Aliyekuwa
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema
ataendelea kuwa mtiifu kwa Rais John Magufuli, Serikali na Chama cha
Mapinduzi tofauti na maneno yanayosemwa mitandaoni.
Tangu
alipoachwa kwenye mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, Machi 23,
kumekuwa na taarifa nyingi feki kwenye mitandao ya kijamii kuhusu
kuenguliwa kwake zikidaiwa kutolewa na mbunge huyo wa Mtama ambazo hata
hivyo, amekuwa akizikanusha.
Akizungumza
jana wakati akikabidhi ofisi kwa waziri mpya wa wizara hiyo, Dk
Harrison Mwakyembe katika ofisi za wizara hiyo mjini hapa, bila kutaja
maneno hayo ya mitandaoni, Nape alisema ataendelea kumuunga mkono Rais
katika dhamira yake njema ya kuleta mageuzi nchini.
“Heshima aliyonipa Rais ni kubwa mno na nitaendelea kumuunga mkono katika dhamira yake njema ya kuleta mageuzi nchini” alisema.
Alimshukuru
Rais kwa kumpa dhamana ya kusimamia wizara hiyo kwa miezi 15 baada ya
kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya kwanza. “Nitaendelea kutoa
ushirikiano kwa wizara hii kwa sababu mimi ni mdau mkubwa wa sekta
hiyo,” alisema.
Waziri
Mwakyembe alisema ataendeleza mazuri yote yaliyofanywa na Nape katika
kuimarisha wizara hiyo na atahakikisha wizara hiyo inakuwa ya mfano
nchini.
Alimsifu Nape akisema katika kipindi kifupi alichokaa katika wizara hiyo amefanya mabadiliko na watu wameanza kuifahamu.
Nape
aliondolewa katika nafasi hiyo siku moja baada ya kamati aliyounda
kuchunguza tukio la kuvamiwa kwa ofisi za Clouds kumkabidhi ripoti.
Mara
baada ya kupewa ripoti hiyo, Nape aliahidi kuikabidhi kwa mamlaka zake
za juu akizitaja kuwa ni Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais lakini
asubuhi ya siku iliyofuata aliondolewa katika nafasi hiyo.
Makabidhiano
hayo yalishuhudiwa na viongozi wengine wa wizara hiyo, naibu waziri,
Anastazia Wambura, katibu mkuu, Profesa Elisante Ole Gabriel na naibu
katibu mkuu, Nuru Millao.
==>Msikilize Hapo Chini Akiongea