Donald Trump alisindikizwa na familia yake alipopanda jukwaani kutoa hotuba baada yake kushinda urais Marekani. Unawafahamu wake zake na watoto?
1. Barron Trump ndiye mwana wa pekee wa Donald na mke wake wa sasa Melania. Ingawa alijitokeza katika mikutano kadha ya kampeni, mvulana huyu wa miaka 10 hajakuwa akioneshwa sana hadharani. Hucheza gofu na babake na anaaminika kuzungumza Kislovenia kwa ufasaha. Mamake alitoka Slovenia.
2. Melania Trump, ni mwanamitindo wa zamani, mzaliwa wa Slovenia, ambaye aliolewa na Donald Trump Januari 2005. Alijitokeza na kumtetea mumewe baada ya kanda ya video kutokewa wakati wa kampeni na kumuonesha akijitapa kuhusu kuwadhalilisha kimapenzi wanawake. Julai 2016, aligonga vichwa vya habari baada ya kutoa hotuba mkutano mkuu wa kitaifa wa chama cha Republican, baada ya Bw Trump kuidhinishwa kuwania urais, ambapo alituhumiwa kuchukua maneno mengi kutoka kwa hotuba iliyotolewa na Bi Michelle Obama mwaka 2008. Alipoulizwa na CNN mwezi Oktoba ni jambo gani angetaka kubadilisha kwa mumewe, alijibu: "Kuandika kwenye Twitter."
3. Jared Kushner ni mume waIvanka, binti mkubwa wa Donald. Bw Kushner ni mwana wa mfanyabiashara tajiri wa New York anayefanya biashara ya nyumba ya ardhi. Amekuwa pia mmiliki wa gazeti la kila wiki la Observer jijini New York kwa miaka 10. Kushner, ambaye ni Myahudi, anadaiwa kuwakera watu wa familia yake alipoandika makala kutetea hatua ya Donald Trump kutumia Star of David (Nyota ya Daudi ambayo ni nembo ya Wayahudi) kwenye ujumbe kwenye Twitter akimshambulia Hillary Clinton. Akiandika kwenye gazeti hilo lake, alisema: "Shemeji yangu hana chuki dhidi ya Wayahudi". Aliendelea: "Tofauti kati yangu na wanahabari na watu wa Twitter wanaodhani huu ni wakati mwafaka sana wa kumshambulia shemeji yangu ni rahisi. Mimi namfahamu (ni mtu wa aina gani), wao hawamfahamu.
4. Ivanka Trump labda ndiye mwana wa Donald Trump anayefahamika zaidi na watu. Ndiye binti wa pekee wa mke wa kwanza wa Trump, Ivana. Alikuwa mwanamitindo mzamani lakini sasa ni makamu wa rais wa shirika la The Trump Organization na pia jaji katika kipindi cha runinga cha babake cha The Apprentice. Alibadili dini na kujiunga na didi ya Kiyahudi baada ya kuolewa na Jared mwaka 2009. Kwenye hotuba mkutano mkuu wa kitaifa wa chama cha Republican, aliunga mkono babake na kusema anatetea haki za wanawake. "Kama mama, wa watoto watatu, najua jinsi ilivyo vigumu kulea familia. Na najua hilo kwa sababu nimebahatika kuliko watu wengi. Familia nyingi Marekani zinahitaji usaidizi. Sera ambazo zinawaruusu wanawake wenye watoto kufanikiwa hazifai kuwa jambo nadra sana, zinafaa kuwa kawaida."
5. Tiffany Trump ni binti wa Donald Trump kutoka kwa mke wake wa pili Marla Maples, mwigizaji wa zamani na nyota wa TV. Hutumia sana Twitter na Instagram, na ujumbe wake mitandao ya kijamii huashiria maisha ya kifahari. Amekuwa sana hajitokezi kwenye kampeni lakini alisifiwa na babake kwa kutoa hotuba nzuri sana wakati wa kongamano kuu la chama cha Republican, ambapo alisema babake ni mtu mwenye sifa za kuwasaidia na kuwahimiza wengine.
6. Vanessa Trump, ambaye jina lake la kuzaliwa ni Haydon, aliolewa na Donald Trump Jr mnamo Novemba 2005. Wawili hao wamejaliwa watoto watano, akiwemo Kai, mwenye umri wa miaka minane (pichani). Vanessa alianza uanamitindo akiwa mtoto na wakati mmoja alikuwa mpenzi wa Leonardo DiCaprio. Yeye huhudumu katika kamati tendaji ya wakfu wa mlamu wake Eric. Huwa na bunduki nyumbani - na kwa mujibu wa mahojiano yake na SilencerCo, kampuni inayounga vifaa vya kunyamazisha mlio wa bunduki, pia ana leseni ya kubeba silaha na hufanya mazoezi ya ulengaji shabaha mara kwa mara.
7. Kai Trump ndiye kifungua mimba waVanessa na Donald Jr, ambao wamejaliwa watoto watano.
8. Donald Trump Jr ndiye mwana wa kwanza wa kiume wa Donald Trump na mke wake wa kwanza Ivana. Kwa sasa ni makamu wa rais mtendaji wa shirika la The Trump Organization. Alimuoa Vanessa Haydon baada ya wawili hao kukutanishwa katika hafla ya maonyesho ya mitindo na babake. Safari yake ya kupata umaarufu imekabiliwa na utata kiasi. Upendo wake, na nduguye Eric, wa kuwinda wanyama wakubwa ulikosolewa baada ya picha kutolewa zikiwaonesha wakipigwa picha na wanyama waliouawa, wakiwemo chui na mamba. Donald Jr alikuwa pia ameshika mkia wa ndovu uliokuwa umenyofolewa kutoka kwa ndovu.
9. Eric Trump ndiye mwana wa tatu wa Trump na Ivana. Sawa na nduguze, yeye pia ni makamu wa rais mtendaji wa Trump Organization. Yeye pia ni rais wa Trump Winery jimbo la Virginia na husimamia klabu za gofu za Trump. Mwaka 2006, alianzisha wakfu wa Eric Trump Foundation, ambao umeahidi kutoa $28m kwa hospitali inayofanya utafiti wa kuwasaidia watoto wanaougua magonjwa hatari. Kama ndiguye Donald Jr, Eric alikosolewa baada yake kufanya ziara ya uwindaji Zimbabwe mwaka 2010. Huenda alivunja sheria ya uchaguzi siku ya uchaguzi alipopakia kwenye Twitter picha ya karatasi yake ya kura, akisema "heshima kubwa kumpigia kura babandu."
10. Lara Yunaska, ni mwandaaji vipindi wa zamani katika runinga na hushiriki mashindano ya mbio za farasi. Aliolewa na Eric mwaka 2014. Aliumia vifundo vya mikono yake miwili akipanda farasi wiki mbili kabla ya harusi yake, sherehe iliyoongozwa na Jared Kushner. Wawili hao hawana mtoto, lakini wana mbwa kipenzi. Kama mtetezi wa haki za wanyama, haijulikani msimamo wake kuhusu upendo wa mumewe wa kuwinda wanyama. Yeye pia hushirikishwa katika shirika Trump Foundation, moja ya nyakfu kubwa zaidi za hisani nchini Marekani. Lara aliambia Fox News mnamo 6 Novemba: "Wanawake wamekereka sana kwamba mgombea kama Hillary Clinton anaamini wanafaa kumpigia kura kwa sababu eti yeye na wao ni wa jinsia moja ... Inashangaza, inakera na inaudhi".