Skip to content
Mjumbe
wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa amesema ataingia Ikulu baada
ya miaka minne ijayo na rafiki yake T.B Joshua amemtabiria kuwa Serikali
ijayo itaongozwa na Chadema.
Lowassa,
ambaye alishika nafasi ya pili katika kinyang’anyiro cha urais mwaka
jana, ameshaonyesha nia ya kuingia tena kwenye mpambano huo wakati wa
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Akizungumza na viongozi na wanachama wa Chadema mkoani Tabora, waziri huyo mkuu wa zamani alisema ana uhakika wa kuingia Ikulu bila ya umwagaji wa damu.
Huku
akishangiliwa, Lowassa ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema,
aliwashukuru wana Tabora na Watanzania kwa ujumla kwa kura walizompa
katika uchaguzi mkuu uliopita.
Lowassa aliwaeleza wanachama na viongozi wa chama hicho kuhusu utabiri wa T.B.Joshua na angalizo alilompa.
Alisema
muhubiri huyo maarufu barani Afrika anayefanya shughuli zake nchini
Nigeria na ambaye alikuja nchini mara baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita,
alimpa angalizo kuwa ili washinde ni lazima wawe wamoja, washikamane na
kuwa majasiri.
“Najua
waandishi wa habari wataandika, lakini sijali rafiki yangu Joshua
ametabiri Serikali ijayo ya Tanzania itaongozwa na Chadema,” alisema.
Lowassa
amekuwa akienda Lagos, Nigeria kuhudhuria ibada za T.B Joshua
anayeongoza kanisa la The Synagogue Church of All Nations na ambaye
amekuwa akitabiri matukio makubwa kutokea sehemu mbalimbali duniani.
Katika
kudhihirisha urafiki wake na T.B Joshua, Lowassa alisema katika
mahafali ya wanafunzi wa vyuo vikuu ambao ni wanachama wa Chadema
yaliyofanyika jijini Dar es Salaam katikati ya mwaka, kuwa CCM ilimuita
nabii huyo nchini baada ya uchaguzi ili amshawishi akubali matokeo.
Lowassa
aliwaambia wanafunzi hao kuwa alimweleza T.B Joshua matukio yote
yaliyotokea wakati wa uchaguzi na hivyo kumfanya nabii huyo aamue
kutohudhuria sherehe za kuapishwa.
Hata
hivyo mwenyewe T.B Joshua hajathibitisha kauli hiyo ya Lowassa. Kuhusu
Tabora, Lowassa alisema ni mkoa wa kihistoria na ndio kitovu cha siasa
nchini kwa kuwa ndiko kulikoanza vuguvugu la mapambano ya kudai uhuru na
kwamba una heshima yake kisiasa.
Aliwataka viongozi na wanachama wa Chadema kuhakikisha wanalinda heshima hiyo kwa kuifanya Chadema kuongoza nchi.
Lowassa,
ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu, aliwaeleza wanachama na viongozi kuwa
ruzuku ni fimbo ya kuwagombanisha wanachama katika vyama vya siasa.
Aliwataka wanachama na viongozi kuhakikisha hawagawanywi na ruzuku na kwamba waulinde Ukawa na wakatae kuvurugwa.
“Vyama vingi nchi za Afrika hugawanywa kwa fedha za Serikali zilizopo madarakani, jambo ambalo sisi tulikatae,” alisema.
Aliwaleza wanachama hao ruzuku inatolewa ili wanachama wabaki wakigombana na kushindwa kufanya mambo ya msingi.
Akiizungumzia
elimu, Lowassa alisema CCM inapata ushindi katika maeneo ambayo yapo
nyuma kielimu na kuitaja mikoa ya Singida, Mtwara, Lindi, Dodoma na
Tabora.
Alieleza
kuwa mikoa iliyo nyuma kielimu ndio ngome ya chama tawala na kwamba
ndio maana anaposisitiza elimu itolewe bure, anajua anachomaanisha.
Mbunge
huyo wa zamani wa Monduli aliambatana na mjumbe mwingine wa Kamati Kuu
ya Chadema, Mwita Waitara, ambaye katika hotuba yake alisisitizia suala
la tume huru ya uchaguzi.
Waitara, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Ukonga aliwataka wanachama wa Chadema kusimama imara kudai tume huru.
Awali,
mratibu wa Chadema wa Kanda ya Magharibi, General Kaduma alisema watu
watakaojaribu kuwagawa wanachama, watawekwa pembeni ili wawaache wengine
waendelee kuongoza chama.
Alisema
madhumuni ya mikutano ya ndani ya chama hicho inayoendelea nchi nzima
ni kupanga mambo yanayohusu ujenzi wa chama chao na kuwakumbusha
viongozi mambo ya msingi ya chama.
Install Application ya JUNGUKUULEO Uweze Pata Habari Kirahisi Zaidi
xxxxxxxxxxxxx