Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imemtaka yeyote anayeona kuwa kauli
iliyotolewa na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Maombezi (GRC), Anthony
Lusekelo maarufu Mzee wa Upako imetishia maisha yake, afungue kesi.
Kamanda
wa kanda hiyo, Simon Sirro aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati
akijibu maswali ya waandishi wa habari waliotaka kujua hatua polisi
waliyoichukua kutokana na kauli aliyoitoa Mchungaji huyo kwamba
waandishi waliomwandika vibaya watakufa kabla ya Machi mwakani.
“Kama
kuna mtu anaona katishika na kauli hiyo aje afungue kesi milango iko
wazi. Kama kuna mwandishi yeyote anayeona ametishika na kauli hiyo aje,
kesi ikifunguliwa tutaifanyia kazi kwa sababu hadi sasa hakuna
aliyelalamika,” alisema.
Kauli
ya Mzee wa Upako aliitoa katika mahubiri yake ya Jumapili ikiwa ni
mwendelezo wa majibu yake kutokana na tuhuma zilizoandikwa kwenye baadhi
ya vyombo vya habari kwamba alimfanyia fujo jirani yake.
Wakati
huo huo, Sirro alisema kuwa wanaendelea na uchunguzi wa madai ya
kupotea kwa Bernard Saanane ambaye ni kiongozi wa Chadema. Kiongozi huyo
anadaiwa kupotea tangu Novemba 18.
“Kuna
watu wanasema wanataka ile miili ichunguzwe… lile ni tukio la Pwani na
mwenye wasiwasi anaruhusiwa kuwasiliana na uongozi wa kule kwa sababu
ule ni mkoa mwingine,” alisema.
Hata
hivyo, alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii
Forum, Maxence Melo alisema atazungumzia suala hilo Ijumaa.