa BOA na Kampuni ya gesi ya Lake.
Mkataba wa Mkopo wa BOA na Kampuni ya Superstar Forwarders, Mkataba wa Ushirikiano baina ya Kampuni ya OLAM Tanzania na Benki ya Attijariwafa, mkataba wa ubia baina ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)na Benki ya Centrale Populaire ya Morocco, mkataba wa Kitaalamu baina ya Shirikisho la Bima la Morocco na kampuni za bima Tanzania.
Pia mkataba wa ushirikiano baina ya kampuni ya kuchanganya chai ya Morocco na Kampuni ya Afri Tea and Coffee ya Tanzania.
Akizungumzia MoU kwenye usafiri wa anga, Rais Magufuli alisema wamekubaliana nchi hizo mbili kuanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwenda Rabat, mji mkuu wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
“Na sisi tumeanzisha shirika letu kidodokidogo linasuasua, lakini tutakuwa na ushirikiano mzuri na Shirika la Ndege la Morocco, na makubaliano haya yote ni mwelekeo nzuri wa kuijenga Tanzania na kuwa na uchumi unaokua kwa asilimia 7.2,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisema Morocco imepiga hatua kubwa kwenye utalii na kwamba mwaka 2015 ilipokea watalii milioni 10.5 na mwakani wanategemea kupokea watalii zaidi ya milioni 14 na kwamba Tanzania imeshaini makubaliano kwenye sekta hiyo kwa lengo la kuendeleza hifadhi za nchi na kuutangaza utalii.
Aidha, alisema makubaliano yote hayo yamelenga kuijenga Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati wa viwanda na kwamba hilo linawezekana kwa kuwa hata sasa hali ya uchumi wa nchi ni nzuri kwa kuwa unakua kwa asilimia 7.2; na taarifa za uchumi zinaonesha kwenye robo ya pili ya mwaka uchumi umekua kwa asilimia 7.9.
“Tuko kwa ajili ya kuujenga uchumi na niwakaribisheni wageni wetu kutoka Morocco, niwahakikishieni kuwa mko salama na karibuni kuwekeza kwa faida ya nchi hizo mbili ambazo uhusiano wake ulianza tangu enzi za Iban Batutu wa Morocco aliyetembelea Kilwa miaka mingi iliyopita,” alieleza Rais Magufuli.