Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Leo
tarehe 30 Aprili, 2018 Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amezindua
ripoti ya Nane ya ulinganishi wa mapato ya Serikali na malipo ya kampuni
za madini, mafuta na gesi asilia kwa mwaka wa fedha 2015/16
iliyoandaliwa chini ya Mpango wa Uhamasishaji Uwazi katika Mapato ya
Madini, Gesi Asilia na Mafuta Tanzania (TEITI) kwa kushirikiana na
Mtaalam Mwelekezi, Boas & Associates na MM Attoneys.
Akizungumza
katika uzinduzi wa ripoti hiyo uliofanyika jijini Dar es Salaam na
kukutanisha wawakilishi kutoka Kamati ya TEITI, Wizara ya Madini,
makampuni ya mafuta na gesi, Waziri Kairuki amepongeza Kamati ya TEITI
na Sekretarieti kwa mchango wake katika uandaaji wa ripoti hiyo.
Mbali
na Pongezi hizo, Kairuki ameiagiza Kamati ya TEITI kuongeza nguvu
katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa mpana wa umuhimu na
wajibu wa TEITI kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na warsha
mbalimbali pamoja na vipindi vya redio na televisheni.
Amesisitiza
kuwa, kipaumbele kiwekwe kwenye maeneo yaliyozungukwa na shughuli za
utafutaji na uzalishaji wa madini, mafuta na gesi asilia na kupata
taarifa ndani ya kipindi cha miezi sita.
Awali
akielezea ripoti hiyo, Kairuki amesema kuwa ripoti hiyo inahusu
tathmini ya mapato ya madini katika kipindi cha kuanzia tarehe 1 Julai,
2015 hadi tarehe 30 Juni, 2016 na kufafanua kuwa jumla ya shilingi
434,627,874,380 zilipokelewa serikalini kutoka kwenye kampuni 55 za
madini, mafuta na gesi asilia zilizoshiriki zoezi la ulinganishi.
Hata
hiyo amesema taarifa inaonesha kuwa kampuni zililipa kiasi cha shilingi
465,164,747,725 za kitanzania serikalini na kusababisha tofauti kati ya
malipo kuwa ni pungufu ya shilingi 30,536,873,345 za kitanzania chini
ya kiasi ambacho Serikali imekiri kupokea.
“
Ni lazima tufahamu ni vipi imejitokeza tofauti hii na ninachukua fursa
hii kuelekeza taarifa hii kupelekwa kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali kwa ajiili ya uchunguzi kama kifungu 18(1) cha Sheria ya TEITI
ya mwaka 2015 kinavyotaka,” alisema Waziri Kairuki.
Katika
hatua nyingine, Waziri Kairuki amefafanua kuwa ripoti imeonesha kuwa
sekta ya madini imechangia zaidi kwa asilimia 85 na sekta ya mafuta na
gesi ikionyesha kuchangia asilimia 15 ya mapato ya Serikali chini ya
Sekta ya Madini kwa mwaka 2015/16
Akielezea
mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya madini, Kairuki
amesema kuwa ili kuhakikisha madini yanakuwa na mchango mkubwa katika
ukuaji wa uchumi, Serikali imeanza kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja
na kufanya mabadiliko ya Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.
Ametaja
hatua nyingine ambayo ni endelevu kuwa ni kufanya tathmini ya jinsi
gani nchi inapata mapato yake kwenye sekta ya madini kutokana na hatua
mbalimbali zinazochukuliwa.
Ameendelea
kusema kuwa jukumu linafanywa na taasisi mbalimbali za Serikali lakini
TEITI nayo inatekeleza jukumu husika kwa kuhakikisha taarifa za mapato
ya madini zinatolewa kwa uwazi kwa wananchi na wadau mbalimbali katika
Serikali, Sekta Binafsi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali.
Wakati
huo huo akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Madini, Profesa Simon Msanjila amesema kuwa mara baada ya ripoti
kuzinduliwa na kukabidhiwa kwa Kamati ya TEITI hatua inayofuatia ni
kamati ya TEITI kuwasilisha ripoti hiyo kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali ili achukue hatua kwenye hoja zilizotokana na ripoti hiyo.
Profesa
Msanjila amezitaka kampuni nyingine ambazo hazikushiriki katika kipindi
cha ukaguzi kujitokeza katika ukaguzi unaofuata ili takwimu halisi za
mapato zifahamike.
Aidha,
ametumia fursa hiyo kukaribisha kampuni nyingine zenye nia ya kuwekeza
kwenye sekta ya madini kujitokeza kwa wingi ili sekta ya madini iwe na
mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
0 comments:
Chapisha Maoni