MSHTAKIWA wa kwanza, Nzira Luhemeja (42), alitokwa na haja ndogo mahakamani baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 40 jela kwa kukutwa na nyama ya Kiboko kilo 70 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi.
Tukio hilo lilitokea juzi katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, ambapo Hakimu Odira Amwol alimhukumu pia Vicenti Makelele (32) katika kesi moja iliyowakabili wakazi hao wa Kijiji cha Mwamkulu wilayani humo.
Hakimu Amwol alisema anawatia hatiani washtakiwa hao baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka uliokuwa unaongozwa na Mwendesha mashtaka wa Tanapa, Elieza Chitalya, ambao ulikuwa na mashahidi wanne huku washtakiwa wakijitetea wenyewe.
Wakati akisoma hukumu hiyo, Mahakama ililazimika kusimama kwa dakika 10 baada ya mshtakiwa wa kwanza Luhemeja kutoa haja ndogo huku jasho likimtiririka.
Polisi walimwondoa kizimbani mshtakiwa huyo na kumpeleka chooni na baadaye kesi iliendelea.
Awali katika kesi hiyo, mwendesha mashtaka alidai kuwa washitakiwa walikamatwa na askari wa wanyamapori waliokuwa doria Julai 21 mwaka huu, katika eneo la Mto Katuma ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi wakiwa na nyama hiyo yenye uzito wa kilo 70, yenye thamani ya Sh milioni tatu.
Katika utetezi wao, mshtakiwa wa kwanza, Luhameja alikana kukamatwa na nyara hizo za Serikali na kudai kuwa yeye alikamatwa wakati akiwa njiani anakwenda kuoga katika mto Mafunsi nje ya Hifadhi ya Katavi.
Mshtakiwa wa pili, alidai kuwa hakukamatwa na nyama hiyo ya Kiboko bali askari wa Tanapa walimkamata wakati akiwa njiani kwenda kuvua samaki Mto Mafunsi.
Kabla ya hukumu kutolewa, hakimu aliwapa washtakiwa nafasi ya kujitetea.
Katika ombi lake, mshitakiwa wa kwanza aliomba mahakama imwachie huru kwani hakutenda kosa hilo bali alisingiziwa na askari wa Tanapa, kwani hata majirani zake wanajua hana tabia hiyo.
Kwa upande wake, mshtakiwa wa pili aliiomba mahakama isimpe adhabu ya kifungo, bali impe adhabu ya kulipa faini kwani ana wategemezi wengi akiwamo mzazi wake ambaye ni mzee sana.
Katika hukumu hiyo, washtakiwa wote wawili walihukumiwa kwenda jela miaka 20 kila mmoja