Maofisa
waandamizi wa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Tawi la
Kariakoo, Dar es Salaam na mfanyakazi mmoja, wamepandishwa kizimbani
katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, wakikabiliwa na makosa ya kujipatia
Sh milioni 66 kwa njia ya rushwa.
Maofisa
hao ni Liberatus Rugumisa (30), Keneth Mawere (29) na mfanyakazi mmoja
Nassoro Nassoro (42) wote wakazi wa Kigamboni, Dar es Salaam.
Mwendesha
Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),
Lupyana Mwakatobe alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi, Adelf Sachore kuwa
washitakiwa hao walitenda makosa hayo kwa madai ya kumpunguzia kodi
mfanyabiashara Humphrey Lema kinyume na sheria zao.
Katika
mashitaka ya kwanza, Mwakatobe alidai kuwa Novemba 18 mwaka huu, maeneo
ya ofisi za TRA Kariakoo wilayani Ilala, Rugumisa na Mawere wakiwa
waajiriwa wa mamlaka hiyo, walijipatia rushwa ya Sh milioni 50 kutoka
kwa Lema kwamba wangempunguzia Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
Pia,
alidai kuwa Novemba 23 mwaka huu, katika duka la kubadilishia fedha la
Cate lililopo kati ya mtaa wa Nyamwezi na Donge, Kariakoo wilayani
Ilala, walijipatia Sh milioni 10 kutoka kwa mfanyabiashara huyo kwa
madai watampunguzia VAT.
Katika
mashitaka ya tatu ambayo yanawakabili washitakiwa wote, inadaiwa
washitakiwa walijipatia rushwa ya dola za Marekani 2,744 sawa na Sh
milioni sita kutoka kwa Lema kwamba wangeweza kumpunguzia VAT, kinyume
na maadili ya kazi hiyo.
Washitakiwa
walikana mashitaka hayo na kurudishwa rumande kwa kushindwa masharti ya
dhamana. Hakimu Sachore alitaja masharti hayo kuwa ni wadhamini wawili
kutoka taasisi inayotambulika, watakaosaini bondi ya Sh milioni mbili.
Hata hivyo, aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 27 mwaka huu kesi hiyo
itakapotajwa.