WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza Wizara, mashirika na taasisi zote za
Serikali na binafsi zianze kutumia nishati mbadala ili kuondoa kabisa
matumizi ya kuni na mkaa.
“Wizara,
taasisi na mashirika yote ya Serikali na binafsi pamoja na vikundi vya
uzalishaji wanaotumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia au
shughuli za uzalishaji waanze kutumia nishati mbadala ili matumizi ya
mkaa yaishe na ikiwezekana yatoweke kabisa,” amesema.
Ametoa
agizo hilo leo (Alhamisi, Mei 31, 2018) wakati akizungumza na mamia ya
wananchi na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam walioshiriki uzinduzi wa
maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja
jijini Dar es Salaam. Kaulimbiu ya mwaka huu ni: “Mkaa ni Gharama: Tumia
Nishati Mbadala.”
Waziri
Mkuu amesema teknolojia bora ya uzalishaji wa mkaa mbadala ambayo
ameiona kwenye maonesho hayo, ikuzwe na kusambazwa kote nchini ili
kuwawezesha wananchi walio wengi waachane na matumizi ya mkaa wa kawaida
na badala yake watumie mkaa-mbadala kwa lengo la kuhifadhi misitu na
kupunguza uharibifu wa mazingira.
Ili
kufanikisha matumizi ya teknolojia hiyo, Waziri Mkuu amesema vibali vya
ujenzi wa majengo makubwa na taasisi kama shule, vyuo, hospitali navyo
pia vianze kuzingatia ufungaji wa mifumo ya nishati ya gesi kwa ajili ya
matumizi ya kupikia ili kurahisisha upatikanaji na matumizi ya nishati
mbadala katika taasisi na majengo makubwa.
“Wahandisi
na wachoraji ramani za majengo waweke njia za kupitisha kwenye michoro
yao ili ujenzi wa nyumba na majengo haya ukikamilika, watumiaji waweze
kutumia teknolojia hiyo,” amesema.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu amesema Mkoa wa Dar es Salaam ni lazima ubadilike
na uachane na matumizi ya mkaa. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mkoa huo
unatumia tani 500,000 za mkaa kwa mwaka.
“Viongozi
wa mkoa na wilaya ondokeni hapa na hili kama ajenda ya mkoa wa Dar es
Salaam, mkaifanyie kazi na Wizara pia ifuatilie mmetekeleza kwa kiasi
gani. Jitihada zilizofanywa na Jiji la Dar es Salaam kupitia kwa
Mstahiki Meya, za kuanza kuwapa mtaji wajasiriamali hawa wanaotengeneza
teknolojia mpya ni lazima ziigwe na nyie kwenye Manispaa zenu.”
“Meya
ametoa fursa na amewaanzishia, na ninyi sasa endeleeni. Tengenezeni
bajeti kupitia Mabaraza ya Madiwani na muwaunge mkono wajasiriamali
wanaotengeneza haya majiko kwa kuwapa teknolojia hii kwenye maeneo yenu.
Wanaotengeneza mashine za mkaa mbadala, wawezeshwe watengeneze mashine
nyingi zaidi na zije kila Manispaa, ili kila Manispaa ianze kutumia
teknonolojia hiyo kupikia,” alisisitiza.
Amewaagiza
Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Manispaa za Jiji la Dar es Salaam
wafuatilie kwa karibu usambazaji wa teknolojia hiyo.
Kwa
upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na
Mazingira), January Yusuf Makamba amesema hali ya mazingira hapa nchini
ni mbaya licha ya kuwa haionekani kwa haraka na watu waishio mijini.
“Hali
ya mazingira nchini mwetu ni mbaya sana na inawezekana watu wanaoishi
Dar es Salaam hawaioni kwa haraka kwa sababu mahitaji yao yote
wanayapata sokoni na madukani,” alisema.
“Wenzetu
wa mikoani na vijijii wanaotegemea mvua na udongo wenye rutuba
wanataabika kwa sababu kipato chao kinaathirika kutokana na uharibifu wa
mazingira,” alisema.
Alisema
mazingira yanafungamana na utalii, kilimo, ufugaji, nishati, maji na
kwamba maendeleo ya nchi pia yamefungamana moja kwa moja na mazingira.
“Asilimia 90 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa kupikia lakini
asilimia 70 ya mkaa wote unaozalishwa nchini Tanzania, unatumika jijini
Dar es Salaam,” alisema.
Waziri
Makamba alisema taasisi za Serikali kama vyuo, magereza, hospitali na
shule zinaongoza kwa matumizi ya kuni na mkaa na hivyo kuchangia
uharibifu mkubwa wa mazingira.
Akitoa mfano, alisema Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kina wanafunzi wapatao 30,000 na kinalazimika kuandaa milo mitatu kila siku.
“Chuo
hiki kina migahawa tisa, kule nyuma kumejaa magogo ya kuni. Kuna
mgahawa mmoja mdogo unatumia magunia 17 ya mkaa kwa siku, sasa huo
mkubwa unatumia magunia mangapi?” alihoji.
Maadhimisho
hayo yaliyozinduliwa leo, yataendelea hadi Juni 5, mwaka huu ambayo ni
siku ya kilele. Pia wiki nzima kutakuwa na makongamano, midahalo na
mjadala wa kitaifa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
0 comments:
Chapisha Maoni